Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UHURU NA URITHI WA KIKOLONI

Wakazi wa Manzese jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Oktoba mwaka 2015

Muktasari:

Miaka 50 baadaye, maadui hawa bado wanaonyesha makucha na wanatushambulia kutoka kila upande kwa kasi ya kutisha. Katika hali hii, kuna haja gani tena kuendelea kutembea kifua mbele tukitangaza uhuru wetu?

Tanzania ni nchi huru na tunajivuna kwa kutembea kifua mbele tukitangaza uhuru wetu. Baada ya kupata uhuru tulitangaza kupambana na adui wakuu watatu: Ujinga, maradhi na umaskini.

Miaka 50 baadaye, maadui hawa bado wanaonyesha makucha na wanatushambulia kutoka kila upande kwa kasi ya kutisha. Katika hali hii, kuna haja gani tena kuendelea kutembea kifua mbele tukitangaza uhuru wetu?

Ukweli usiopingika ni kwamba tumerithi mambo mengi ya kikoloni, hata na yale ambayo tuliyachukia wakati ukoloni, tumeyarithi na kuyakumbatia. Haya ni kama vile mfumo wa uongozi, muundo wa Bunge na mengine mengi kama vile sheria.

Tunasikia watu wakikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi, sheria hii ya uchochezi ni ile ya kikoloni, ni sheria ile ile iliyomkamata na kumshtaki Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere miaka hiyo, pia ni sheria hiyo hiyo iliyomkamata na kumfunga Marehemu Mzee Rashid Kawawa.

Ukiangalia mazingira ya mapambano haya ya wale wanaosema kuna uchochezi na wale wanaofikiri wanatetea haki zao, ni yale yale kama ya wakati wa kupigania uhuru, tofauti ni kwamba wakati ule ulikuwa ni ukoloni na leo ni uhuru wenye urithi wa kikoloni.

Kwa vile urithi huu una nguvu nyingi za kumpumbaza mtu, ndiyo maana hadi leo hii tumeshindwa kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini.

Siasa za wakoloni zilikuwa na mfumo wa ‘Wagawe uwatawale’, na si ‘Wagawe uwaongoze’. Ukweli ni kwamba ili mwanadamu aendelee vizuri anahitaji uongozi na wala si utawala.

Walitugawa kwenye makundi ya kikabila, kidini na kwenye makundi ya walionacho na wasionacho. Siasa zetu leo hii ni mfumo ule ule wa Kikoloni. Siasa zinatugawa.

Badala ya kufikiria umoja wetu na kuijenga Tanzania yetu, tunagawanyika katika makundi ya kisiasa. Tunajenga uhasama mkubwa na chuki kama za wakati ule wa kikoloni.

Kwa njia hiyo hawa wanasiasa wanapata mwanya mzuri wa kututawala. Ukabila unaanza kurudi kwa mwendo kasi, udini unanukia na vyama vya siasa vinajenga ukuta badala ya kujenga daraja!

Kuna mengi ya kujadili juu ya mada hii ya urithi wa kikoloni. Lakini kwa leo nijikite kwenye mitalaa. Katika elimu, tumerithi mitalaa ya kikoloni. Hadi leo hii tunaiendeleza na tunaendelea kutembea kifua mbele tukiisifia mitaala ya kikoloni inayoendelea kuleta giza badala ya mwanga! Mitalaa hii inayowatengeneza watawala badala ya viongozi!

Mfano nchi zote zilizoendelea zinatanguliza falsafa kama msingi wa elimu zote. Mtu, anaweza kuuliza, kama falsafa ni msingi wa elimu zote mbona mitalaa yetu hapa Tanzania haina somo la falsafa? Mbona falsafa haifundishwi sekondari?

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiyo kimeanza kuifundisha, lakini bado haijashika kasi inayotakiwa. Jambo la kushangaza, bado falsafa inabezwa sambamba na masomo yote yasiyokuwa ya uhandisi, kwa msemo wao pale mlimani, falsafa nayo ni “Nguin”. Jibu ni kwamba mitalaa yetu bado ni ya kikoloni.

Wakoloni hawakutaka tufikiri! Tungefikiri wasingeweza kututawala, ukoloni na ukoloni mamboleo vingeshindwa! Hivyo walitengeza mitalaa ya kuandaa “kasuku”. Waliandaa watu wa kuwafanyia kazi kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi zao.

Waliandaa watu wa kuutukuza uzungu na kuendeleza fikra za uzungu. Mitalaa yao, ambayo ndiyo tunatumia hadi leo ililenga kudumaza fikra. Mfumo wa ‘ukasuku’ uliwasidia kututawala na wanaendelea kututawala hadi leo!

‘Ukasuku’ unazaa uelewa finyu ama wa nidhamu husika ya kitaaluma au uelewa finyu wa misingi ya uamuzi yanayohusu maisha yetu. Huu ueleo finyu unatupelekea ama kwenye kurubuniwa kirahisi au kuelekeza nguvu zetu kwenye mambo ambayo yanaonekana katika nyuso zetu kama ndiyo mtatuzi wa matatizo yetu, lakini ukingalia katika vipimo vya mbali ni mambo ambayo ama yana utata ndani yake au yanatupeleka kwenye furaha ya muda mfupi na majonzi ya muda mrefu.

Mifano ni mingi, mfano ukoloni mambo leo, unaozaa utandawazi, soko huria, ubinafsishaji, uwekezaji na mambo mengine yanayokuja bila kuchujwa na fikira pevu!

Mitalaa ya kikoloni, ambayo tunatumia hadi sasa hivi imekumbatia dhana ya usomi na kazi. Kwamba mtu anasoma ili aje afanye kazi. Akute kazi inamsubiri. Kama anavyosema Dk Adolf Mihanjo katika kitabu chake cha: “Falsafa na Ufunuo wa Maarifa”:

“Miaka michache iliyopita dhana nzima ya usomi iliendana na kazi. Msomi baada ya kumaliza shahada yake tegemeo lake lilikuwa moja kwa moja ni kazi. Kazi ilikuwa kwake ni kitu ambacho kilikuwa kinamsubiri. Hali sasa hivi ni kinyume, msomi baada ya kumaliza shahada yake hana uhakika wa kupata kazi na hata kama akipata mara nyingi hupata kazi kinyume na ile ambayo ama aliitarajia au ameisomea” (Falsafa na Ufunuo wa Maarifa, Uk wa 15).

Kulingana na maoni ya Dk Mihanjo, ambayo kwa kiasi kikubwa ni ukweli mtupu ni kwamba ukosefu wa ajira na wa kazi ya kutabirika unawatupa wasomi wengi kwenye dimbwi la mahangaiko ya kutokuwa na uhakika wa soko la ajira. Changamoto hii kwa vyovyote vile lazima itupeleke kwenye msukumo wa mtazamo mpya wa utoaji wa elimu. Ni lazima kuangalia upya mitaala yetu.

Badala ya elimu ile inayolenga moja kwa moja soko la ajira, yahitajika kutolewa kwa elimu ambayo humuunda mtu ajiunde mwenyewe, yaani ile ambayo humsaidia mtu kupanua upeo wa mang’amuzi yake na uwezo wake wa kuutafakari ulimwengu.

Somo la falsafa ni silaha kali ya kupambana na maaduni wetu watatu, ujinga, maradhi na umaskini. Falsafa ni mwanga wa kufanya watu kuona ukweli. Mfano leo hii watu wanachubua ngozi zao na kufurahi kwamba wanafanana na wazungu, lakini majonzi ya kupata magonjwa ya ngozi ni kilio kisicho koma.

Tunafurahia kula vyakula vya kizungu na kufurahi kwamba tumeingia kwenye ustaarabu, lakini majonzi ya magonjwa ya moyo na kansa ambayo ni mageni kabisa katika jamii yetu ni kilio kisichokoma.

Tunafurahia kupokea risasi na silaha zote za moto kwamba ni bora kuliko mkuki, lakini majonzi yanayofuata ni vita, majanga ya wakimbizi na ujambazi. Uelewa finyu unatusukuma kwenye furaha za muda mfupi na furaha ambazo kiini chake si furaha.

Mwanga wa falsafa utawafanya Watanzania kutambua kwamba baada ya miaka 50 ya uhuru taifa letu limefanywa kuwa ni shimo la takataka.

Mali zote zinazochukuliwa na takataka zinaletwa na kutupwa nchini.

Watu wataona ukweli wa kuwatoa machinga katikati ya jiji na kuwatupa pembezoni kama lengo la kuandaa mwanya mzuri wa kuanzisha maduka makubwa kama lile la Mlimani City. Bila kuwasafisha wamachinga, nani atakwenda Mlimani City?

Kwa vile wakoloni walikuja kwa lengo la kutawala na kupanua makoloni yao ili kusaidia maendeleo ya uchumi wa nchi zao waliendeleza ile dhana ya enzi za kati (Medieval Period), katika kipindi hiki falsafa iliwekwa chini ya mateka ya Kanisa Katoliki ambapo ilitumiwa (hasa na Aristotle na Plato) kama chombo cha kujenga misingi ya kimetafizikia ya kulieleza neno la Mungu katika ufasaha ambao uliacha akili iking’aa na mwanga wa ukweli.

Hata hivyo, hali hiyo ilibadilika katika kipindi cha uvuvumko. Katika kipindi hiki falsafa iliachwa kama dhana huru na kazi yake kubwa ilikuwa ni kutoa taarifa ya uamuzi wa kisayansi, kijamii, kielimu, kidini na kisheria.

Wakoloni, walikwepa kutoa mwanga wa uvuvumko, maana watu wangehoji dini za kigeni na kutawaliwa.

Mwanga wa uvuvumko, ungewasaidia Waafrika(Watanzania) kukumbatia elimu ya kulinda na kuheshimu mila na desturi zao, elimu ya kulinda na kuheshimu historia, dini na utaalamu wa Kiafrika ambao kwa vile haukuandikwa umepotea, baada ya kulaaniwa kuwa ni ushenzi na Wazungu. Hivyo kwa kuogopa mwanga wa uvuvumko Wakoloni walitengeneza mitaala isiyokuwa na somo la falsafa.

Leo hii tunapolia na mbadiliko ni wakati mzuri wa kuzama katika tafakari na kujiuliza maswali mengi Je, tunaona kwamba mitaala yetu bado ni ya kikoloni? Mitaala hii imekuwa ikibadilishwa badilishwa bila majadiliano na kusikiliza hoja za wananchi.

Na kila ikibadilishwa inakuwa ya kikoloni zaidi! Kuna wakati waheshimiwa wabunge walipinga kwa nguvu zote matumizi ya Kiswahili. Mwaka 2004 mitaala ilibadilishwa na watu wakalalamika, Serikali ya Awamu ya Nne, imerudisha mitaala ya zamani, lakini bado mitaala hii kwa vile haina somo la falsafa, bado ina kasoro kubwa ya kuweza kuleta upevu wa fikra.

Kwenye uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano tufanye uamuzi juu ya mitaala yetu; falsafa ifundishwe kwa wanafunzi wote wa ngazi ya sekondari hadi chuo kikuu kwa Kiswahili. Mitaala ya elimu itengenezwe kwa kuzingatia umuhimu wa somo la falsafa.

Kwa njia hii itakuwa rahisi hata viongozi wa nchi kupenyeza falsafa zao na kuwanoa vijana, ambao wanalilia Tanzania mpya ya kuwa na fikra pevu. Bila kujenga taifa la watu wanaofikiri na kuzama katika fikra pevu ni vigumu kuleta maendeleo.

Kuna haja ya kuiangalia mitaala yetu na kuingiza somo la falsafa. Mitaala ya kikoloni na ukoloni mambo leo lazima kuizika. Hapa Kazi tu iwe ni kaulimbiu ya kutupilia mbali fikra za kikoloni na kujenga fikra pevu ya kujikomboa kutoka kwenye giza na kuingia kwenye mwanga, iwe ya kujithamini sisi kama Watanzania na kujivuna na Tanzania yetu.

Hapa Kazi tu iwe nia na aina ya nguvu mpya ya kulijenga Taifa linalojiamini na kujitawala kimawazo.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na simu namba +255 754 633122 au [email protected]