Tanzania yaanza safari ya uchumi wa dola trilioni 1 za Marekani ifikapo 2050
Muktasari:
- Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo (FYDP IV) kama hatua ya kwanza ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani moja ndani ya miaka 24.
New York, Marekani. Serikali ya Tanzania imeanza rasmi utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa 2026/27–2030/31, ukiwa hatua ya kwanza ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani ifikapo mwaka 2050.
Hatua hiyo imeelezwa katika Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa (HLPF 2026) linaloendelea New York, Marekani.
Akizungumza katika mkutano wa pembeni wa jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais–Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Tausi Mbaga Kida amesema mpango huo unalenga kubadili mafanikio ya ukuaji wa uchumi kuwa ongezeko la uzalishaji, ajira zenye tija, mauzo ya nje, uongezaji thamani wa bidhaa na ustawi wa wananchi.
Amesema uchumi wa Tanzania kwa sasa unakua kwa asilimia 5.9 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 ifikapo mwisho wa mwaka huu, lakini msisitizo wa Serikali ni kuhakikisha ukuaji huo unawanufaisha wananchi kupitia ajira, ongezeko la kipato na kupunguza umaskini.
Dk Kida amesema sekta za kilimo, misitu na uvuvi zinaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania, zikichangia asilimia 24.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025, huku mchango wa sekta ya uvuvi ukiongezeka kutoka asilimia 1.9 mwaka 2020 hadi asilimia 2.2 mwaka 2025. Amesema Serikali inalenga kuhamisha uchumi kutoka utegemezi wa kuuza malighafi kwenda kwenye uchumi unaosindika mazao, kuongeza thamani ya bidhaa, kutumia teknolojia na kuwaunganisha wazalishaji wa ndani na masoko ya kikanda na kimataifa.
Pia, ametangaza kuwa Tanzania itawasilisha Mapitio ya Tatu ya Hiari ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) Julai 14, 2026.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Togolani Mavura, amesema mageuzi ya viwanda Afrika yanapaswa kuwa jumuishi kwa kuwashirikisha wakulima wadogo, wanawake, vijana, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara wadogo.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Karen Vardanyan, amesema Tanzania imeonesha mfano wa matumizi ya fedha bunifu katika maendeleo, akitaja ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, pamoja na mafanikio ya hatifungani ya kijani ya Tanga Uwasa iliyokusanya Dola 20.8 milioni za Mwarekani kwa miradi ya maji inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Washiriki wa mkutano huo wamesisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na FYDP IV utategemea ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, Umoja wa Mataifa na washirika wa maendeleo.
Kupitia dira hiyo, Tanzania inalenga kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani, kuongeza pato la wastani kwa mtu hadi zaidi ya Dola 7,000 kwa mwaka na kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini ifikapo mwaka 2050.