Teknolojia ya mionzi: Tamu na chungu ya tiba ya mionzi kwa mwanadamu

Mgonjwa huyu anahudumiwa kwa kupitia tiba ya mionzi hospitalini. Pamoja na uzuri wake aina hiyo ya tiba ina athari kubwa kwa mwanadamu isipotumiwa kwa usahihi. Picha kwa hisani ya mtandao wa www.kalenehospital.com

Muktasari:

Daktari huyo anatajwa kufariki kutokana na kansa ya damu, na baadhi ya watu waliokuwa karibu nae kikazi,  wakiwemo waliokuwa wanafunzi wake, wanabainisha kuwa daktari huyo baadhi ya nyakati hakuwa akivaa vifaa  vya kumkinga na mionzi.

Daktari bingwa wa masuala ya mionzi katika hospitali moja kubwa nchini aliyefariki miaka kadhaa iliyopita, kifo chake kinahusishwa na athari za mionzi aliyokutana nayo kazini kwake katika chumba cha X-Ray, hospitalini hapo.

Daktari huyo anatajwa kufariki kutokana na kansa ya damu, na baadhi ya watu waliokuwa karibu nae kikazi,  wakiwemo waliokuwa wanafunzi wake, wanabainisha kuwa daktari huyo baadhi ya nyakati hakuwa akivaa vifaa  vya kumkinga na mionzi.

Ikiwa ni miaka kadhaa sasa tangu afariki, watoto zake wawili aliowaacha wangali wadogo, nao wanasumbuliwa na kansa ya damu na hata shule wanazosoma wamewekwa katika uangalizi maalum dhidi ya watoto wenzao ambao ni watundu na wakorofi.

Daktari huyo ni mmoja kati ya maelfu ya watu ambao wanapoteza maisha, kupata saratani na magonjwa mengine kutokana na athari za mionzi iwe ya X-ray, T-scan au Utra sound ama kwa kukutana nayo moja kwa moja au kutokana na kutumia huduma hizo mara kwa mara.

Kulingana na ripoti ya Kamati ya Wanasayansi ya Shirika la Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Athari za Mionzi ya Nguvu za Atomic (UNSCEAR), tiba ya mionzi inachukua asilimia 98 ya vyanzo vyote vya mionzi ulimwenguni.

Tiba hiyo ambayo ni pamoja na X-Ray, CT Scan, Utra Sound na matumizi ya mionzi katika kutibu saratani,  kwa kiwango kikubwa ina madhara kwa binadamu na inaweza kusababisha kifo hasa kwa mtumiaji wa mara kwa mara.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya mionzi katika tiba kuliko wakati mwingine, huku ikikadiriwa kuwa zaidi ya vipimo bilioni 3.6 vya X-Ray vinafanyika kila mwaka.

Mkufunzi wa mionzi katika Chuo cha Afya na Tiba Muhimbili, Experditor Mahanja anasema mionzi inayotumika katika X-Ray, Utra Sound, CT Scan ina athari kubwa inapokwenda moja kwa moja katika mwili wa mtu ambaye sio mlengwa.

Anabainisha kuwa mionzi ina athari za kimaumbile (Genetic) katika chembechembe hai katika mwili wa binadamu, na mtu anaweza kupata saratani ambayo inaweza kuhama kutoka  kizazi kimoja hadi kingine, huku  watoto wakizaliwa wakiwa na vilema na athari zingine.

"Hivi sasa sheria ni kali sana na udhibiti ni mkubwa kulingana na sheria za kimataifa" anasema na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo ndio maana kuna vizuizi maalum ambavyo vinatumika kwa wafanyakazi walio katika vyumba vya X-Ray ili kuwakinga na mionzi.

Anasema kila baada ya mwezi, vizuizi hivyo ((Throming Detector),husafirishwa hadi katika Kituo cha Tume ya Nguvu za Atomiki (IAEA) kilichopo Arusha kwa ajili ya ukaguzi wa kiwango cha mionzi ambayo ipo katika vizuizi hivyo.

“ Kila baada ya mwezi kuna kiasi cha mionzi ambacho kinatarajiwa kukutwa katika kizuizi hicho, na ikitokea dozi ikazidi mtumiaji inabidi atoe maelezo au kuondolewa katika utendaji kwani anakuwa hatarini" anasema.

Mahanja anatoa mfano wa mfanyakazi mwenzao mmoja ambaye kifaa chake kilikutwa na kiasi kikubwa cha mionzi kuliko kawaida baada ya kupelekwa kukaguliwa, hivyo alitakiwa kutoa maelezo.

“Sheria ni kali za usimamizi wa matumizi ya mionzi hivi sasa, na kutokana na kuongezeka kwa teknolojia athari za mionzi zimethibitiwa kwa kiasi kikubwa kwa watumiaji hivi sasa kuliko wakati mwingine” anaeleza.

Naye mwanasayansi mwandamizi katika Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC), Dk. Wilbroad Muhogora anasema kupiga X-ray au kutumia aina nyingine ya mionzi,  inapaswa kuwa jambo la mwisho kufanywa kwa mgonjwa kutokana na ukweli kuwa nishati hiyo sio rafiki kwa mwili wa binadamu.

Anasema athari za mionzi zipo wazi na hata jumuia ya kimataifa hulazimika kutoa uangalizi wa kipekee katika matumizi ya minururisho hiyo.

Anaeleza zaidi kuwa mfano rahisi wa athari ni mabomu ya nyuklia yaliyopigwa katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japani wakati wa mwisho wa Vita ya Pili ya Dunia Agosti  1945.

Dk Muhogora anasema athari za mionzi hiyo ya nyuklia zinatajwa hadi hivi sasa, kwani watu wengi bado wanazaliwa wakiwa na vilema, saratani za aina mbalimbali, kansa ya damu na athari zingine ambazo zinasababisha magonjwa ya kurithi na hata vifo.

Anasema bado matukio ya athari za mionzi kwa binadamu yapo mengi, na hata kuvuja kwa vinu vya nyuklia katika nchi za  Urusi Japani,  ni ishara za wazi kuwa mionzi ingawa ina faida, lakini pia ina athari mbaya kuliko inayofikiriwa.

"Mionzi katika maeneo hayo sio tu imeathiri binadamu bali pia hata mimea,  na ndio maana Serikali kupitia tume ya mionzi ilitoa tahadhari kwa umma kuhusiana na vyakula vinavyotoka nje hususan nchini Japan baada ya tukio la Fukushima" anasema.

Daktari wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa hospitali hiyo, anasema elimu zaidi inahitajika hususan katika hospitali za ngazi ya wilaya,  kwani vifaa vya kujikinga ni vichache na havikidhi haja.

"Utakuta katika hospitali ya wilaya kuna wafanyakazi wa X-ray watatu hadi wanne, lakini kifaa ni kimoja" anasema na kuongeza kuwa hali hiyo inahatarisha usalama kwa wale wasiovaa kifaa hicho wakati wa kazi.

Anaiomba serikali kuchukua hatu za makusudi kuhakikisha vyumba vya mionzi au X-ray vinapata vifaa vya kutosha, badala ya kuwa kama ilivyo sasa hususan katika hospitali za pembezoni.