Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Athari za urani; nani mkweli?

Kutokana na athari kubwa za urani ni kawaida kuona wafanyakazi wake wakiwa wamejifunika hivi, je Tanzania imejiandaa kupambana na athari zake? Picha ya Maktaba.     

Muktasari:

Kwa mujibu wa makisio yake, MTRL inatarajia kuchimba takribani tani 4.5 milioni za madini hayo kwa mwaka baada ya kufanya utafiti wa kina tangu mwaka 2005 ilipopewa leseni ya kuchunguza uwepo wa madini hayo hapa nchini.

Wakati kampuni ya Mantra Resources Tanzania Limited (MTRL) ikiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa uchimbaji wa urani katika mradi wake wa Mkuju huko wilayani Namtumbo wadau wa madini na mazingira wameiasa serikali kutoruhusu uchimbaji mpaka pale itakapotoa elimu ya kutosha kwa wananchi dhidi ya madhara ya uchimbaji huo.

Kwa mujibu wa makisio yake, MTRL inatarajia kuchimba takribani tani 4.5 milioni za madini hayo kwa mwaka baada ya kufanya utafiti wa kina tangu mwaka 2005 ilipopewa leseni ya kuchunguza uwepo wa madini hayo hapa nchini.

Tanzania imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya madini ya aina tofauti ambayo baadhi yameanza kuchimbwa katika sehemu mbalimbali huku wachimbaji wadogo au wawekezaji wakihusika.

Urani ni miongoni mwa madini ambayo yamegundulika kuwepo katika baadhi ya maeneo hasa kwenye bonde la ufa. Serikali imethibitisha uwepo wa madini haya katika mbuga ya Selous game reserve ambayo yanasemekana kuwa na yenye kiwango cha juu kimataifa. Maeneo mengine ni pamoja na wilaya za Bahi na Manyoni mkoani Dodoma na, mkoa wa Singida.

Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Rosa Luxemburg Stiftung (RLS) la Ujerumani mwishoni mwa Mei walizindua taarifa kuhusu madhara kwa afya na mazingira ya uchimbaji wa madini ya urani kwa kutumia uzoefu kutoka nchi ambazo zimeshaanza uchimbaji wa madini haya kama Mali na Niger.

“Watanzania wengi hawana utaalamu na ujuzi wa kutosha kuchimba madini haya,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Mhfoudha Hamid, aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa taarifa hiyo.

 

 

Hamid aliasa kuwa ni vyema wananchi wakashirikishwa, hasa kwa kupewa elimu kuhusu madhara ya uchimbaji wa madini haya, ili wawezekukabiliana ipasavyo na viashiria vya madhara pindi vitakapojitokeza.

Katika uzinduzi huo mambo kadhaa yalipendekezwa yafanywe kabla Serikali haijaruhusu uchimbaji rasmi. Yaliyopendekezwa ni pamoja na tathimini ya matumizi ya maji, matumizi ya ardhi, udhibiti wa mionzi na usafirishaji wa madini hayo kutoka migodini mpaka bandarini.

Inaelezwa kuwa madini haya hayana madhara yakiwa ardhini lakini yakichimbwa, madhara mengi hujitokeza dhidi ya wachimbaji na wote walio karibu na maeneo ya machimbo huku uchafuzi wa maji ukiwa ndiyo unaochangia kuenea kwa magonjwa mengi kama saratani ya damu, figo, ubongo, ini na magonjwa ya moyo, upungufu wa kinga za mwili, watoto kufia tumboni pamoja na vifo vya watoto wachanga, au kuzaliwa na ulemavu wa ubongo.

“Urani ni kifo. Ni bora kuwa maskini lakini mwenye afya njema kuliko kuwa tajiri usiye na afya ya uhakika, hii itakunyima furaha ya fedha ulizonazo. Ni vyema Serikali ikaangalia vyanzo mbadala vya mapato visivyo na madhara makubwa kwa wananchi,” anasema Dk Mtonga, Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa linalozuia matumizi ya silaha za urani (IPPNW), aliyekuwepo katika uzinduzi huo.

Anaeleza kuwa madhara ya urani hayalingani na faida zake na kuwa mapato yatakayopatikana kamwe hayataweza kugharimia matibabu ya maradhi yatakayokuwapo baadaye.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Madini (TMAA), Injinia Dominic Rwekaza anaeleza kuwa uchimbaji wa urani una madhara lakini inategemea na hatua iliyofikiwa.

“Uchimbaji wa urani ni majanga. Ukifika Mkuju urani ipo juu juu, lakini madhara yake ni baada ya kuanza kuchimbwa. Tume ya Nguvu za Atomiki wanajipanga kuelimisha umma juu ya madhara yake,” anasema Rwekaza.

Inaelezwa kuwa kinu kimoja cha kuzalisha urani, kutoka kwenye mwamba na kabla haijarutubishwa, huhitaji kiasi cha lita milioni 40 za maji kwa siku. Ripoti inataka ufafanuzi wa Serikali juu ya upatikanaji na umwagaji wa maji haya baada ya matumizi.

Mshauri wa masuala ya kiufundi wa taasisi ya kimataifa isiyo ya kiserikali ya WaterAid, Herbert Kashililah anasema kiasi hicho cha maji ni kikubwa kwa matumizi ya siku moja kwa kampuni moja na kwamba yanaweza yakaathiri watumiaji wengine.

“Kwa matumizi haya ni lazima mabwawa mengi yajengwe ili kuepusha athari kwa mazingira na binadamu. Sera ya maji ya Taifa imeainisha kuwa kipaumbele cha kwanza ni binadamu, ikifuatiwa na viumbe wengine na yanayosalia ndiyo kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi kama umwagiliaji, viwanda na madini,” anasema Kashililah.

Mwaka 1983, Wakala wa Mazingira nchini Marekani (EPA) aligundua kuwa nyumba zilizo ndani ya maili moja kutoka machimbo ya urani, zilikuwa katika hatari kubwa ya kupata saratani.

Wakala huyo alieleza kuwa wakati wa uchimbaji maji mengi yanayotumika huchangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa maji yatumiwayo na viumbe hai.

Maji haya machafu, ambayo hutunzwa katika mabwawa ili kupunguza nguvu za mionzi, huingia katika mkondo wa maji na kusambaza mionzi hiyo ambayo ni hatari kwa afya na mazingira vile vile.

Madhara mengine yaliyobainishwa ni udhibiti wa mionzi. Urani inazalisha mionzi ya aina tatu ambayo ni alfa, beta na gama. Wakati wa uchimbaji, asilimia 85 ya mionzi hii hubaki katika mashimo au vifusi vilivyochimbwa.

Mionzi hii huweza kusambaa kwa mmomonyoko wa udongo, mapitio ya wanyama, mafuriko, vumbi, mimea na hata makosa ya kiufundi.

Kuvurugwa kwa uzazi na watoto kuzaliwa na ulemavu wa ubongo na viungo. Madhara haya yameonekana katika nchi zenye uzoefu wa uchimbaji wa urani kama Niger, Namibia, Malawi, DRC, Australia, Ujerumani, Ufaransa na Japan.

Matumizi makubwa ya ardhi ambayo itachimbwa, kuwekwa kifusi na hata ujenzi wa mabwawa kwa ajili maji taka yatakayozalishwa baada ya kusafishwa kwa madini.

Ikumbukwe kuwa mionzi hubaki katika kifusi na hata maji taka haya kwa hiyo tahadhari ni lazima ichukuliwe. Kwa maeneo kama Mkuju ambako kuna hifadhi ya wanyama, hatari ni kubwa zaidi endapo kosa lolote litafanywa.

LHRC wanasisitiza kuwa wachimbaji wa urani wana kubwa ya kuugua kifua kikuu huku kukiwa na uwezekano wa kuathiri figo kutokana na madini hayo kuingia mwilini kupitia maji ya kunywa au chakula.

Taarifa inaonyesha kuwa urani ina matumizi mawili pekee; kufua umeme au kuzalisha silaha za nyuklia. Tanzania haina lengo lolote la kutumia madini haya kuzalisha chochote kati ya hivyo viwili.

Mkurugenzi wa RLS hapa nchini, Siegfried Schroeder, anatahadharisha kuwa uchimbaji wa madini una hatari kubwa.

“Madhara na hatari ya urani ni lazima yawekwe bayana kwa wadau wote. Kuna taarifa za kansa kwa wafanyakazi wa migodi ya urani nchini Namibia. Ujerumani ina kinu cha nyuklia lakini imeamua kukifunga…pamoja na hayo bado inaendelea kugharamia madhara yake,” alisema Schroeder.

Schroeder aliongeza kuwa Tanzania haina cha kufanya na urani zaidi ya kuzalisha umeme ambao una mbadala kutokana na kuwepo kwa vyanzo vingi visivyo au vyenye madhara madogo zaidi.

Kwa kutambua hatari ya uchimbaji wa urani, LHRC inaiasa serikali kutoharakisha uidhinishaji wa uchimbaji wa madini hayo katika baadhi ya miradi kama Mkuju ulio chini ya Kampuni ya Mantra Tanzania, kwa vile suala hilo linagusa haki za msingi ikiwamo ya kuishi, maji safi na salama na mazingira salama pia.

“Kwa kuwa urani ni hatari kuliko madini mengine, tunahitaji kujipanga ili kuhakikisha haturudii makosa ya nyuma,” anasema Hamid.

Wizara ya Nishati na Madini imewahi kukanusha kuwapo kwa madhara yatokanayo na uchimbaji wa urani kauli inayokinzana na ile ya Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc).

Wizara hiyo ilishutumu taarifa zilizotolewa na wanaharakati walioasa juu ya athari za kiafya na mazingira ikisema kuwa madai hayo si ya kweli kwa vile hatua inayofikiwa katika uzalishaji hapa nchini haina uwezo wa kuacha athari zinazosemwa.

“Tanzania haitarutubisha urani. Hatua za urutubishaji na matumizi yake katika kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za afya, kilimo, ujenzi na mifugo zitafanyika katika nchi zilizoendelea kama Japan, Ufaransa na Urusi. Katika hatua hizo ndipo huweza kusababisha madhara yanayoongelewa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya wizara.

Faida zilizobainishwa baada ya kuanza kwa Mradi wa Mkuju, utakaodumu kwa miaka 12, ni pamoja na mrabaha wa Dola za Marekani 190 milioni (zaidi ya Sh304 bilioni), kodi kiasi cha dola 363 (zaidi ya Sh581 bilioni) na kodi ya kipato cha mtumishi (PAYE, zaidi ya Sh80 bilioni) huku zaidi ya ajira 690 zikitolewa kwa Watanzania.

Je nani mkweli kuhusu athari za urani; Wataalamu au wanasiasa?