Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unavyomlea ndivyo anavyokua, shtuka!

Picha na Mtandao

Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ni usemi wa wahenga wenye tafakari lukuki.

Na ukiutafakari kwa kina, hasa pale unapofikiria malezi ya mtoto tangu alipozaliwa hadi kufikia hatua ya kujitegemea, ni wazi utabaini jambo jema ama baya kwa mwanao.

Nasema hivyo kwa sababu, tukiangalia tabia nzuri au mbaya ya mzazi aliyonayo, mara nyingi hurithiwa pia na mtoto anayemzaa.

Mara zote wataalamu hutuambia tabia ya mzazi mara nyingi hurithiwa na mtoto katika makuzi yake.

Mzazi mwenye tabia njema na anayependa kuchangamana na jamii katika shida na raha, ndiyo hurithiwa pia na kizazi chake katika makuzi yao kwa sababu nao hufuata nyayo zake.

Kwa mfano, mtoto anayetoka katika familia ya mzazi kwa mfano mwandishi wa habari, polisi au daktari, tunaambiwa huwa kuna uwezekano mkubwa naye akarithi fani hizo.

Halikadhalika mzazi akiwa na tabia mbaya, kuna uwezekano mkubwa watoto wake nao wakarithi tabia hiyo isiyofaa machoni kwa walimwengu.

Wataalamu wanasema ukitaka kujua tabia ya mtu, basi chunguza tabia za watoto wake. Ukikuta watoto wanatumia lugha chafu, wanasema uongo, wadokozi au wanaharibu mali za watu, jua kwa kiasi kikubwa tabia hizo zimesababishwa na mazingira ya malezi waliyokulia nyumbani.
Tabia mbaya ya mzazi huathiri kwa kiwango kikubwa tabia ya mtoto wake.

Tafiti zinaonyesha mtoto anayetoka katika familia yenye mzazi anayevuta sigara au kunywa pombe, naye ana uwezekano wa kuvuta sigara mara nne zaidi ya yule ambaye mzazi wake hanywi wala havuti sigara.

Hii ni kwa kuwa watoto wanajifunza zaidi kwa kuona, lakini pia mazingira yanayowazunguka huwaathiri kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande mwingine, shule, marafiki, majirani na vyombo vya habari, kwa kiasi fulani navyo vinaathiri tabia za watoto, lakini bado haifuti ukweli kuwa wazazi wana mchango mkubwa katika kuathiri tabia za mtoto kuliko kitu kingine chochote.

Mzazi ndiye anayechagua shule ya kusoma mtoto wake, mzazi anaweza kuamua rafiki gani aambatane na mwanaye na yupi asiambatane naye.
Mzazi huamua mtoto aende kwa jirani yupi na asiende kwa nani. Kama haitoshi, mzazi huyohuyo anaweza kudhibiti matumizi ya vifaa kama vile redio, simu, runinga na kompyuta kwa watoto wake.

Lakini pia hata akishapevuka na kufikia hatua ya kutaka kujitegemea, basi mzazi huyohuyo anadhani kuwa bado analo jukumu la kumchagulia mke au mume mtoto wake.

Hata hivyo, tukirudi katika hatua ya malezi mtoto aanzapo shule na kuendelea, wazazi wengi hudhani jukumu lao ni kulipa ada, kununua vitabu, kalamu na sare za shule tu na akishamaliza hapo, anadhani jukumu lake ndiyo limemalizika kwa upande wa shule, jambo ambalo si sahihi.

Kwa hakika mambo haya ni muhimu, lakini ni sehemu ndogo tu ya majukumu yao.

Ila tukitazama kwa kina, mzazi ana mchango mkubwa zaidi ya hapo katika mafanikio ya mwanawe kielimu.

Nasema hivyo kwa sababu anapaswa kwenda mbali zaidi ya hapo. Mzazi anapaswa kufuatilia mahudhurio ya shule ya mtoto wake na kujua kama anafundishwa na kuelewa awapo darasani.

Na kama mwanaye bado haelewi, ni kitu gani akifanye ili kumsaidia zaidi katika safari yake ya masomo.

Kama hiyo haitoshi, mzazi anapaswa kujua kama mwanaye anaonyesha tabia njema kwa walimu wake na wanafunzi wenzake.

Kama atafanya hivi, mtoto huyo atapata msukumo na kujibidiisha pale alipolegalega. Na kwa kuwajibika huko, kutawapa pia nguvu na kuwatia moyo walimu wanaomfundisha mtoto huyo ambao nao wataweza kutilia mkazo na kuboresha maendeleo yake kitaaluma na kimaadili.

Wapo wazazi wengine ambao hawafuatilii maendeleo ya kielimu ya watoto wao kwa kutoa kisingizio cha kutojua kusoma na kuandika. Hoja hii haina mashiko hata kidogo.

Tafuta njia mwafaka kuhakikisha unajua maendeleo ya mwanao shuleni. Bahati nzuri karibu kila kona ya nchi hii wametapakaa wasomi wanaoweza kukusaidia kutathmini maendeleo ya mwanao.

Kadhalika, walimu wa mwanao ni wataalamu wazuri wanaoweza kukupa picha nzima ya maendeleo yake.

Mzazi anapaswa kuweka utaratibu wa kuzungumza mara kwa mara na walimu wanaomfundisha mtoto wake kwa lengo la kufahamu maendeleo yake shuleni.

Ili mtoto huyo aweze kukua na kuenenda katika malezi mema anayoyahitaji mzazi, basi anapaswa pia kumdhibiti asichangamane na makundi hatarishi.

Mfano makundi ya marafiki wasiopenda shule, wenye lugha chafu na wasiopenda kuheshimu wakubwa.

Dunia ya leo si ya zamani ambayo mtoto alikuwa mali ya jamii. Alipofanya kosa alikemewa na kila mtu hata kama si mzazi wake.

Siku hizi watu hawajali na utu umewatoka, hawajali kitakachomkuta mtoto wa mwingine. Kwa sababu hiyo, ni vema kila mzazi akatathmini ni watoto ama marafiki wapi wanaoambatana na mwanawe kwa lengo la kumuepusha na ushawishi.

Kuhusu maendeleo ya teknolojia ya habari, nathubutu kusema hapa kuna msiba mkubwa kwa kizazi cha sasa.

Kwa sababu wazazi wengi hawajui na wala hawatathmini kipi mtoto wake anapaswa kukifuatilia kama sehemu ya kujifunza na kipi akiache kinachokwenda kumpotosha kwenye runinga na kwenye simu za kiganjani.

Hii ni tabia ya hatari na inaathiri tabia za watoto wengi. Utakuta baba au mama na watoto wamekaa sebuleni wanatazama muziki au filamu iliyojaa picha za kutatanisha na pengine kuaibisha. Wengi wetu tumechotwa na fikra za usasa.

Kwa hiyo mtoto wa kike, wa kiume, baba na mama wote wanatazama filamu au muziki wa kisasa uliojaa picha za nusu uchi na matendo mengine yasiyoandikika.

Tabia hizi husababisha watoto kujua mambo ya faragha wakiwa katika umri mdogo. Usishangae yale utakayomuacha atazame katika runinga ukamkuta anafanya au anafanyiwa katika umri mdogo.

Hivyo ni wakati sasa wa kila mzazi, mlezi kutafakari kwa kina juu ya malezi bora kwa watoto kwa kuenenda katika njia zisizopotosha.