Mazungumzo ya afya yanavyoimarisha familia
Muktasari:
- Wataalamu wa afya na malezi ya watoto wanaeleza kuwa mazungumzo ya kiafya kati ya wazazi na watoto, ni msingi muhimu wa kujenga familia yenye afya na ustawi wa muda mrefu.
Dar es Salaam. Tujiulize kwanza, je, tuna utamaduni wa kuzungumzia afya katika familia zetu? Hili ni swali zuri sana katika jamii ya sasa ya kiutandawazi, maana katika familia nyingi za Kitanzania, wazazi hutumia muda mwingi n tu kuhakikisha watoto wao wanapata chakula, mavazi, elimu na mahitaji mengine muhimu.
Hata hivyo, jambo moja ambalo wakati mwingine husahaulika, ni mazungumzo ya mara kwa mara kuhusu afya.
Wataalamu wa afya na malezi ya watoto wanaeleza kuwa mazungumzo ya kiafya kati ya wazazi na watoto, ni msingi muhimu wa kujenga familia yenye afya na ustawi wa muda mrefu.
Mazungumzo ya kiafya yanahusisha mada mbalimbali, kuanzia usafi wa mwili, lishe bora, mazoezi ya mwili, afya ya akili, hadi mabadiliko ya mwili yanayotokea wakati wa kubalehe. Kupitia mazungumzo hayo, watoto hupata maarifa sahihi yanayowasaidia kufanya uamuzi bora kuhusu afya zao.
Siku zote wazazi ndio walimu wa kwanza wa watoto wao katika masuala ya afya. Mtoto anayejengewa mazingira ya kuzungumza kwa uwazi na wazazi wake, huwa na uwezekano mkubwa wa kukuza tabia nzuri za kiafya na kujiepusha na hatari mbalimbali zinazoweza kuathiri maisha yake.
Mwanasaikolojia Pendo Joseph alishawahi kusema kwenye warsha ya afya ya mama na mtoto iliyofanyika katika Hospitali ya Rugambwa: "Wakati mtoto anapopata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu mwili wake, magonjwa au mabadiliko anayoyapitia bila kuogopa kukemewa, anajenga uelewa mzuri wa namna ya kujitunza. Hilo linaweza kumsaidia hata anapokuwa mtu mzima."
Katika dunia ya sasa yenye maendeleo makubwa ya teknolojia, watoto wengi hupata taarifa kupitia simu za mkononi, mitandao ya kijamii na marafiki. Ingawa baadhi ya taarifa hizo ni sahihi, nyingine zinaweza kuwa za kupotosha na kuhatarisha afya zao. Ndiyo maana wataalamu wanasisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwa chanzo cha kwanza cha taarifa sahihi za kiafya kwa watoto wao.
Mazungumzo ya kiafya pia huimarisha uhusiano wa karibu kati ya mzazi na mtoto. Mtoto anayejisikia kusikilizwa na kueleweka huwa na ujasiri wa kushiriki changamoto anazokutana nazo maishani. Hii inaweza kusaidia kugundua matatizo ya kiafya au kihisia mapema kabla hayajawa makubwa.
Kwa mfano, mtoto anayepitia msongo wa mawazo, unyanyasaji au matatizo ya kisaikolojia, anaweza kuwa tayari zaidi kueleza hali yake kwa mzazi ambaye amejenga utamaduni wa mazungumzo ya wazi.
Vilevile, mazungumzo kuhusu afya ya uzazi yanaweza kuwasaidia vijana kuelewa mabadiliko ya miili yao na kujikinga dhidi ya tabia hatarishi.
Mzazi hana budi kumweleza mtoto wake kwa kina kuhusu habari za uzazi na mambo mengine yanayoendelea katika ulimwengu huu yanayotendeka kinyume. Zungumza na mwanao kinagaubaga bila kificho, usiogope wala kumwonea haya utamsaidia kukua vizuri na kuishi katika afya njema.
Usisubiri awe mkubwa
Wataalamu wanaeleza kuwa mazungumzo kuhusu afya hayapaswi kusubiri hadi mtoto awe mkubwa. Kuanzia umri mdogo, wazazi wanaweza kuzungumzia umuhimu wa kunawa mikono, kupiga mswaki, kula vyakula vyenye virutubisho na kufanya mazoezi. Kadiri mtoto anavyokua, mada zinaweza kupanuka na kujumuisha afya ya akili, kubalehe na masuala mengine yanayolingana na umri wake.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayotajwa na wataalamu ni kwamba baadhi ya wazazi huona aibu kuzungumzia mada fulani na watoto wao. Wengine huamini kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwachochea watoto kujaribu mambo mapema.
Lakini ukweli ni kwamba watoto wanapokosa taarifa sahihi kutoka kwa wazazi wao, huenda wakazitafuta mahali pengine na kupata taarifa zisizo sahihi.
Juliana Julius, anasema mara nyingi kwa jamii zetu za Kiafrika utamaduni wa kukaa tu na familia kuzungumzia mada fulani ya afya haupo bali majadiliano hutokea pale mada fulani inapoibuka au kusikika kwenye radio au runinga ndipo tunazungumza.
“Mfano unaposikia mtu anaumwa ugonjwa wa zinaa, unaweza kukaa mkajikuta mnajadili tu kuhusu huo ugonjwa na namna ya kuuepuka, au hata magonjwa mengine mtakaposikia ndipo mnajadili na kujua,” anasema Juliana.
Wazazi wanashauriwa kutumia lugha rahisi, inayoeleweka na inayoendana na umri wa mtoto. Pia wanapaswa kusikiliza kwa makini maswali ya watoto na kujibu kwa uaminifu badala ya kuwakemea au kuwapuuza.
"Mazungumzo ya kiafya si tukio la siku moja. Ni mchakato unaohitaji kuendelea kila siku kupitia matukio ya kawaida ya maisha ya familia. Wakati wa kula, kutembea pamoja au hata wakati wa kutazama televisheni, mzazi anaweza kupata nafasi ya kuzungumza na mtoto kuhusu afya," anasema Dk Gloriamaria Kunambi.