Uchumi wa Afrika wakua, lakini wengi wangali na njaa
Kijana akiwa amevalia raba zilizotoboka
Muktasari:
Ripoti hii huorodhesha mataifa kwa vigezo vya wastani wa miaka ambayo watu wa taifa husika huishi, viwango vya elimu, ubora wa maisha miongoni mwa masuala mengine.
Kila mwaka, Serikali, wanahabari, wataalamu wa maendeleo na wengineo husubiri kwa hamu kutolewa kwa Ripoti ya Ustawi wa Binadamu, inayotayarishwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP).
Ripoti hii huorodhesha mataifa kwa vigezo vya wastani wa miaka ambayo watu wa taifa husika huishi, viwango vya elimu, ubora wa maisha miongoni mwa masuala mengine.
Ripoti hii inapotolewa, Serikali na raia wa mataifa yaliyoorodheshwa kuwa bora hujivunia mafanikio yao. Lakini yale yanayoorodheshwa chini, kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo ilikuwa ya mwisho barani Afrika mnamo 2013, yanalaumiwa.
Wakati UNDP ilipotangaza mnamo 2012 kuwa ingezindua kwa mara ya kwanza Ripoti ya Ustawi wa Binadamu Afrika, wengi walitarajia ingeorodheshaa kila taifa.
Kuanzisha Mjadala
Mjadala huu ulianzishwa kwenye kurasa za ufunguzi wa ripoti hiyo na msimamizi wa UNDP, Helen Clark na Tefefnework Gettu, ambaye wakati huo alikuwa mkurugenzi wa tawi la Afrika la UNDP. Clark aliandika: “Ni matumaini yangu kuwa Ripoti ya Ustawi wa Binadamu Afrika, ambayo ni ya kwanza, itaupa nguvu mjadala kuhusu jinsi ya kuimarisha uwezo wa kujitosheleza kwa chakula na kuleta hatua mahsusi zaidi.”
Utangulizi wa Gettu nao ni mwito kwa viongozi wa Afrika: “Lazima Afrika ikome kuombaomba chakula, iwapo viongozi wa Afrika katika muda wa miaka 30 iliyopita wangetimiza matarajio ya watu wao, ripoti hii haingetayarishwa.
Robo moja ya watu katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hawangekuwa na utapiamlo, na theluthi moja ya watoto wa Afrika hawangekuwa na matatizo ya ukuaji bora.”
Aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo anakariri maoni ya Gettu akisema uongozi wa Afrika unafaa kulaumiwa kuhusiana na masuala ya uzalishaji wa chakula.
Katika mageuzi ya kuhakikisha yanajitosheleza kwa chakula, mataifa ya Asia yalitumia hadi asilimia 20 ya bajeti zao katika kilimo, ikilinganishwa na kati ya asilimia 5 na 10 katika mataifa ya Afrika.
Hii ni licha ya maazimio ya viongozi wa Afrika mnamo 2003 ya kutengea sekta ya kilimo asilimia 10 na zaidi ya bajeti zao za kitaifa. Kwa sasa Afrika inatumia fedha nyingi katika jeshi kuliko kilimo.
Njaa kwa wananchi
Afrika ni bara lililo na ardhi kubwa yenye rutuba, lakini imeshindwa kuwalisha raia wake.
“Njaa na utapia mlo ni tatuzo kubwa Afrika licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kilimo,” aeleza Gettu. Afrika ina ujuzi, teknolojia, na mbinu za kumaliza njaa na uhaba wa chakula”.
Kulingana na UNDP, eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndilo lenye uhaba mkubwa zaidi wa chakula duniani, huku viwango vya umaskini vikiwa ni vya kutisha.
Asilimia 25 ya watu milioni 856 milioni wanaoishi eneo hilo wana utapiamlo, huku watu 15 milioni wakiwa kwenye hatari zaidi katika ukanda wa Sahel, na idadi nyingine sawa na hiyo katika Pembe ya Afrika.
Kuendelea kuwepo kwa uhaba wa chakula katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kunadidimiza matumaini ambayo yamekuwa yakiangaziwa kwenye ripoti zinazoonyesha kuwa uchumi Afrika unakua kwa haraka.
Kulingana na ripoti hizo, uchumi wa Afrika umekuwa ukikua kati ya asilimia tano na sita katika muongo mmoja uliopita. Licha ya ukuaji huo, anasema Clark, “ukuaji huu wa kiuchumi haujasaidia kumaliza njaa na utapia mlo barani Afrika.”
Inaonekana kuwa viongozi wengi wa Afrika wanakubaliana kuhusu hatua hizi. Kwa mfano, rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa barani Afrika, Ellen Johnson-Sirleaf wa Liberia, anachukulia wanawake kuwa na mchango “mkubwa na muhimu” katika kuhakikisha kuna chakula cha kutosha.
Kulingana na Rais Johnson-Sirleaf, elimu bora pamoja na uwezo wa kupata rasilimali za kuzalisha chakula kama vile ardhi, fedha na wafanyakazi kunaweza kuongeza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 20.
Msimamo wake unaafikiana na ule wa ripoti ya UNDP, ambayo inahimiza mataifa ya Afrika “kukomesha hali ya miongo mingi ya kutenga wanawake wanaoshiriki kilimo,” kwa sababu elimu kwa wanawake inaweza kusaidia kupunguza utapiamlo miongoni mwa watoto, zaidi kuliko mapato ya familia yanapoongezeka.
Ikilinganishwa na maeneo mengine duniani, wanawake barani Afrika ndio wanaonyimwa zaidi haki ya kupata na kutumia ardhi.
Wakati fulani, aliyekuwa rais wa Kenya, Mwai Kibaki alihusisha lishe bora na afya ya kiakili na kimwili, na kuongeza kuwa, “pia inawezesha watu kutekeleza uhuru wao na uwezo katika nyanja tofauti.” Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyoorodheshwa kuwa katika hatari kubwa ya uhaba wa chakula.
Wakati wa utawala wake, Rais Kibaki alisema kiangazi kilichodumu miaka mitano kilikuwa na madhara kwa kilimo. Lakini sekta ya kilimo nchini Kenya imefufuliwa kutokana na kufifia kulikofika asilimia 2.3 mnamo 2009, hadi ukuaji wa asilimia 6.3.
Wachanganuzi wanaamini kuwa kilimo ndicho nguzo ya uchumi wa Kenya, ambao Shirika la Fedha Duniani (IMF) linakisia utakua kwa asilimia 6.2 mwaka huu.
Anders Ostman, ambaye alikuwa mkuu wa kanda ya Afrika ya Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden, alishauri Kenya na mataifa mengine ya Afrika kukipa kilimo umuhimu zaidi.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema mwaka jana kuwa Serikali yake itawasaidia wakulima kutumia mbinu za kisasa za teknolojia ya kilimo kwa lengo la kuleta “mageuzi” katika sekta hiyo.
Hata hivyo, Afrika inakumbwa na changamoto nyingi katika ukuaji wa kilimo. Wengi wanakubaliana kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yatakuwa na madhara kwa kilimo.
Madhara ya kiangazi na njaa ndiyo masuala yanayoangaziwa zaidi, ingawa kushindwa kupata chakula kutokana na umaskini pia ni tatizo kubwa.
“Matatizo ya utapia mlo na njaa za misimu haziangaziwi sana,” inasema ripoti ya UNDP. Uzalishaji zaidi wa chakula sio hakikisho la kuwepo kwa chakula cha kutosha iwapo hakutakuwa na ustawi katika huduma za afya, barabara bora, nafasi zaidi za ajira na kuimarisha uwezo wa wanawake.
Licha ya uhaba mkubwa wa chakula katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuna maeneo yenye matumaini. Nchini Nigeria, Ajenda ya Mageuzi katika Kilimo inatarajiwa kuhakikisha chakula cha kutosha na kubuni nafasi 3.5 za kazi kufikia 2015.
Kwa upande wake, Ghana imepunguza kwa nusu viwango vya umaskini kwa kuwasaidia wakulima wa cocoa, na hivyo kuwa taifa la kwanza Afrika kuafikia lengo la Kwanza la Milenia, ambalo ni kupunguza kwa nusu viwango vya umaskini kufikia 2015.
Malawi ilianzisha mpango mkubwa wa kuwasaidia wakulima kwa mbegu na mbolea ya bei nafuu, hali iliyosaidia kumaliza uhaba wa chakula wa tani 1.3 milioni katika muda wa miaka miwili.
Nchini Senegal, utapia mlo miongoni mwa watoto ulipungua kutoka asilimia 34 hadi 20 kati ya 1990 na 2005 kutokana na kuongezwa kwa fedha zilizotengewa kilimo kwenye bajeti.
Ilipoongeza mgawo wake wa bajeti kwa kilimo kutoka asilimia 1.6 hadi 7.7 mnamo 2009, Sierra Leone ilikuza tani 784,000 cha mchele, ambacho ni kiasi zaidi ya mahitaji ya nchi hiyo ambayo ni tani 550,000.
Kadri bara la Afrika linavyoimarika kiuchumi, linafaa kuchukua hatua za haraka kuwapa raia wake chakula cha kutosha na chenye lishe. Macho yanawatazama viongozi wa sasa wa Afrika kuona kama watatimiza lengo hili.
Hali ya Tanzania
Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, hata hivyo kwa namna inavyoonekana ni kwamba hakuna jitihada za dhati za kuwasaidia wananchi hao wawe na maendeleo makubwa.
Ahadi nyingi zimekuwa zikitolewa, bila kuwa na mafanikio yanayotazamiwa. Msingi wa kutokuwa na mafanikio mazuri katika sekta ya kilimo ni mipango duni ya Serikali.
Sera zinazohusiana na kilimo siyo tu kwamba nyingi hazifahamiki kwa wakulima, hata wataalamu wa kilimo wamekuwa wakilalamikiwa kutofanya kazi zao vizuri;
kwamba wengi wao wanakaa zaidi ofisini badala ya kwenda shambani kushirikiana na wakulima kama inavyotakiwa ili kuyaondoa matatizo yao.