Simulizi ya muuza kahawa ‘smart’

Umaridadi huficha umasikini, huu ni usemi anaoishi nao Robert Dickson (30) anayetafuta riziki kwa kutumia ubunifu wake mwenyewe.

Dickson ni mzaliwa wa Dodoma ambaye maisha yake kwa sasa yapo jijini Dar es Salaam akiuza kahawa.

Licha ya kutoka kwenye familia duni, kupendeza ni jambo alilolipa kipaumbele kwake akiamini muonekano hauna uhusiano wowote na hali ya kiuchumi ya mtu.

Kwa takribani miaka 10 sasa amekuwa akitegemea kipato kinachotokana na biashara ya kuuza kahawa anayotembeza mitaani kikombe kimoja kikigharimu Sh100.

Ukipiga hesabu za haraka unaweza kuona kama anapoteza muda, lakini kwa kauli yake anasema anapata pesa za kumuwezesha kujitimizia mambo mbalimbali katika maisha.

Muonekano wa Dickson umekuwa kivutio kikubwa kwa wateja na hilo ndilo linamtofautisha na wauza kahawa wengine.

Kila siku ana uhakika wa kujikusanyia kati ya Sh25,000 hadi Sh20,000 kutokana na mauzo ya kahawa.

Ukikutana naye kwa mara ya kwanza unaweza usiamini kama anauza kahawa aliyobeba kutokana na umaridadi wake.

Siku zote Dickson huanza shughuli ya kuuza kahawa akiwa amevalia suti, vazi linalotumika sana na wanaofanya kazi katika ofisi binafsi au za umma.

Vazi hili ambalo ni nadra kuonekana kwa mtu anayefanya biashara ya kutembea, linamfanya awe kivutio kwa watu anaokutana nao akiwa kwenye harakati zake za kujitafutia riziki.

Hata hivyo, Dickson akizungumza na Mwananchi anasema mara kadhaa amekuwa akikutana na maswali kama kweli anafanya biashara hiyo kujitafutia kipato au yupo kwa ajili ya kazi maalumu.

Anasema umaridadi ni kitu anachokipenda tangu akiwa kijiji kwao na alipofika mjini akaona atumie muonekano kujitofautisha na wengine wanaofanya biashara kama yake.

“Tangu nikiwa mdogo napenda kupendeza, wakati nakua kule kijijini kwetu nilikuwa naona wanaovaa suti wanaheshimiwa, nikawa natamani siku nikiwa na uwezo wa kumudu vazi hilo ndilo nitakalolitumia kwenye shughuli zangu bila kujua nitafanya shughuli gani,” anasema Dickson.

“Nasema sikujua nitafanya nini maana kiukweli sina elimu ya kunifanya niwe na uhakika kwamba nitaajiriwa, niliishia darasa la saba na hata huo mtihani sikufanya.”

“Nikiwa darasa la saba nilisoma wiki chache za mwanzo utoto ukanizidi nikaacha shule na huo ndio ulikuwa mwisho wa kujihusisha na masuala ya elimu,” anasema Dickson.

Jinsi alivyoanza kuuza kahawa

Baada ya kuhangaika huku na kule mkoani Dodoma mwaka 2012 akaona aje kujaribu bahati yake jijini Dar es Salaam.

Anasema alipata mwaliko wa ndugu yake aliyekuwa ameshaanza maisha katika jiji hilo la kibiashara kazi yake ikiwa ni kuuza kahawa.

Dickson alipowasili Dar es Salaam nduguye akampatia vifaa ambavyo ni vya msingi wa biashara ya kahawa, hivyo naye akaingia rasmi kwenye biashara hiyo.

Anasema kwa pamoja wakawa wanazunguka mitaani na kwenye vijiwe kusaka wateja wa kinywaji hicho ambacho mara nyingi hutumiwa wakati wa jioni.

“Nilipofika mjini nilitaka kujiweka vizuri kama walivyo watu wa mjini, nilikuwa nahakikisha navaa nguo safi wakati wote nikiwa kwenye biashara. Kuna ambao nilikutana nao wanafanya biashara hiyo, sikupendezwa na muonekano wao sikutaka kuwa kama wao,” anasema Dickson.

“Yaani unamuona mtu amevaa nguo chafu na wala hajali, sikuelewa inawezekanaje unafanya biashara ukiwa na muonekano wa hovyo, hili ndilo linasababisha wafanyabiashara ndogondogo tusiheshimiwe huko mitaani. Binafsi sikukubaliana na hilo nikadhamiria kuwa tofauti.”

Akiwa bado anajitafuta riziki kupitia kahawa, Dickson akaona aanze kujitofautisha na wenzake kwa kujipa muonekano wa tofauti ndipo alipodunduliza fedha zake za biashara na kupata Sh80,000 kisha akanunua suti.


Jamii inavyompa tafsiri tofauti

Huo ndio ukawa mwanzo wa Dickson kujitofautisha na wauza kahawa wengine wanaotembeza bidhaa hiyo mitaani huku akijijengea umaarufu uliomfanya kupewa majina ofisa, mtumishi na mengine mengi yaliyohusishwa na muonekano wake.

“Kuna wakati nakutana na watu ambao wanakataa kwamba mimi sio muuza kahawa, eti nafanya biashara hii kama sehemu ya kuzugia lakini nina kazi maalumu ambayo nimetumwa kwenye mtaa husika,” anasema Dickson.

“Kwa kiasi fulani kauli za aina hii huwa zinanipa mawazo kwa nini nihisiwe hivyo, kwa sababu ya muonekano wangu.

“Hata hivyo, wanashangaa siku zinazidi kusonga, miaka inakatika mimi bado nauza kahawa nikiwa na mavazi yangu yale yale na hata baadhi ya waliokuwa wananishuku sasa wamekuwa rafiki zangu,” anasema Dickson.

Kwa kuwa huo ndio utambulisho wake kwenye biashara, anasema hutunza fedha angalau kila mwaka ili aweze kupata suti, lakini kutokana na udogo wa kipato chake na mtindo wake wa kuvaa kila siku suti zake nyingi huchakaa mapema.

Kama ambavyo wengine hujiandaa kwa ajili ya biashara zao, maandalizi ya Dickson kila uchwao yanahusisha kupiga pasi suti ili akiingia mtaani aonekane maridadi tayari kuzunguka kwa wateja wake.

“Sasa hivi kuna nyumba ambayo naishi kama mlinzi, kabla ya hapo nilikuwa naishi kwenye nyumba ya kupanga ambayo haikuwa na umeme, hivyo nilikuwa nalazimika kwenda kwa fundi cherehani wa jirani kwa ajili ya kunyoosha,” anasema.

Neno kutoka kwa Dickson kwenda kwa vijana wengine ni kwamba umaridadi huficha umasikini na unaweza kujipa mwonekano unaotaka bila kujali kazi unayofanya, muhimu ni kupenda kile unachofanya.

“Usiruhusu kazi au shughuli unayofanya ikawa kikwazo katika muonekano unaotaka uwe, wote tunakubaliana na ukweli kwamba, sasa hivi zile kazi za kuajiriwa kuzunguka kwenye kiti ukiwa umenyonga tai ziko chache mno na wanaopata pia ni wachache.

“Kama hivyo ndivyo basi kimbilio kubwa la vijana ni kwenye kujiajiri au biashara ndogondogo, sasa tusiache kujipenda.”

“Naamini hata shughuli za kujiajiri zinahitaji uwe msafi, ujipende kwa kifupi upendeze na hii inaweza kuwavutia zaidi watu kufuata huduma yako kuliko kwenda sehemu nyingine,” anasema Dickson.

Licha ya kufanya biashara hii kwa muda mrefu, anasema bado hajafikia mafanikio ambayo amekuwa akiyatamani ikiwamo ndoto yake ya kufungua kijiwe cha kahawa cha kisasa kitamuingizia kipato na kutoa ajira kwa wengine.

Kwa sasa Dickson hajaoa wala hana mtoto hivyo jukumu kubwa alilonalo ni kuwasaidia wazazi na wadogo zake jambo analoamini atalifanya kwa ukubwa zaidi akifanikiwa kuwa kijiwe cha kisasa cha kuuzia kahawa.