Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Changamoto zilizopo katika kuunda mifumo ya elimu

Wanafunzi wakiwa darasani

Muktasari:

Mfumo wa elimu ni utaratibu mzima ambao nchi inajiwekea katika kuelimisha watu wake. Kwa kawaida elimu hii hutolewa katika shule za matayarisho, shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali. Pia huweza kutolewa kama elimu ya watu wazima.

Katika siku za hivi karibuni tumekuwa na mjadala kuhusu mfumo wetu wa elimu. Tumehoji ubora na uwezo wake wa kukidhi mahitaji ya kitaifa. Makala haya yanajaribu kuangalia changamoto zinazoikumba nchi zetu katika kuunda mifumo ya elimu.

Mfumo wa elimu ni utaratibu mzima ambao nchi inajiwekea katika kuelimisha watu wake. Kwa kawaida elimu hii hutolewa katika shule za matayarisho, shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali. Pia huweza kutolewa kama elimu ya watu wazima.

Nchi nyingi barani Afrika ziliwekwa chini ya utawala wa kikoloni baada ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1884-1885 ambapo nchi za kibeberu zilijitwalia na kugawana nchi zetu za Afrika.

Historia ya ukoloni, madhumuni na madhara yake kwa nchi hizi yameainishwa kwa undani zaidi na wasomi kama Walter Rodney katika kitabu chake cha ‘Jinsi Ulaya ilivyorudisha nyuma maendeleo ya Afrika’. Kwa ufupi, kitu cha kuzingatia ni kwamba chini ya ukoloni, mfumo wote wa nchi na sekta zake ikiwemo elimu zililenga kukidhi mahitaji ya kinyonyaji ya wakoloni.

Baada ya mapambano ya kupigania uhuru wa kisiasa kufanikiwa, ilionekana kuwa uhuru huo hautoshi kwani ukoloni mamboleo uliendelea kuwanufaisha mabeberu. Viongozi mbalimbali wa Afrika kama Kwame Nkrumah wa Ghana waliliona jambo hili mapema. Hivyo basi Tanzania baada ya kupata uhuru wake wa bendera mwaka 1961 ilidhamiria kupambana na madhara yaliyojiri wakati wa ukoloni katika sekta zote.

Mwaka 1967 Azimio la Arusha lilitangazwa ili kuweka mikakati ya kujiletea maendeleo kupitia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Sekta muhimu kama vile elimu na kilimo ziliundiwa sera mahususi zilizolenga kuleta maendeleo chini ya siasa hiyo.

Lionel Cliffe na John S. Saul, katika juzuu ya pili ya kitabu chao walichokihariri kuhusu Ujamaa nchini Tanzania, wamekusanya makala zinazoonyesha mwelekeo wa maendeleo yaliyolengwa kwa kipindi hicho.

Hata hivyo, kuanzia miaka ya mwisho ya 1970 ilionekana kuwa sera hizo zilikuwa hazileti maendeleo yaliyotarajiwa na watendaji wengi serikalini walianza kukata tamaa. Umaskini uliendelea kukua huku nchi ikizongwa na madeni makubwa kwa wafadhili na benki za kimataifa.

Ni dhahiri kuwa hali hiyo isingeweza kuruhusiwa iendelee bila ukomo. Kushindwa kwa sera hizo kulitokana na muundo wa uchumi wa ukoloni mamboleo ulioendelea licha ya kutangazwa kwa Ujamaa na Kujitegemea.

Uchumi wetu tegemezi uliogubikwa na ushauri na utaalam toka nchi za kibepari usingeweza kutoa ufumbuzi mbadala. Hivyo kuanzia miaka ya mwanzo ya 1980 hadi kufikia mwaka 1992 lilipopitishwa Azimio la Zanzibar, sera ya Ujamaa na Kujitegemea ilianza kupewa kisogo.

Mtazamo mpya

Kwa kweli hali hiyo ilikuwa lazima itokee kwani mtazamo wa nchi za kibeberu na mfumo wao wa ubepari ulikuwa umeshapiga hatua nyingine ya kutoka katika ukoloni mamboleo kuelekea uliberali mpya na utandawazi.

Uliberali mpya kama ilivyokuwa ukoloni mamboleo ni mwendelezo wa unyonyaji na ukandamizaji wa nchi zetu katika sura mpya chini ya ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.

Aina hii ya ubeberu ilishabikiwa sana na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Magareth Thatcher, na aliyekuwa Rais wa Marekani, Ronald Reagan.

Tabia ya uliberali mpya ni kughilibu nchi zetu kuwa zinaweza kupata mafanikio makubwa ya kimaendeleo kama zitakumbatia mitaji kutoka nje na kufungua milango kwa wawekezaji toka nchi za kibepari.

Kwa kuzingatia uliberali mpya, sera za nchi zetu zinaelekezwa katika kujenga uchumi wa kibepari kwa kutilia mkazo sekta binafsi na kurasimisha mali za wananchi ikiwemo ardhi. Pia zimeelekezwa katika kuiondoa Serikali katika uendeshaji wa uchumi wa nchi.

Yaani Serikali inakuwa msimamizi au mwezeshaji tu katika soko huria. Madhara ya msimamo huu yameshaanza kuonekana kwa serikali kushindwa kudhibiti mfumuko wa shughuli za wawekezaji na mwelekeo wa sekta binafsi ambayo badala ya kuleta maendeleo imeongeza machungu ya kudidimiza uchumi wa nchi na kunufaisha tabaka la mabepari uchwara wachache wanaoshirikiana na wawekezaji.

Athari kwenye elimu

Sekta ya elimu nayo haiwezi kuepuka madhara haya na siyo ajabu kuwa uboreshaji tunaofanya katika elimu, ukawa ni uwekaji wa mazingira mazuri kwa ajili ya uliberali mpya.

Hii ina maana ya kutoa wasomi watakaokumbatia uliberali unaohamisha rasilimali za nchi kwenda nje huku Watanzania walio wengi wakiendelea kusota katika lindi la umaskini. Watu wanaoonekana mafisadi hivi sasa watakuwa ‘cha mtoto’ mbele ya tabaka hili la ndani linalozidi kujengeka.

Mwelekeo wa shule zetu katika ngazi mbalimbali hauna dalili ya kutoa wanafunzi wanaoweza kudodosa kwa undani kwa nini nchi yetu inazidi kudidimia kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali.

Hii ni kutokana na mitalaa inayotengenezwa kwa kutegemea wafadhili na washauri wanaowataka wao.

Ni kweli kabisa kuwa Serikali imejaribu kutoa kipaumbele kwa sekta ya elimu kwa kuongeza bajeti ya elimu lakini jambo la kujiuliza ni, je, pesa hizo huwa zinaishia wapi?

Ukitembelea shule mbalimbali utagundua kuna matatizo makubwa. Licha ya ukosefu wa vitendea kazi na mazingira yasiyo mazuri ya kusomea, walimu wako katika hali ya kusononeka kwa ujira mdogo wanaopata.