Ushauri na unasihi usivyopewa nafasi shuleni

Wanafunzi kama hawa wanahitaji ushauri na unasihi kuhusu masomo, ajira na maisha kwa jumla. Picha na mtandao wa huffingtonpost
Muktasari:
- Wanafunzi wa aina hii ni wengi, wamejaa katika taasisi nyingi za elimu ya juu nchini. Inasikitisha kuwa hadi kufikia kiwango hicho cha elimu, kijana wa Kitanzania hajui kwa nini anasoma anachosomea sasa chuoni.
Jenga taswira hii katika fikra zako. Unakutana na mwanafunzi wa elimu ya juu nchini, unamuuliza kwa nini alichagua kozi anayosemea, lakini anakosa jibu mwafaka.
Wanafunzi wa aina hii ni wengi, wamejaa katika taasisi nyingi za elimu ya juu nchini. Inasikitisha kuwa hadi kufikia kiwango hicho cha elimu, kijana wa Kitanzania hajui kwa nini anasoma anachosomea sasa chuoni.
Pius Msomba, ni mwanafunzi wa sanaa na ualimu katika Chuo Kikuu cha St Augustine Songea, anasema hakutegemea kama angekuja kuwa mwalimu na anapokumbuka safari yake ya elimu tangu akiwa ngazi ya awali, hakumbuki kupata ushauri kuhusu masomo au kazi.
Kitendo cha Msomba kusomea kozi asiyoitarajia, ni matokeo ya wanafunzi wengi nchini kukosa ushauri na unasihi kuhusu masomo na ajira tangu wakiwa katika madaraja ya chini ya elimu.
Mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Christian Bwaya anasema, ushauri wa masomo na ajira ni mwongozo wenye lengo la kumsaidia mwanafunzi ili aweze kujitambua na kubaini uwezo alionao katika masomo na kazi
Ni ushauri wenye faida mbalimbali ambazo Bwaya anazitaja kuwa ni pamoja naa kumsaidia mwanafunzi kujitambua na kujua uwezo wake ili anapofanya uamuzi afanye akiongozwa na uelewa badala ya kukurupuka.
Pia, humsaidia kutambua kazi zilizopo na kujua zinahitaji sifa zipi na uwezo wa namna gani na kumwezesha kurekebisha uamuzi aliyoyafanya kimakosa.
Anasikitika kuwa pamoja na umuhimu wa program hizi, shule nyingi nchini zinashindwa kuziendesha kwa mtazamo kuwa ni programu zinazopaswa kuendeshwa na shule za kimataifa.
Anasema hata walimu hawafundishwi kwa undani somo la unasihi, hivyo wengi wanashindwa kuwa wanasihi, taaluma anayosema inahitaji watu waliosomea.
“Walimu wenyewe hawaelewi na hawana uwezo wa kumshauri mwananfunzi vyema katika masomo au kufuata kitu fulani” anasema Bwaya.
Bwaya anasema kama wanafunzi wangepewa huduma ya ushauri wa masomo na ajira, ingewasaidia kuwa watulivu kiakili na hisia, kwa kuwa wanakotoka nyumbani hukutana na changamoto nyingi katika familia na jamii. Kwa upande mwingine ushauri huu unaweza hata kusaidia kukuza ufaulu kwenye mitihani.
Mdau wa elimu, Hussein Madeni anaeleza kuwa ingawa taaluma hii haifanyi vizuri hapa nchini kutokana na uelewa mdogo wa jamii, ukweli ni kuwa ni huduma inayohitajika mno kwa mzazi, mwanafunzi na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu.
‘’Ushauri wa stadi za maisha kwa wazazi, wanafunzi na jamii kuhusu elimu ya mazingira yanayowazunguka, vina nafasi kubwa katika kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo, achilia mbali mbinu za kujieleza, kupambana na msongo wa mawazo na hisia, uwazaji, ubunifu, utoaji uamuzi na uongozi,’’ anasema.
Anaongeza: ‘’Kuna mifano ya wanafunzi wanaoomba chuo huku hawajui wanaomba kozi gani na sababu gani wanaomba kozi hizo.’’
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kidete, Masalu Fortunatus, anasema kimsingi walimu wana nafasi kubwa ya kutimiza ndoto za wanafunzi wao ikiwa watawapa mwongozo unaofaa kuhusu maisha yao.
Japo shule anayofundisha haina programu maalumu za kishule kuhusu ushauri na unasihi, anasema baadhi ya walimu hutumia mikusanyiko ya klabu za wanafunzi kuwapa mawaidha kuhusu masomo na ajira.
“Katika kipindi unaweza kutenga dakika 15 kuwaeleza wanafunzi kupitia sayansi ya jamii na lugha lakini ni muda ambao hautoshi kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi, labda walimu wa madarasa wanaweza kutumia muda wao wakati wa kukutana na wanafunzi wao,”anasema.
Mwalimu huyu anakiri kuwa naye ni mwathirika wa mfumo wa shule nyingi kutokuwa na programu za ushauri na unasihi kwa wanafunzi.
“ Sikupata nafasi ya kushauriwa, nilichokipigania hakikutimia, ndio ikanilazimu kusomea ualimu baada ya kukosa mtu thabiti wa kunishauri na kusimamia ndoto zangu,’’ anaeleza.
Ushauri tangu mapema
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema ili kuwe na tija kwa programu za ushauri na unasihi, hazina budi kuanza kwa wanafunzi tangu wakiwa ngazi ya elimu ya awali
“Wataalamu wa elimu na wasomi wanatakiwa waendelee na kukazia suala hili lifanyike kwa kila ngazi ya elimu ili iwe msingi bora wa watu kutimiza kile walichokusudia na pia nchi itanufaika kwa kuwa utendaji utabadilika na mtu atafanya kazi kwa kuipenda, maana ameishi katika ndoto yake, anasema na kuongeza;
‘’Mitalaa ya elimu katika shule izingatie masuala ya ushauri na kuwaongoza walimu kuitumia kama moja ya utekelezji wa kutoa elimu kwa jamii, ili kupata mafanikio yenye tija katika elimu na kwengineko.
Mchango wa wazazi
Kama ulivyo uhalisia kuwa mwalimu wa kwanza ni mzazi, ushauri na unasihi kuhusu elimu na maisha vinapaswa kujengewa misingi kwa watoto tangu wakiwa nyumbani, kwa kuwa wazazi ndiyo wang’amuzi wa kwanza wa uwezo wa kiakili wa mtoto.
Bakari Heri ni mzazi wa mtoto anayesoma darasa la kwanza, anasema amekuwa karibu mno kujua nini mwanawe anakipenda kwa maisha ya baadaye ili aanze kujenga mazingira ya kumwezesha kufikia matarajio yake.
“Najivunia kuwa ni mmoja wa wazazi makini, nipo karibu na walimu wake na huwa nawauliza wanamuonaje mtoto wangu na pengine uwezo wake uko katika masomo gani,’’ anaeleza na kuongeza:
“ Ukaribu wangu kwake umeniwezesha kung’amua kuwa anapenda kuwa daktari, hivyo kwa sasa mimi na mama yake tumekuwa tukimsisitizia kujifunza kwa juhudi masomo kama hesabu kwa kuwa ni msingi wa masomo ya sayansi.’’
Ushauri na unasihi kama fursa
Madeni anasema ushauri na unasihi, ni huduma inayoweza kutumiwa kama fursa ya walimu kujiongezea kipato.
Hata hivyo, anashangaa kuwa walimu hata wale waliosomea masuala haya, wanashindwa kufungua kampuni za ushauri na unasihi.