Mtindo wa kitenge unavyozidi kuchanja mbuga kimataifa.?

Muktasari:
“Nilipofika hapa mwaka mmoja uliopita nilivutiwa sana na nmna wanawake wa Kitanzania walivyohadari katika kuchanga rangi, wanavaa nguo zenye rangi ya kung’aa na bado wanapendeza.”
Mavazi ya kitenge yamezidi kujiongezea umaarufu nchini. Wabunifu wa mavazi wamekuwa wakijitahidi kila kukicha kulipendezesha vazi hili na kuonekana katika mitindo tofauti tofauti.
Katika zama hizi kitenge kimekuwa kikitengenezewa kwa ubunifu wa aina mbalimbali ikiwamo gauni, koti, suruali kwa wanawake na wanaume, mikoba, viatu, suti nk.
Miaka ya nyuma kidogo ilikuwa ni nadra sana kumuona msichana mrembo kutinga nguo iliyotengenezwa kwa kitenge na kwenda nayo ofisini au katika hafla mbalimbali za jioni.
Miaka hiyo kitenge kilivaliwa zaidi na wanawake wa makamo na ilikuwa katika shughuli na sehemu maalumu kama kanisani au msibani, vijana walilipa kisogo vazi hilo kwani lilionekana lisilokwenda na wakati.
Mambo yamebadilika na kitenge sasa ndio habari ya mjini, wabunifu nguo nao wamekuwa wakiongezea vazi hilo naksi kwa kulipamba kwa namna tofauti na kulifanya lionekana kuwa na hadhi ya kipekee.
Pia katika kuongeza soko la vazi hilo kimataifa, wanawake 22 wajasiriamali kutoka mkoani Ruvuma wamepata fursa ya kuonyesha bidhaa zinazotokana na vitenge na shanga katika maonyesho ya mitindo ya kimataifa yatakayofanyika katika Jiji la Milan nchini Italia hapo mwakani.
Maonyesho hayo yanajulikana kama Milan Expo 2015 yatashirikisha mataifa zaidi ya 150 na kushuhudiwa na wageni wanaofikia 25 milioni.
Fursa hiyo imetokana na ushirikiano baina ya wanawawake hao na ubalozi wa Italia nchini na shule ya mitindo kutoka nchini humo, ambapo wametengeneza mitindo ya mavazi inayojulikana kama Mikomanile Moda Millano.
Balozi wa Italia nchini anasema anachovutiwa zaidi kuhusu mavazi na fasheni kwa wanawake Watanzania ni namna wanavyochanganya rangi.
“Nilipofika hapa mwaka mmoja uliopita nilivutiwa sana na nmna wanawake wa Kitanzania walivyohadari katika kuchanga rangi, wanavaa nguo zenye rangi ya kung’aa na bado wanapendeza.”
Mwanamitindo maarufu nchini Ally Remtura anasema maonyesho hayo yatakuwa fursa nzuri ya kutangaza wanamitindo wa ndani kimataifa.
Anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo wabunifu mavazi ni uhaba na ufinyu wa soko la nguo zao na namna ya kujitangaza na kujilikana.
“Hii itakuwa njia nzuri sana, kwani nguo hizo zitakuwa zimetengenezwa hapa hapa nchini na kutangazwa kimataifa, ni nadra sana kwa fursa kama hii kutokea.”
Akizungumzia onyesho hilo, Mkurugenzi wa Kikundi cha Mkomile, Janneth Lupenza alisema ushirikiano huo utawawezesha kujulikana kimataifa na hivyo kuongeza soko la bidhaa zoa.
Anasema hapo awali, walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kuzalisha bidhaa katika kiwango duni, lakini kutokana na mafunzo ya kuongeza ujuzi waliyoyapa, wamefanikiwa kutengeneza nguo katika ubora zaidi.
“Tunatarajia matokeao chanya baada ya maonyesho hayo, nina hakika kazi za wabunifu wa Tazania zitaongezeka thamani.”
Janneth anaiomba serikali kuunga mkono juhudi zinazofanywa na watu binafsi hasa katika kuwasaidia kujitangaza kwani hiyo ndiyo changamoto kubwa wanayokumbana nayo.