ACT Wazalendo yasusia vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa, yataja sababu

Muktasari:
- Wakati ACT Wazalendo wakitoa msimamo wa kususia, vyama vingine vya siasa vimesema vitashiriki mkutano huo huku vikisema huwezi kususia bila kujua linaenda kuzungumzwa jambo gani.
Dar es Salaam. Kamati ya Uongozi Taifa ya chama cha ACT Wazalendo imetangaza kutoshiriki vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa vinavyoanza kesho Machi 12 hadi 13, 2025 huku kikitaja sababu tatu za kufikia uamuzi huo kikidai vikao hivyo kugeuka jukwaa la kuhalalisha na kusafisha uchafuzi na wizi katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Sababu nyingine walizozibainisha ni baraza hilo linaloratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupoteza uhalali baada ya kushindwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na vyama vya siasa, kwa ajili ya kujenga na kukuza misingi ya demokrasia ya vyama vingi.
Vilevile, Serikali kupuuza maazimio ya baraza hilo ya kuboresha uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika Oktoba 11, 2024 jijini Dodoma na kutanguliwa na vikao vya kamati za baraza na kamati ya uongozi ya baraza.
Wakati ACT Wazalendo wakieleza hayo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Juma Ali Khatibu amewajibu akisema kama wameamua kususia huo ni uamuzi wao lakini baraza bado linaendelea na uhai wake wa kufanya vikao kwa kuwa lipo kwa mujibu wa sheria.
“Baraza linaundwa na vyama 19, ikitokea chama kimoja au vitatu vinasusia, huo ni uamuzi wao. Baraza litaendelea na liko kisheria na Serikali imekuwa sikivu. Wao si wa kwanza, mbona hata Chadema waliwahi kususa lakini mwishoni mwishoni waliamua kurejea kundini,” amesema.
Amesema uamuzi wao hauwatishi huku akieleza wao wanajua chama hicho kinafanya siasa na wanatafuta umaarufu (kiki) wamewasikia lakini wataendelea na wajumbe wote wameshafika Morogoro kwa ajili ya kikao hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 11, 2025 na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, uamuzi wa kususia kikao hicho uliazimiwa kwenye kikao cha kamati kuu kilichofanyika Machi 10, 2025.
“Hatutashiriki kwa sababu Baraza la Vyama vya Siasa linaloratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini limepoteza uhalali baada ya kushindwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na vyama vya siasa, kwa ajili ya kujenga na kukuza misingi ya demokrasia ya vyama vingi nchini, ambalo lilikuwa ndiyo lengo lake kuu wakati linaanzishwa,” amesema.
Amedai limegeuzwa kuwa jukwaa la kutumika kuhalalisha na kusafisha uchafuzi na wizi katika chaguzi kama ilivyofanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, uchaguzi mkuu 2020 na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Wito wa ACT Wazalendo
Ado amesema katika taarifa yake kwamba chama hicho kinaitaka Serikali kama kweli inataka walichukulie baraza hilo kuwa ni chombo makini kushiriki shughuli zake, basi iweke mezani kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya kupata tume huru ya uchaguzi na marekebisho mengine ya sheria za uchaguzi.
“Tunataka maboresho ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na pia mabadiliko madogo ya Katiba yatakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki. Chama kimewasilisha tena kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa uchambuzi wake wa kina wa masuala yanayohitaji kufanyiwa maboresho, ili kuhakikisha uchaguzi mkuu 2025 unakuwa huru na wa haki,” amesema.
Vyama vingine kushiriki
Wakati ACT Wazalendo wakitoa msimamo wa kususia vyama vingine vya siasa vimesema vitashiriki mkutano huo, huku vikisema huwezi kususia bila kujua linaenda kuzungumzwa jambo gani.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi (Bara), Joseph Selasini amesema chama hicho kitashiriki mkutano huo na yeye mwenyewe yupo Morogoro kushiriki.
Selasini amesema ACT Wazalendo kususia kikao hicho hawajui wanachokitaka, kwani ulikuwa wakati mwafaka kwa kuungana na vyama vingine kujipanga na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohamed Abdallah amesema watashiriki kwa kuwa wana mambo mengi wanayaangalia katika uchaguzi ujao.
“Si kila jambo la kususia, CUF kama kawaida huwa tunashiriki na tunapenda mambo kupata usuluhishi kupitia mikutano na si kususia inaweza kuwa na hasara,” amesema.
Mwenyekiti wa TLP, Richard Lyimo amesema hawawezi kususia ni mawazo yasiyofaa na hawawezi kufanya hivyo bila kujua ni jambo gani linaenda kuzungumzwa.
“Itika wito kwanza nenda kasikilize wanazungumza jambo gani, huwezi kutangaza unasusia bila kujua wanaenda kujadili nini hayo ni mawazo mfu,” amesema.