ACT-Wazalendo kuunguruma K’njaro, Mwigamba akumbushia mapito ya kukisajili

Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Shangwe Ayo.

Muktasari:

ACT-Wazalendo kujifungia kesho Jumamosi katika mkutano wa kidemokrasia kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kutahimini miaka 10 ya kuanzishwa kwake

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo, kesho Jumamosi Aprili 27, 2024 kitafanya mkutano wake wa kidemokrasia kujadili mwenendo wa demokrasia na uelekeo wa chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mita, vijiji na vitongoji.

Mkutano wa kidemokrasia ambao upo kikatiba katika chama hicho utakuwa wa sita tangu kuanzishwa kwa ACT-Wazalendo mwaka 2014. Kwa sasa ACT-Wazalendo imefikisha miaka 10 na mkutano huo utakuwa sehemu ya kusheherekea miaka hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 26, 2024, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Shangwe Ayo amesema maandalizi ya mkutano utakaofanyika mkoani Kilimanjaro yanakwenda vizuri.

Ayo amesema mkutano utakaokutanisha viongozi wakuu wastaafu, wa sasa na wanachama kutoka maeneo mbalimbali utajadili masuala mbalimbali yanayolenga kuhakikisha chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kinapiga hatua za maendeleo.

“Tutajadili historia ya chama, kilivyoanzishwa na kinavyoelekea, namna baadhi ya viongozi waliokuwa CUF (Chama cha Wananchi) walivyoahamia ACT-Wazalendo na kauli mbiu ya Shusha Tanga pandisha Tanga ilivyofanya kazi,” amesema Ayo.

Machi mwaka 2019, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) na viongozi waandamizi walikihama chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Hatua hiyo ilitokana na kuwepo kwa mgogoro wa uongozi ndani ya CUF uliokigawa chama hicho pande mbili za wanaomuunga mkono Maalim Seif na Profesa Ibrahim Lipumba (mwenyekiti) jambo ambalo lilifikishwa hadi mahakamani.

Chanzo cha mgogoro huo kilisababishwa na hatua ya Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wake Agosti 2015, kisha kuandika barua ya kutengua uamuzi wake siku chache kabla kufanyika mkutano mkuu wa chama hicho.

Mbali na hilo, Ayo amesema katika mkutano huo, kiongozi mstaafu wa chama (KC), Zitto Kabwe ataeleza namna alivyohama Chadema na kuanzisha ACT-Wazalendo.

Zitto aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema bara na aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo walivuliwa uongozi na kufukuzwa uanachama mwaka 2013 wakituhumiwa kukisaliti chama hicho.

Kwa mujibu wa Ayo, mkutano huo utatumika pia kutambulisha rasmi nembo mpya mwonekano wa bendera ya ACT-Wazalendo, kama kilivyoahidi katika mkutano mkuu uliofanyika Machi 5 na 6, mwaka huu.

“Tutakuwa na wageni mbalimbali wakiwAmo viongozi wa vyama vya upinzani na viongozi wa dini, pia wanachama wetu watashiriki na kuulizwa maswali kwa njia ya kidijitali,” amesema Ayo.

Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Biman amesema mkutano huo unaowakutanisha wanachama mbalimbali wa chama hicho una lengo pia la kujenga umoja wa WanaACT-Wazalendo.

Kwa upande wake, Wakili Peter Madeleka ambaye ni mmoja wadau walioichangia ACT- Wazalendo katika kufanikisha mkutano mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Machi 5 na 6 amesema:"ACT- Wazalendo kimeonyesha ukomavu ndani ya siasa za vyama vingi vya Tanzania licha ya kuanzisha miaka michache.”

"Kina mwenendo mzuri na kimeonyesha kuna kitu ndani ya demokrasia ya vyama vingi, ni chama kilichojidhatiti, kina falsafa nzuri kina kizingatia usawa wa kijinsia kuanzia uongozi wake wa juu, kikiendelea hivi kitakuwa tishio," amesema Madeleka.

Aliyekuwa mmoja wa waanzilishi wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba amekipongeza chama hicho kwa kufikisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake akisema haikuwa kazi rahisi kukisajili.

"Tulipata shida sana, tulizungushwa katika mchakato wa kukianzisha lakini tulivumilia hatimaye tukafanikiwa, nakumbuka mwaka 2014 tulishiriki uchaguzi wa kwanza wa serikali za mitaa vijiji na vitongoji ingawa hatukuwa na ruzuku lakini tulipata viongozi zaidi ya 300 katika maeneo mbalimbali.

"Mwaka 2015 tulishikiri uchaguzi mkuu na kufanikiwa kupata mbunge mmoja (Zitto) madiwani 32, meya na naibu meya wa manispaa ya Ujiji na tukapata ruzuku ya Sh 2.2 milioni, sasa hivi imepanda," amesema Mwigamba ambaye ameshakihama chama hicho.

Mwigamba aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho, ameipongeza kufikisha miaka hiyo huku akidokeza lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ilitokana na baadhi ya vyama vya upinzani kuonekana kama mali ya mtu binafsi.