Wahamasisha wanafunzi kusoma vitabu maktaba

Mkufunzi wa wakutubi kutoka Korea, Ja Youn Lee, akizungumza na wanafunzi mkoani Morogoro.Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
- Kimsingi, shuleni kunatajwa kama mahala ambako mtoto anaweza kukuza uwezo wake wa akili kwa ajili ya kupambana na changamoto za kimaisha.
- Kwa upande mwingine, methali hii inaweza kuwataka wazazi kuwajengea watoto msingi wa kusoma vitabu katika maktaba.
Samaki mkunje angali mbichi. Methali hii inaweza kutumiwa kuwahimiza wazazi kupeleka watoto shuleni.
Kimsingi, shuleni kunatajwa kama mahala ambako mtoto anaweza kukuza uwezo wake wa akili kwa ajili ya kupambana na changamoto za kimaisha.
Kwa upande mwingine, methali hii inaweza kuwataka wazazi kuwajengea watoto msingi wa kusoma vitabu katika maktaba.
Usomaji vitabu ni njia mojawapo ya kupanua akili ya binadamu.
Binadamu anayependa kusoma, anairutubisha akili yake kuelewa mambo mbalimbali yanayomzunguka maishani.
Kampeni ya Tanzania ya Kesho
Ili kujenga utamaduni wa kujisomea ambao kwa Watanzania wengi umewashinda, baadhi ya wadau walianzisha mradi wa Tanzania ya Kesho unaohamasisha wanafunzi kusoma vitabu katika maktaba.
Mkufunzi wa wakutubi kutoka Korea, Ja Young Lee anasema lengo la Tanzania ya Kesho ni kumfumbua macho na kumwamsha mwanafunzi wa Kitanzania kutoka usingizini.
Hilo anasema linaweza kufanyika kwa kuwahamasisha wanafunzi wa shule ya msingi kutumia maktaba na kupenda kusoma vitabu.
“Programu ya Tanzania ya Kesho ina lengo la kuwajengea wanafunzi kupenda kujua historia kwa kusoma vitabu mbalimbali,” anasema na kuongeza:
“Maktaba ndiyo sehemu rafiki ya kusoma vitabu kwa njia nzuri kwani vitabu vimekuwa viuzwa bei ghali lakini maktaba kuu za mikoa ni rahisi kufikika kwa wanafunzi.’’
Anasema mpaka sasa tayari wakutubi 18 kutoka mikoa ya Dodoma na Morogoro, wamepatiwa mafunzo ya kuwahudumia wanafunzi kutumia maktaba na kujisomea vitabu.
Anaeleza kuwa katika maktaba nyingi za Tanzania, kumejaa vitabu vya lugha ya Kiingereza na hivyo kuwawia ugumu wa wanafunzi wasiojua Kiingereza.
Kwa kugundua udhaifu huu Ja Young anasema aliamua kutafsiri vitabu 50 vya masomo mbalimbali kwa ajili ya watoto wa Kitanzania.
Mmoja wa wakutubi walionufaika na mafunzo hayo, Judith Lugongo anasema kuwa amejifunza namna ya kuandaa mpango wa maktaba kuhusu kuwafundisha watoto, namna ya kuchagua vitabu vya kusoma na kupata maarifa mbalimbali.
Aidha, anaeleza kuwa licha ya kupata maarifa ya kuwafundisha watoto, sasa ana ufahamu wa kutosha wa kufundisha jamii namna ya kutumia maktaba kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali kwa kutumia machapisho.
“Nimefurahi kupata mafunzo; mkufunzi Ja Young Lee ni mbunifu kwani licha ya kutupatia mbinu mbalimbali za kufundisha watoto na kuhudumia jamii, ameweka kivutio cha watu wanaotembelea maktaba kupata fursa ya kupima urefu na uzito pasipo malipo,’’ anaeleza.
Mkutubi mkuu wa maktaba ya Mkoa wa Morogoro, Edward Fungo anaeleza kuwa mafunzo hayo yameongeza ufanisi kwa upande wa uongozi wa maktaba kwa kutengeneza vivutio kwa wanafunzi kuvutiwa kusoma vitabu.
Anasema baada ya mafunzo hayo wametengeza programu maalumu kwa wanafunzi wote wa shule za msingi kuingia maktaba na kusoma vitabu bure siku za Jumamosi.
“Wakutubi wetu nane wamefaidika na mafunzo haya. Wanafunzi wamehudumiwa kulingana na muongozo wa mafunzo unavyolenga namna ya kuwahudumia na kutengeneza ushawishi wa usomaji wa vitabu maktaba,”anasema.
Mwanafunzi wa darasa la nne, Shule ya Msingi Mwere A mkoani Morogoro, Ally Hassan anasifu jitihada za kutafsiri vitabu hasa vya hadithi kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Kitendo cha vitabu vya Kiingereza kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, kitasaidia wanafunzi kuingia maktaba na kusoma vitabu vingi,’’ anasema na kuongeza:
‘’Lugha ya Kiingereza imekuwa siyo rafiki kwa wanafunzi wengi na maktaba vitabu vya Kiswahili vipo vichache tofauti na vile vya Kiingereza.’’