Ziara ya Kinana Zanzibar yairejeshea CCM uhai

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana akiwa katika harakati zake za kisiasa za kujenga uhai wa CCM Visiwani Zanzibar . Picha na Mwinyi Sadallah.
Muktasari:
Ziara za Kinana mikoani, zinatajwa kuwa na tija kwa chama tawala, kutokana na kuchangia kurejesha uhai wa chama hicho kwa wananchi.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana akifuatana na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kisiwani Zanzibar imefufua matumaini ya wanachama wa chama hicho tawala.
Kilichosababisha kufufuka kwa matumaini hayo ni kauli alizozitoa kiongozi huyo wa CCM mbele ya viongozi na makada wa chama hicho kisiwani hapa.
Kinana katika hotuba zake, hakuhubiri siasa na badala yake ni kama aliyekuwa anawafunda viongozi na makada wa chama hicho tawala na kuhimiza upendo, umoja na maelewano ndani ya chama hicho.
Alitumia muda mwingi wa hotuba zake sehemu mbalimbali kuwakumbusha wabunge na wawakilishi kufanya kazi kwa kushirikiana na mwisho akawahimiza watendaji wa ngazi mbalimbali za kisiasa katika chama hicho kushusha mabega yao chini, kuepuka itifaki ndefu na mbwembwe alizosema hazina tija wala maslahi kwa CCM na wananchi wanaowawakilisha.
Kinana akawaambia watendaji hao wa CCM kuwa ni jambo lililowazi kwamba upendo na umoja unapokosekana katika taasisi au kundi hupoteza malengo na madhumuni ya taasisi husika.
Alisema hali hiyo inapotokea hujenga ufa na mgawanyiko, lakini pia husababisha viongozi kushindwa kuwafikia wanachama na wale wanaowawakilisha jambo alilosema lina athari kubwa inayoweza kuzaa madhara na hasara kwa taasisi wanayoiongoza.
Kinana hakuishia hapo, aliwaonya viongozi wenye tabia ya kubaki maofisini na kushindwa kukisaidia chama hicho kubadilika na kuanza kushughulikia kero na matatizo yanayowakabili wananchi.
Aliwakumbusha viongozi wa CCM Zanzibar kuwa, kabla ya kuchaguliwa kwao walikuwa wanyonge na wenye mikakati ya kukijenga chama lakini baada ya kuwa viongozi sasa wanatamani kuvaa majoho ya utukufu.
Akionekana kusema yale yanayowagusa na kuwakera wana-CCM wengi; Katibu Mkuu huyo aliwaambia watendaji hao wa CCM kuwa, hakuna mheshimiwa wala anayetamani kudharauliwa ndani ya chama hicho na badala yake wajue kuwa wanachama na viongozi wote wanastahili heshima ya kutambuliwa utu wao bila kudharauliwa au kupuuzwa.
“Hiyo ndiyo misingi iliyoachwa na vyama vya Tanu na ASP ambayo imerithiwa na chama chetu, hivyo kila aliyekubali kukitumikia chama hiki anatakiwa kuweka mbele maslahi ya umma kabla ya kujitazama yeye,” alisema.
Kinana alisema matumizi na neno mheshimiwa si ya CCM na badala yake kauli yao ya msamaiti wa asili ni ndugu na si vinginevyo. Aliwataka wabunge, wawakilishi na madiwani kuacha kujiita wao ni waheshimiwa au wanapopigiwa simu na wananchi kutoa visingizio ili kukwepa kusikiliza matatizo yao.
Aliwakumbusha kazi ya kisiasa ni ya kujitolea na si ya kulipwa ujira au kudai posho, “anayefanya kazi za kisiasa kwa kutegemea posho akae pembeni ili kuwapisha wenzake wakiendelea na kazi ya kukiendeleza chama hicho.”
Aliongeza; “Wapo wanaojiona wapo tofauti na wengine kwasababu tu wameshika mpini wa madaraka au kuchaguliwa na wananchi kwenda Baraza la Wawakilishi na Bungeni huko Dodoma. Wanafikiri wana akili nyingi na maarifa kuliko watu wengine jambo ambalo si kweli na halina maana,” alisema.
Kiongozi huyo pia alisema, kuna haja na ulazima wakati wa kutafuta wagombea, demokrasia ikapewa nafasi yake; “wagombea wanaopendwa na kuaminiwa na wananchi kwa ushirikiano wao, uaminifu na utumishi bora, wasiwekewe mizengwe na badala yake waungwe mkono na kusaidiwa kushinda,” alisema Kinana na kuongeza:
“Na wale wagombea wanaoshindwa katika mbio za uchaguzi wawe waungwana wa kukubali matokeo na si kuunda makundi ya kuwapinga walioshinda.”
Hata hivyo Kinana alionekana kuwagusa wananchi na wanachama wa CCM Zanzibar kwa kutumia mtindo uliokuwa ukifanywa na Rais wa ASP, hayati Mzee Abeid Amani Karume ambaye hakuwa akijali wadhifa na cheo chake.
Kinana aling’oa visiki, kujenga nyumba za chama, alilima mashambani, kupanda mikarafuu bila kujali kama ni kiongozi wa juu wa CCM.
Apokelewa na mabango
Akiwa katika Kijiji cha Miwani Jimbo la Uzini, kiongozi huyo wa CCM alipokelewa na wananchi waliobeba mabangao yenye jumbe mbalimbali ambapo aliwapokea na kufuata bango moja baada ya jingine na kuyasoma.
Miongoni mwa jumbe zilizokuwapo kwenye mabango yale ni kukosekana kwa huduma za jamii. Barabara mbovu, ukosefu wa maji safi, zahanati, nyumba za waganga na wauguzi.
Mara baada ya kuyasoma Kinana alisema masuala yote hayo atayachukua na kuyawasilisha mbele ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Seriali ya Jamhuri ya Muungano ili hatua za utekelezaji zifanyike mara moja.
Aliwaambia kuwa kazi ya kuzisimamia SMZ na SMT ni za CCM ambao wamepewa dhamana na wananchi kupitia ilani yake ya uchaguzi mwaka 2010/15.
“Kitendawili kinabaki kwa wabunge na wawakilishi wanaoishi kama paka na panya kwenye majimbo yao,” alisema.
Hata hivyo ndani ya chama hicho kuna makundi ya hasama na kuwindana, hakuna maelewano wala upendo kama ule autakao Kinana uwapo na kudumishwa.
Hili sijui kama litapatiwa ufumbuzi au ni jambo la kuvunda lisilo ubani.
Hiyo ni kutokana na ubinafsi wa viongozi hao wa chama na uduni wa kutatua migogoro inayoendelea kuumiza wananchi.