Vyama vionyeshe misimamo yao kuhusu ubeberu

Rais Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya wenyeviti wa vyama vikuu vya siasa nchini. Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu,vyama havina budi kuweka bayana msimamo yao kuhusu ubeberu.Picha kwa hisani ya blogu ya bayana.
Muktasari:
Kwa hali ilivyo, Serikali iliyo madarakani na hata vyama vya siasa vinavyotamani kuingia madarakani, vinaonekana kushindwa kutengeneza mfumo wa kupambana na utatu huu.
Watanzania tuna changamoto tete ya kuuondoa utatu usiokuwa mtakatifu, yaani umaskini, ujinga na maradhi.
Kwa hali ilivyo, Serikali iliyo madarakani na hata vyama vya siasa vinavyotamani kuingia madarakani, vinaonekana kushindwa kutengeneza mfumo wa kupambana na utatu huu.
Mapambano ya kuondoa utatu usiokuwa mtakatifu yanakwenda mbali zaidi ya matamko ya kisiasa. Ni lazima tutambue kwamba bila jitihada kubwa kuhakikisha tunapata elimu nzuri na bora, afya nzuri kwa kila Mtanzania na uhuru wa kujieleza na kutenda, ni vigumu kuyafikia mabadiliko tunayoyatarajia.
Mabadiliko yataletwa na elimu. Mabadiliko hayataletwa na asasi za kimataifa. Asasi zinajenga uwezo kwa kulenga matakwa ya nchi zinazotoa fedha. Misaada ya kujenga uwezo inalenga nini na wapi? Nani anapendekeza eneo la kujenga uwezo?
Elimu ndiyo nguzo ya mabadiliko, lakini ni elimu ipi? Ni elimu ya kujitambua na kujifanyia tathimini au ya kutaka kuwa kama mabeberu? Mabadiliko hayawezi kuja bila uongozi sikivu na wenye ari ya kujifunza kusikiliza.
Kubadilisha mwelekeo wa mabadiliko na kuubatiza jina la kupunguza umaskini ni mbinu chafu za kibeberu! Afrika imepotea, imemezwa katika nyanja zote. Hivyo mabadiliko ni ajenda muhimu katika bara letu na hasa katika Taifa letu la Tanzania.
Tunahitaji shule nzuri na vyuo ili kufikia mabadiliko ya kweli. Vyuo vyetu vikuu viwe chachu ya mabadiliko. Tafiti mbalimbali zisisubiri wahisani au Serikali bali zisukumwe na bidii ya kutaka kuleta mabadiliko. Ni bahati mbaya kwamba viongozi wetu wamebaki kuimba kaulimbiu na kutoa ahadi. Wapinzani nao wameelekeza nguvu zao katika kulaumu na kukosoa.
Wote kwa pamoja wamemezwa na misemo ya ghiliba za mabeberu: utawala bora, kurekebisha uchumi, ubinafsishaji na utandawazi.
Mabeberu wanafadhili vyombo vya habari na kuvielekeza viandike yale yanayoendana na sera za kibeberu. Sekta zote zimeingiliwa kwa kisingizio cha ufadhili; na kila ufadhili ni lazima uandamane na masharti pamoja na fungu la kulipa wataalamu washauri kutoka nje; fungu la makongamano na semina na mambo mengine ambayo kwa njia moja ama nyingine yatazirudisha fedha zao kule zilikotoka.
Serikali yetu inaendeshwa kwa msaada wa fedha za mabeberu; wanatujengea barabara, wanajenga shule na hospitali. Wanapotoa misaada hiyo, tunaambiwa uchumi wao si mzuri na watu wao hawana kazi na makazi. Kwanini watusaidie sisi huku, wakati wao wana matatizo kibao?
Hakuna mwanasiasa hata mmoja anayesimama na kueleza msimamo wa Tanzania juu ya kutawaliwa na ubeberu na kuutumikia ubeberu.
Tunaambiwa kwamba ubeberu unaongoza mabadiliko katika nchi za Afrika kwa manufaa ya nchi hizo za kibeberu.
Takwimu za kuaminika zinaonyesha kwamba idadi ya wataalamu 100,000 kutoka nchi za kibeberu wako Afrika, wakifanya kazi na ushauri kwa kulipwa dola bilioni 4. fedha ambazo zingeweza kuchangia kuleta maendeleo, zinarudi kwao kwa njia ya mishahara ya wataalamu.
Misaada, ruzuku na mikopo inatolewa kwa malengo ya kuendeleza ubeberu katika nchi za Kiafrika. Wachumi wanaoishauri Afrika na mashirika ya kifedha ya hawafanyi vizuri kwao, lakini kila wakija Afrika, wanapokelewa vizuri tena kwa zulia jekundu.
Yahitaji msimamo kupambana na ubeberu
Bila kuwa na msimamo thabiti dhidi ya ubeberu, hatuwezi kupiga hatua ya kweli kuelekea mabadiliko tuyatakayo. Ubeberu ni ubepari kandamizi ambao hauongozwi tena na mtaji pekee bali pia na mashinikizo na hila za mashirika ya kimataifa na nguvu za kijeshi.
Ni ubepari kandamizi uliovuka mipaka na kuenea dunia nzima. Ni ubepari usioangalia utu wa watu, usioangalia uharibifu wa mazingira bali faida. Ni ubepari ambao Mwalimu Julius Nyerere, aliubatiza jina la unyama.
Lenin, aliuelezea ubeberu kuwa ni ubepari uliokomaa na kupevuka ambao mhimili wake ni kusambaa kwa mitaji, uwekezaji katika nyanja za fedha, viwanda na biashara. Ubeberu huu katika Afrika ulisambaa kupitia mfumo wa ukoloni.
Ukoloni wa Kifaransa ulisambaza viwanda na uwekezaji mwingine katika makoloni yake yote. Uingereza ilifanya hivyo hivyo. Kwetu sisi na hadi leo bado kuna uwekezaji huu wa kibeberu ulioanza kwenye karne ya 19. Ubelgiji ilifanya hivyo kule Congo.
Lenin, kwa wakati wake hakuchambua kwa kina juu ya siasa ya ubeberu wa zama hizi za utandawazi, ingawa upo uhusiano mkubwa kati ya uchumi wa kibeberu na siasa za kibeberu.
Uhusiano wenyewe ni kwamba dola hupaswa kulinda maslahi ya kibeberu kwa gharama yoyote.
Katika mfumo wa kibeberu dola haiwezi kujenga na kudumisha mfumo wa kidemokrasia unaojali haki na masilahi ya wazalishaji. Kazi ya dola linalomilikiwa na mabeberu, ni kuweka mazingira mwafaka ya ulimbikizaji kwa manufaa ya mabeberu.
Kukumbatia siasa za kibeberu ni kuruhusu wageni kuhodhi njia kuu za uchumi. Kama njia kuu za uchumi wa nchi zinahodhiwa na kampuni na mashirika ya kibeberu, maana yake dola inakuwa wakala wa mabeberu. Hili likitokea ni aina nyingine ya ukoloni. Tutakuwa na uhuru wa bendera, lakini tunaishi kwenye nchi ambayo uchumi wake unaendeshwa na mataifa ya nje.
Bila kubadili sura ya uchumi wa kibeberu, si rahisi kuwa na mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia. Maana kazi ya siasa ni kulinda maslahi ya kiuchumi ya tabaka lililohodhi njia za uzalishaji.
Kama uchumi wa nchi unahodhiwa na wageni, kazi ya wanasiasa na serikali itakuwa ni kuwalinda wageni na masilahi yao. Kama uchumi utakuwa na sura ya kitaifa na utakuwa mikononi mwa wazalendo, kazi ya siasa na serikali itakuwa ni kuwalinda wazalendo na masilahi yao ya kiuchumi.
Tunapoelekea uchaguzi mkuu
Hivyo tunapoelekea uchaguzi mkuu, ni muhimu kwa vyama vya siasa kuonyesha msimamo ulio wazi. Vyama hivi viko upande gani? Viko upande wa wazalendo au viko upande wa wageni?
Hili ni lazima lionekane wazi, ni vigumu kuwa swahiba wa pande hizi mbili. Huu ni wakati wa vyama kutangaza misimamo yao katika suala hili nyeti.
Bahati mbaya hatujajadili vya kutosha namna ya kufanya mabadiliko ya siasa na uchumi katika nchi yetu. Bila kufanya hivyo historia itatuhukumu kwa usaliti na unafiki. Bila kuwa na msimamo thabiti dhidi ya ubeberu hatuna haki ya kusema tunataka mabadiliko.