Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umuhimu wa wanandoa kutunza siri

Muktasari:

  • Ukiwa kwenye ndoa, acha kuongea kabisa ili usijikute ukivujisha siri ukidhani siyo siri wakati ni siri.

Kuna busara wakati wa kuwafunda wanawali katika jamii moja nchini Uganda isemayo kuwa wanapoolewa lazima wajifunze kufunga miguu na kufungua macho badala ya kufungua miguu na kufunga macho.

Hii hufanyika wakati mwali akijiandaa kwenda kwa mumewe. Wazazi hufanya hivyo kwa kujua kuwa nyumbani kwa mwali huacha kuwa kwao na huko aendako ndiko hugeuka kwake. Hamjasikia kwa Waswahili wakimwimbia bi harusi kuwa ‘sasa wenda kwako, utarudi huku kutembea?

Busara hii, licha ya kuzuia vishawishi vya  uasherati, inalenga kuwaambia wanandoa kuwa makini na waliowazunguka kuhusiana na maisha na ndoa zao. Inawahimiza kuchambua mambo na kujua ya kusema na ya kutosema. Siyo kila jambo lazima lisemwe au kuwekwa wazi kwa wasiohusika.

Tumeshagusia kwenye kitabu cha kwanza namna mashoga wanavyoweza kuvunja ndoa.

Pia, tuligusia juu ya imani au ushauri visivyofanyiwa utafiti vinaweza kuvunja ndoa. Ndoa nyingi zimevunjika na nyingine zitavunjika kwa sababu hizo. Hivyo, kama njia ya kuwafunda vijana, tumeamua kuchagua kisa hiki kufikisha ujumbe na ujuzi kadhalika.

Kuna kisa cha mama tulichosoma kwenye gazeti moja la nchini Zimbabwe. Kisa hiki ni juu ya mwanandoa mwenye majivuno na asiyetunza siri za ndoa yake.

 Akiwa amekwenda kusuka nywele kwenye saluni, alizoea kumlaumu mumewe kwa wenzake kuwa alikuwa akimwachia pesa kidogo.

Maskini hakujua kuwa alichoona kidogo, kilikuwa kikubwa kwa wenzake. Hivyo, baada ya kuwa akijisifu kwa kumsimanga mumewe kwa ‘kutomwachia’ pesa nyingi, walitokea waliotamani wangeolewa naye wakaanza kumuandama hadi ndoa ikavunjika na  mhusika akashangaa kujikuta aliyechukua nafasi yake alikuwa ni  mmojawapo wa mashoga yake aliyezoea kumlalamikia juu ya tabia za mumewe.

Kimsingi, huyu mama hakufunga miguu na kufungua macho. Alipaswa afunge mdomo na kufungua masikio. Je, ni wangapi wameishashuhudia au kukutwa na haya?

 Je, hapa utamlaumu nani kama siyo wewe mwenyewe? Huwa tunawashauri na kuwahimiza wanandoa kutofanya maisha yao au ndoa zao magazeti au matangazo.

 Je, ni wangapi hufunga miguu na kufungua macho au kufanya kinyume? Je, hili halina faida kubwa kwao kama watalishika, kulikumbuka na kulitekeleza?

  Unaweza kujisikia raha kuwasimulia wenzako juu ya maisha yako bila kujua madhara yake.

Hata hivyo, si wasikilizaji wako wote hujisikia kama unavyojisikia. Hivyo, si vibaya kushauri na kusisitiza kwa wanandoa kuchambua na kujua ya kusema na kutosema.

 Tunajua kuwa si wote wanapata bahati au kuwa na desturi, mila, na tamaduni za kufanya hivi hasa wakati huu wa utandawazi ambapo vijana wanaweza kukulia mbali na jamii zao hadi kuoa au kuolewa.

Hivyo, kwa kuliibua na kulikumbushia hili, tunalenga kuwasaidia wasio na fursa au walio nayo lakini wasizingatie.   

  Wewe na mwenza wako ni sawa na kata na mtungi. Siri ya mtungi apaswaye kuijua ni kata tu.

Hivyo, unapofungua mdomo ukaziba masikio, utaumia utake usitake. Kama hujaumia, ni suala la muda

Pia, ni vizuri kubainisha kuwa unapaswa kujua mambo ambayo ni siri na yasiyo siri. Kama hujui, acha kuongea kabisa ili usijikute ukivujisha siri ukidhani siyo siri wakati ni siri.

Hivi usiposimulia juu ya maisha yako utakosa nini ikilinganishwa na kuyasimulia ukaishia kujuta?

Hata habari huwa hatuzipati bure. Ama utanunua chombo cha habari kama gazeti, runinga, au redio ndio uzipate au ulipie kwa wanaozitoa.

Mbali na majanga na misiba, hakuna habari za bure duniani hasa wakati huu ambapo kila kitu ni bidhaa inayoweza kutumiwa na baadhi ya watu kutengeneza faida hata kama ni kwa hasara ya kuwaumiza wengine.

Turejee tulikoanzia. Mbali na kushauriwa ufunge miguu na kufungua masikio, tuseme wazi. Je, unakosa nini usipofichua siri zako?

 Je, unapata nini unapozisambaza? Kwani, lazima kila unachofanya wakijue watu wakati hujui wafanyayo? Hata ukiyajua wafanyayo, kwani lazima uyafahamu kwa kuhatarisha maisha, ndoa, na siri zako? Hivyo, usikubali kuwa habari kwani si kila habari ni nzuri. Waandishi wa habari husema heri upate habari kuliko wewe kugeuka habari.