ACT waibua kilio mabomu Mbagala, Serikali yajibu

Muktasari:

  • Chama cha ACT Wazalendo kimehoji sababu za kutolipwa kwa fidia kwa baadhi ya waathirika wa mambomu ya Mbagala miaka 14 iliyopita kikiitaka Serikali iwajibike.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimehoji sababu za kutolipwa kwa fidia kwa zaidi ya wakazi 1,300 wa Mbagala jijini hapa walioathiriwa na mabomu miaka 14 iliyopita.

 Mabomu hayo yalilipuka mwaka 2009 katika kambi ya 671 JK ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo, majeruhi, kuharibiwa kwa makazi na mali za wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya alipoulizwa kwa simu, amesema tayari Serikali imeshashughulikia jambo hilo, bila kueleza kwa kina.

“Suala hilo limeshashughulikiwa na Serikali.”

Mbali na kiongozi huyo, Mwananchi imemtafuta Mkurugenzi wa Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu hiyo, Meja Jenerali Charles Mbuge, ambaye naye alitaka suala hilo aulizwe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene kuzungumzia hilo.

Simbachawene naye alipotafutwa, hakupokea simu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 1 jijini hapa, Waziri Mkuu kivuli wa chama hicho, Dorothy Semu amedai kuwepo kwa watu 1, 361 ambao hawajalipwa au kupunjwa fidia zao, miongoni mwa wakazi 12,000 walioathiriwa na mabomu hayo.

Amesema chama hicho kilifuatilia suala hilo kwa kuchambua taarifa mbalimbali (Orodha ya waathiriwa, malipo, risiti za malipo, kiasi cha bajeti kilichotumika na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na baadaye kutembelea baadhi ya waathirika.

“Tumeshangazwa sana kuona kwa zaidi ya miaka 14 tangu kutokea kwa mlipuko hiyo kuna waathirika wapatao 1,361 kutolipwa fidia yao,” amesema.

Ametaja malalamiko ya waathiriwa hao kuwa ni pamoja na kuwepo kwa malipo kidogo, utaratibu mbovu wa tathmini ya athari za mabomu, utaratibu wa malipo kutokueleweka na usiri wa malipo.