Sababu wana Hiphop kuachana na ngumu nyeusi

Kwa miaka mingi nchini wasanii wa Hip Hop au Rap walifanya harakati zao kupitia muziki huo. Wasanii kama Sugu, Profesa Jay, Wagosi wa Kaya, Kali P, Afande Sele, Izzo Bizness, Roma, Bonta, Nay wa Mitego, Kala Jeremiah na wengineo wanasifika kwa kutoa nyimbo zilizopeleka ujumbe kwa watawala na mamlaka za Serikali, kitu ambacho kwa siku za karibuni kimekuwa nadra.

Mwananchi limefanya mahojiano na wasanii waliowahi kufanya aina hiyo ya muziki, kusikia kwa nini hivi sasa hakuna ngumu nyeusi.


Nikki Mbishi

Rapa huyu ambaye wimbo wake “I’m Sorry JK” ulifungiwa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) anasema wanamuziki wamekuwa wakitumika kwenye kampeni za kisiasa, hivyo kuna hali ya kufungamana kati yao na wanakosa uhuru wa kusema au kukosoa. “Hata mwanzo ilikuwa hivyo maana sio maadui, sanaa ilikuwa huru inajitegemea na kutumika kama hamasa kwenye shughuli za kisiasa, ukilipwa ngumu kumkosoa kiongozi wa namna hiyo hata kama anakosea,” anasema Nikki. “Sheria zimekuwa nyingi, watu wanaogopa, sijui wanatekwa, unakamatwa, mara unahojiwa kwa nini hiki, vitu kama hivyo, tulishapitia sisi wengine,” anasema na kuongeza:

“Watu wanaangalia familia zao, malengo yao, tofauti na zamani msanii alikuwa ni mtu wa jamii, anazungumzia matatizo kama walivyofanya kina Sugu wakati wanaanza,” anasema Nikki Mbishi.

Nikki anadai kuwa miaka ya nyuma wasanii walikuwa wanapanda majukwaa waliyoitwa na wanasiasa na kuimba nyimbo kuhusu wanasiasa hao hao, lakini sasa hivi huwezi kufanya hivyo.

“Watu wanaona bora tuwaimbie walevi, hata hao wenye media wanaogopa wakicheza wimbo kama huo kuna Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), itawatia matatani, sasa nani anataka mambo kama hayo?” anasema na kuhoji Nikki.

Ukitoa ‘I’m Sorry JK’, nyimbo nyingine za Nikki Mbishi zilizozungumzia masuala ya kisiasa na kijamii ni ‘Natoka Tanzania’ na ‘Sauti ya Jogoo’ ambao umebeba jina la albamu yake ya kwanza.


Kala Jeremiah

Anasifika kwa utunzi mzuri wa masuala ya kisiasa na kijamii, ametoa ngoma maarufu kama ‘Wimbo wa Taifa’ aliomshirikisha Nakaaya Sumari, ‘Nchi ya Ahadi’ aliomshirikisha Roma, ‘Wale Wale’ aliomshorikisha Ney wa Mitego na Nay Lee, ‘Ready to Die’ aliofanya na Nay Lee.

Ngoma zote hizi zinazungumza masuala mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi na mamlaka za Serikali.

“Mimi nadhani ndio nilikuwa mwanzilishi kwa kusema ile moja kwa moja licha ya kaka zetu, Wagosi wa Kaya walikuwa wameshaanzisha, lakini ile ya kusema moja kwa moja nilianza mimi akafuata Roma. “Mimi nishaimba kila tu, ukitaka wimbo wowote kuhusu kitu chochote ukienda kwenye maktaba (YouTube) ya Kala Jeremiah utaupata.”

Kuhusu madai kuwa aina hiyo ya muziki inafungiwa, Kala anasema sio kweli, kwani yeye tangu ameanza muziki hakuna wimbo wake wowote uliofungiwa na Basata, akieleza uandishi uliobalansi mambo hauwezi kuleta shida.

“Sana sana Basata walishawahi kunipongeza kwa kufanya muziki mzuri wa kuelimisha jamii, na mimi ndiye msanii pekee mwenye barua au cheti rasmi kutoka serikalini kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutambua mchango wangu kulisaidia Taifa kwenye mambo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Hata ukiwa mwandishi wa habari, ukibalansi vizuri stori yako uliyemlenga akisoma ataona unataka ajifunze kitu, shida ni namna ya uwasilishaji. Tofauti na hapo nakuchana ukisikiliza unaona kina ukweli na sijaongeza chumvi au sijafanya kwa nia ya kukudhalilisha,” anasema Kala.


Izzo Bizness

Alifunika zaidi pale alipoachia ngoma yake ‘Rizi One’, akimtaka aongea na mshua, Izzo Izzo Bizness anasema kwa kuachia wimbo tu tayari ametimiza wajibu wake na changamoto alizoimba humo hadi leo zipo, hivyo sio suala la kutoa wimbo mwingine kama huo bali ni kukumbusha changamoto hizo zitatuliwe.

“Nimeimba kuhusu rushwa ambayo hadi sasa ipo, wazee kupewa mafao yao kwa wakati pale wanapostaafu, matatizo ya dawa ya kulevya, kazi kutolewa kirafiki au kindugu, hivyo vitu vipo hadi sasa bado vipo havijafanyiwa kazi.

“Juzi Nay wa Mitego ametoa wimbo amezungumzia mambo haya haya, kabla ya ‘Rizi One’ kuna wimbo nipo na Mwasiti upo kwenye EP yangu unaitwa ‘Maisha Yamepanda Bei’, unaelezea jinsi maisha yetu yalivyopanda bei, nimegusia vitu wazazi wetu wapitia na hali ya uchumi ilivyo na namna wananchi wanavyoteseka.

Wagosi wa Kaya

Kundi hili linasifika kwa mtindo wake mzuri wa kuwasilisha ujumbe, wametoa nyimbo kali kama ‘Wauguzi’, ‘Tanga Kunani’, ‘Trafiki’, ‘Walimu’, ‘Kero’, ‘Bei Juu’, ‘Fat na Soka’, ‘Dereva’ na nyinginezo.

Mkoloni kutoka Wagosi wa Kaya anasema sanaa inatumika kwenye jamii kuburudisha, kuelimisha, kuonya, kutoa tahadhari na kufikisha ujumbe kupitia vyombo vya habari, ila sasa mzani umeegemea kwenye kuburudisha tu. “Si kwamba wasanii hawaoni, wanaona mambo mazuri na mabaya lakini wameamua kukaa kimya, labda hawaoni ni njia sahihi ya wao kupata kipato. “Jamii pia haitaki vitu hivyo ndiyo maana haiwaungi mkono, kila siku wanapenda starehe na vitu vya kufurahisha, ndiyo maana hata waliokuwa wanaitetea wameamua kuachana na hizo nyimbo. “Msanii anaona akiimba nyimbo za starehe atapata fedha, hata vyombo vya habari vinacheza zile zenye mlengo wa kibiashara siyo za kutetea jamii, hili ni tatizo.” “Kuna hatari kubwa inayokuja mbele, kwamba utakayetumia muziki kuelezea matatizo, kuonya, kukemea au kutahadharisha jambo fulani, usipokuwa makini utaonekana kama adui, sio mtu unayeitakia jamii hiyohiyo unayoitetea mema,” anasema Mkoloni.

Ikiwa jamii haina mwamko wa aina hiyo ya muziki je, Wagosi wa Kaya waliwezaje kufanikiwa? Mkoloni anasema ubunifu ndio kitu pekee kilichowasaidia kukubalika kwenye jamii.

Hata hivyo kuna wasanii waliingia matatani kutokana na mistari ya nyimbo zao. Mfano Machi 2017 Nay wa Mitego alishikiliwa na Jeshi la Polisi nchini mara baada ya kuachia wimbo wae ‘Wapo’ ambao unadaiwa kukosoa baadhi ya mambo serikalini na mwenendo wa viongozi fulani.

Aprili , 2017 msanii wa Hip Hop, Roma Mkatoliki naye alitekwa na baada ya kutoka madai yalikuwa hali hiyo ilitokana na aina ya muziki anaoufanya.

Hata hivyo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati ule, Dk Harrison Mwakyembe alitoa tamko kuwa hayati John Magufuli amesema msanii huyo aachiwe huru kwani naye ni mpenzi wa wimbo huo, akimtaka aongeze maneno mengine ikiwamo ya wakwepa kodi wanaoikosesha Serikali mapato.