Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna nafuu kubwa kutumia magari yanayotumia gesi asilia

Muktasari:

Mhandisi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),  Modestus Lumato anasema licha ya jiji la Dar es salaam kuwa na idadi kubwa ya magari, hadi sasa ni magari 70 tu yaliyowekewa mfumo wa gesi  asilia na kwamba ya sababu ya kuwa na idadi ndogo ya magari yanayotumia gesi asilia ni kuwepo kwa kituo kimoja tu cha kujazia gesi kilichopo Ubungo.

Gesi asilia ikitumika kwenye magari inaweza kupunguza zaidi ya nusu ya gharama mafuta na kuleta unafuu katika sekta ya usafirishaji nchini.

Huu ni kwa mujibu wa uchunguzi  uliofanywa jijini Dar es salaam hivi karibuni na kubaini kuwa lita moja ya mafuta ya petroli ambayo bei yake ni wastani wa Sh2,000, inaweza kutembea kilomita tisa mpaka 12 wakati nusu lita ya ujazo wa gesi ya asili ambayo inauzwa kwa bei ya Sh880 inaweza kutumika kusafiri kilometa 12.

Mhandisi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),  Modestus Lumato anasema licha ya jiji la Dar es salaam kuwa na idadi kubwa ya magari, hadi sasa ni magari 70 tu yaliyowekewa mfumo wa gesi  asilia na kwamba ya sababu ya kuwa na idadi ndogo ya magari yanayotumia gesi asilia ni kuwepo kwa kituo kimoja tu cha kujazia gesi kilichopo Ubungo.

Kituo cha kujaza gesi asilia  Ubungo, kina uwezo wa kujaza magari 200 kwa siku hata hivyo wafanyakazi wa kituo hicho wanasema kwa siku wanapokea kati ya magari matano hadi saba.

Anasema TPDC hivi sasa ina kituo kimoja tu katika nchi nzima cha kujazia gesi asilia kwenye magari yaliowekewa mfumo wa gesi asilia.

Uchunguzi uliofanywa katika kituo cha kujazia gesi kwenye magari cha Ubungo umebaini kuwa iwapo basi linajaza mafuta ya petroli kwa Sh 300,000, basi hilo likifungwa mfumo wa kutumia gesi asilia litajaza gesi asilia ya Sh150,000.

Kwa mujibu wa Lumato magari ambayo yanaweza kufungiwa mfumo wa gesi asilia ni yale ambayo yanatumia mafuta ya petroli na sio dizeli.

Anasema kabla mteja hajawekewa mfumo wa gesi asilia, usalama wa mitungi, sheria za udhibiti wa magari na elimu ya usalama ni mambo ambayo yanafanyika na kwamba  gari ambalo linatumia gesi linakuwa na mtungi ambao umejazwa na kushindiliwa kiwango kikubwa na mgandamizo wake.

Kupunguza gharama

Matumizi wa gesi asilia katika magari hapa nchini yatafanikiwa kama Serikali itachukua hatua madhubuti  ya kuondoa ushuru wa forodha unaotozwa katika vifaa vinavyotumia gesi kutoka nchi za nje. Anasema mwandishi Beatrice Philemon katika uchunguzi wake.

Kwa mujibu wa uchunguzi wake, anasema matumizi ya nishati hiyo kuendeshea magari ni nafuu zaidi kutokana na muundo wa teknolojia inayotumika.

Hata hivyo, Philemon anaeleza kuwa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje kwa ajili ya kuwekwa katika magari yanayotumia gesi, vinatozwa  ushuru mkubwa.

Meneja Mradi kutoka kampuni ya Triangle Tanzania Limited, Bernard Sepetu anasema mfumo wa ubadilishaji  magari  ili yaweze kutumia nishati ya gesi asilia badala wa petroli  ulianzishwa   mwaka 2008 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC)  pamoja na  Pan African Energy Tanzania Ltd.

“Vifaa vyote inabidi tuviagize kutoka nje ya nchi, vinapofika hutozwa ushuru wa forodha wa asilimia 25 ambao ni mkubwa ukilinganisha na gharama ya gesi. Pia vinatozwa kodi ya ongezeko la thamani  yaani (VAT) ambayo ni asilimia 18,”anasema.

 Sepetu anaishauri serikali kuondoa ushuru unaotozwa katika vifaa hivyo kwa sababu  wananchi wengi wametambua umuhimu wa gesi asilia ambayo ni nafuu kutumika katika uendeshaji wa magari yao badala ya mafuta.

Hata hivyo anasema wateja wa mikoani wenye nia ya magari yao kufungiwa mfumo wa gesi asilia  wamekuwa wakijitokeza kuhitaji kuwekewa mfumo huo hivyo  anaiomba serikali kuharakisha utaratibu wa kufikisha gesi mikoani ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo.

Gesi na sheria

Mwanasheria na Mkurugenzi  Mtendaji wa Lawyers Environmetal Action Team (LEAT) Dk.Nshala Rugemeleza anasema   kutokamilika kwa sheria ya gesi, ndiyo sababu zinazochangia gesi asilia kutotumika na wengi, licha ya kupunguza gharama za matumizi majumbani na hata kuendeshea magari.

Anaeleza kuwa laiti sheria ya gesi ingekuwa imekamilika, ingeweza kupitisha sheria ya magari kufungwa mfumo wa gesi asilia tofauti na hali ilivyo hivi sasa.

“Gari zinazowekewa betri za kuchaji zinasafiri bila kelele kilometa 200 ndipo chaji inakwisha na unachaji tena kwa muda mfupi tu unaendelea na safari kwa kilometa nyingine 200. Sisi Tanzania bado tunasuasua kwenye matumizi ya gesi asilia, nadhani sekta ya madini ni lazima iwe na viongozi wenye utashi na wafanyakazi wawe na ujuzi na uzalendo katika nchi yao’’,anasisitiza DkNshala.

Gesi asilia inakoa fedha za kigeni

Baadhi ya nchi zinazotumia teknolojia ya gesi asilia kwenye magari ni Afrika Kusini, Misri na Msumbiji.

Utafiti umebaini kuwa
matumizi ya mfumo huo yatachangia kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza nishati ya mafuta kutoka nje ya nchi pamoja na  kuokoa uharibifu wa mazingira, kwa sababu gesi haizalishi hewa ukaa ambayo ni hatari katika mazingira.

 Baadhi ya nchi zilizoendelea ulimwenguni ikiwemo Norway zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea magari. Takwimu zinaonyesha kuwa magari  yapatayo milioni 11 duniani yanatumia gesi asilia na nchi inayoongoza ni Pakistan yenye  magari milioni 2.1, ikifuatiwa na Argentina yenye  magari 1.8 na  Brazil yenye magari 1.7.

Utafiti uliofanywa na TPDC umebaini kuwa gesi asilia ikitumiwa wakati wote, injini ya gari itadumu zaidi kwa sababu haizalishi uchafu  ikilinganishwa na  petroli na kwamba kama mwenye gari alikuwa anabadili mafuta ya injini  kila baada ya kilomita 3,000,  mfumo wa kutumia gesi asilia utamwezesha kubadilisha  baada ya  kilomita 6,000.

 Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Nishati na Madini Dk Ben Moshi anakiri kwamba ujio wa matumizi ya gesi asilia katika huduma mbalimbali nchini, unaweza kuathiri kampuni nyingi za mafuta zinazofanya biashara nchini.

Dk. Moshi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi katika kampuni ya mafuta ya PUMA Energy, anasema kampuni za mafuta nchini hazina budi kukubaliana na mabadiliko yanayokuja kupitia mapinduzi ya nishati ya gesi ili yasipoteze soko la mafuta.

 

Naye Mhandisi   Lumato anasisitiza kuwa gesi asilia ndiyo inayoweza kuinua uchumi kwa haraka, kwa kuwa tayari faida kubwa imepatikana tangu kupatikana kwa gesi ya Songosongo.

Anasema tayari Taifa limepata dola za Marekani milioni 117.5 kuanzia mwaka 2004 hadi 2012, na uchumi umeokoa dola bilioni 4.4 kati ya mwaka 2004/2012 .

“Nchi inapoteza sh.trilioni 1.6 kwa mwaka kwa kutumia mafuta kuzalisha umeme kisha kununua umeme kulingana na mikataba mibovu ambayo inalitafuna Taifa, gesi asilia inayotumika ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyogundulika  kwa hiyo unaweza kuona faida ya gesi asilia’’,anasema.