UCHAMBUZI: Hatutarajii haya kwa wasanii Tamasha la Ziff

Muktasari:
Hii ni fursa ya kipekee kwa wasanii kuhudhuria tamasha hili ili kujifunza na kukutana na waigizaji nguli kutoka nchi za nje.
Ifikapo Julai 9, tamasha linalokusanya idadi kubwa ya waigizaji na waandaaji wa filamu duniani kote, Zanzibar International Film Festival (ZIFF), litaanza rasmi katika Viwanja vya Ngome Kongwe vilivyopo Unguja.
Hii ni fursa ya kipekee kwa wasanii kuhudhuria tamasha hili ili kujifunza na kukutana na waigizaji nguli kutoka nchi za nje.
Pia, tamasha hili linawapa fursa nzuri kwao kujitanua kimataifa kwani wataweza kupata nafasi ya kujuana na waandaaji wa kimataifa, hii inaweza pia kuwa uchochoro wa kuwawezesha kufanya kazi nje ya nchi baada ya kubadilishana mawasiliano yao.
Kwa miaka mitatu mfululizo nimeshuhudia wasanii wakishindwa kuhudhuria siku za mwanzo za tamasha kwa kisingizio cha kukosa fedha kwa ajili ya gharama ya malazi na chakula. Miaka yote wamekuwa wakisubiri tamasha lilikaribia ukingoni hufika tena baada ya kulipiwa gharama zote na waandaaji.
Wakati tamasha hili likifanyika kwa mara ya 19 sasa, sidhani kama yupo msanii ambaye amenufaika kama wafanyavyo wasanii wengine wa nje.
Watengeneza filamu duniani wamekuwa wakichuana kuwania nafasi chache ambazo hutolewa ili wapate nafasi ya kushiriki.
Uongozi wa Ziff kila mwaka hupokea maelfu ya maombi ya wadau wa filamu kutoka kila kona ya dunia, wakitaka kupata nafasi ya kuhudhuria kwa kuwa wanajua manufaa yake.
Watu hawa hulipia vibali kwa pesa nyingi, viza, nauli, kugharamia malazi na kila kinachohitajika ili mradi tu waipate nafasi hiyo adimu.
Kwa wasanii wetu hali ni tofauti, kwa uwazi kabisa wanakiri kuwa huwa hawaendi mpaka uongozi wa tamasha hilo uwalipie gharama zote.
Waswahili husema kwenye miti hakuna wajenzi, lakini umefika wakati wasanii waamke ili waiokoe tasnia ya filamu na maigizo nchini inayosuasua.
Waone umuhimu wa kulitumia tamasha hili kama nyenzo ya kuiamsha tasnia ya filamu nchini kwa kujichanganya na kuchota ujuzi kutoka kwa wazoefu wanaohudhuria.
Ikumbukwe kwamba marehemu Steven Kanumba alilitumia vizuri Tamasha la Ziff na kumsaidia kukutana na wasanii wakubwa na kufanya kazi nyingi za kimataifa. Alitambua fursa iliyopo katika tamasha hili, hakuzilazia damu na alifanikiwa kuingia katika ushindani wa kimataifa.
Itakumbukwa Prince Richard ambaye alikuja kuwa meneja wa kimataifa wa mwigizaji huyo, alikiri kwamba lazima atafanya kazi na Kanumba baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza kwenye Tamasha la Ziff.
Kanumba alilitumia tamasha hilo kuhakikisha anafanikisha malengo yake lakini viatu vyake vinaonekana kuwa vikubwa kwa wasanii wenzake waliobaki.
Nilisikitishwa na kile alichokizungumza mwigizaji wa kike kutoka Guinea Bissau, Ady De Batista katika siku ya nne ya tamasha la 17 kuwa anamkumbuka marehemu Kanumba huku akisisitiza kuwa alitamani kukutana na mwigizaji yeyote mkubwa kutoka Tanzania.
“Ninasikitika nimeshindwa kukutana na mwigizaji yeyote kuzungumzia changamoto zinazohusu sanaa ya filamu Tanzania, lakini pia kubadilishana uzoefu. Nakumbuka kuhusu Kanumba lakini hatutamuona tena, Mungu amlaze pema,” mwigizaji huyo anatamba na filamu ya “The Thorn of the Rose”.
Kuna kitu kimoja kinanishangaza, hivi inawezekana vipi kukawa na ujio wa wageni ambao wenyeji wanajifungia ndani?
Wasanii mjitambue na kulitumia tamasha la Ziff liwanufaishe na mlete mabadiliko katika tasnia ya filamu nchini.