TUONGEE KIUME: Tunatamani kuwapenda wake zetu lakini tatizo lipo hapa

Ukweli ni kwamba Watanzania bado tunaamini kazi za nyumbani ni za wanawake.

Kufua, kuosha vyombo, kupika, kusafisha nyumba, kunyoosha nguo hizo ni kazi za kina mama. Halafu unadhani tunaoamini hivyo ni sisi wanaume tu? Wala, mbona mpaka hao wanawake wenyewe wanaamini hivyo.

Na kwa sababu hiyo, ndiyo maana mwanamke akitokea kupata mwanamume anayefanya kazi za nyumbani huona kama ameokota dhahabu, atapita anamtangaza saluni zote; ‘mie mbona mume wangu anafua nguo zetu kila Jumapili, na chakula tumeweka zamu ya kupika, yeye Jumatatu mpaka Jumatano, mimi Alhamisi mpaka Jumamosi.

Na wale ambao hatufanyi hivyo tunaonekana hatujali hata kidogo. Lakini kuanzia leo, napenda wanawake wafute mtazamo huo vichwani mwao, nitawaeleza kwa nini.

Nataka wanawake wajue wanaume wasiofanya kazi za ndani wanajali, tena wanajali kuliko hata wanaume wanaofanya kazi za nyumbani.

Kwa sababu vuta picha mwanamume unaosha vyombo, mke wako yuko sebuleni anatazama TV, halafu mara mama yako anakuja kuwatembelea, anafika anakuta mwanaye unaosha vyombo, mke yuko sebuleni anatazama tamthilia, unadhani kitu gani cha kwanza kitakachoingia kichwani kwa mama yako?

Au hata wake zetu, nao si wana kaka zao, vuta picha mke wako amekwenda kumtembelea kaka yake, anafika anakuta wifi yake yuko nje anasuka, halafu mume yuko jikoni anakuna nazi ili apike mboga hapo akiwa tayari ameshaivisha wali.

Unadhani kitu gani cha kwanza kitatembea kichwani mwa mke wako? Wanaume wasiofanya kazi za nyumbani wana majibu.

Wanaume tunaokataa kazi hizi tunajali sana, tunawapenda wake zetu, hatufanyi kazi za nyumbani kwa sababu hatutaki kuwagombanisha wake zetu na mama zetu, hatutaki dada zetu wawakalie shingoni kuwaambia mmeturoga, si unajua mawifi na wakwe wa kibongo wanavyoongea, kwa hiyo tunajaribu kuepusha migogoro isiyo ya lazima inayoweza kuvunja familia.

Na kimsingi wala hakuna tatizo kwa mwanamume kufanya kazi za nyumbani, mbona watu wanaoishi kwa kufuata taratibu za kimagharibi wanafanya na hakuna wanachopungua. Tatizo ni walimwengu hapa nchini.

Kwa hiyo kama unaona unatamani sana mumeo afanye vitu za namna hiyo basi hakikisheni angalau mnatengeneza kautaratibu fulani kanakoondoa aibu kwa mume wako machoni mwa walimwengu kwa sababu kama tulivyosema, hakuna tatizo lolote mwanamume kufanya kazi za ndani lakini tatizo ni walimwengu.

Na hatuwezi kuishi kama vile ni vipofu wa walimwengu, kwamba hatuwaoni, hapana, lazima tuwazingatie.

Kumbuka, kwa familia zinazoishi kwa kufuata taratibu za kimagharibi hayo ni mambo madogo sana, hayana shida yoyote, lakini kwa kina sisi Waswahili, hayo mambo hatujazoeshwa, kwa hiyo tunapofanya, tuyafanye polepole dada na mama zetu wasije kuwaambia mmetupa limbwata.