KUTOKA LONDON : Kiswahili kinavyozidi kuparaganya herufi ‘r’ na ‘l’
Muktasari:
- Nchi kumi na moja! Ongezea idhaa kadhaa za redio, televisheni na mitandao jamii ughaibuni inayokitukuza Kiswahili. Jazia, vyuo.
Watanzania tuamke jamani. Tumelala.
....Kiswahili kilianzia kwetu. Nchi 11 zinazungumza lugha hii iliyotuunganisha na kutuletea amani zaidi ya miaka 100!
Nchi kumi na moja! Ongezea idhaa kadhaa za redio, televisheni na mitandao jamii ughaibuni inayokitukuza Kiswahili. Jazia, vyuo.
Hapa London kiko chuo maarufu cha lugha- SOAS ( School of Oriental and African Studies- Shule ya Masomo ya Mashariki na Afrika). Mtaa wa Russel Square, katikati ya jiji. Si vichochoroni kwa walalahoi. Hapa Russel Square alipigwa kisu mhadhiri wa Kimarekani miezi michache iliyopita na gaidi aliyechanganyikiwa akili. Julai 7, 2005 basi lililipuliwa na magaidi wanne waliofariki kishabiki na kishabiki.
SOAS iko Uzunguni.
Ukiingia chuoni utashangaa namna vijana – kutoka mataifa mbalimbali wanavyozungumza Kiswahili, tena kwa hamasa. Mwaka 2010 niliitwa kutumbuiza ngoma kusheherekea kuanzishwa klabu ya wazungumzaji Kiswahili, SOAS.
Mmoja alinieleza alivyoporwa na teksi ya kihuni akitalii Tanzania. Lakini hakulichukua tendo la kuibiwa na vibaka kujenga chuki kwa Watanzania. Kila mahali huwepo wazuri na wabaya alisema. ”Kila kapu huwa na matufaha yaliyooza na mazuri” – ni msemo wa Kiingereza usiopenda kuweka watu wote katika kundi moja. Wenzetu wanakipenda Kiswahili.
Siku hiyo hiyo ya 2010, alikuwepo pia mzee wetu, mtaalamu msifika wa Kiswahili, Dk Farouk Topan. Namheshimu. Wakati nikisoma bado Mzumbe kilikuwa kipindi cha malumbano makali kati ya washairi wa vina na mizani na washairi wa mashairi huria yasiyofuata kanuni za urari au mfanano huo. Profesa Euphrase Kezilahabi (mwandishi mashuhuri wa riwaya za Kiswahili) alitoka na mkusanyiko wa mashairi guni ulioitwa Kichomi. Utangulizi wake uliandikwa na Dk. Farouk Topan. Dk Topan kaandika vitabu vingi vya taaluma ya Kiswahili na tamthiliya.
Alifundisha muda mrefu SOAS. Kastaafu. Bado wapo wahadhiri wengi wa Kiswahili toka Kenya na Tanzania.
Mwezi jana nilikutana naye Dk Topan ndani ya tafrija kusheherekea miaka 400 ya maisha ya mwandishi nguli wa Uingereza William Shakespeare. Dk Topan alialikwa rasmi kuhutubia jumba maalumu la Waismailia hapa London. Akaelezea uhusiano wa Kiswahili na fasihi zake Shakespeare. Walijazana wengi pale hasa Wahindi waliozaliwa Afrika Mashariki. Wanakihusudu Kiswahili ingawa walihamia nje zamani.
Dk Topan alitaja baadhi ya waandishi wetu waliotafsiri kazi zake Shakespeare kuja Kiswahili. Kama Mwalimu Nyerere aliyetafsiri Mabepari wa Venice (Merchants of Venice) na Julius Kaizari, kisa cha mfalme wa Kirumi aliyeuawa na mawaziri wake.
Mitaani je?
Mwezi jana lilikuwapo tamasha la siku kadhaa kusheherekea masuala ya watu weusi jumba maarufu la starehe Royal Festival Hall. Nikaajiriwa kuendesha darasa la Kiswahili kupitia muziki. Aliyenialika ni dada wa Ki-Eritrea anayekifagilia KIswahili. Nikatumia wimbo mashuhuri wa “Malaika” na “Sura Yako” wa Sauti Sol- wanamuziki toka Kenya. Kwa nini nyimbo hizi zilitumiwa? Kwa sababu maneno yake yameandikwa mtandaoni na You Tube. Nani watunzi? Wa Kenya. Zingatia wa Kenya walivyo mstari wa mbele katika utunzi wa nyimbo za Kiswahili. Mwingine unaosifika ni Jambo Jambo (Hakuna Matata) wa Bendi ya Uyoga au Mushrooms.
Mwezi huo huo wa Septemba nilialikwa kujiunga na kundi la mtandao jamii wa “WhatsUp” - Kiswahili Club. Hawa wala si wazee walioishi Tanganyika enzi za Ukoloni na Ujamaa. La hasha.. Wengi ni vijana waliozaliwa baada ya 1980. Wanakienzi Kiswahili. Hunitaka niwasahihishe kila wanapoandika au kuzungumza....
Hii ni mifano michache tu ya jinsi lugha hii inavyozidi kusambaza matawi na mabawa duniani.
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa ulitangaza lugha 10 zinazokua kasi duniani na kudai Kiswahili ni ya saba!
Itaendelea
Nyingine ni Kispanyola, Kichina, Kiarabu, nk.
Maana yake nini?
Mosi , biashara.
Mnaolilia ajira.
Zingatieni.
Mangapi unayoweza kuyafanya kuuza Kiswahili?
Kwanza je unakimanya vizuri ? Kama bado jifunze sarufi sawasawa. Pili, zingatia matumizi sahihi ya maneno na lahaja. Viko Viswahili vya aina saba. Fasaha, Kingwana (Cha Kongo), Kingazija, Cha ukanda wa Ziwa Victoria (Burundi na Rwanda), Kimvita, Kishenge (au Kiswanglish cha Kenya), na Kimrima (cha Dar es Salaam na mwambao). Je unavifahamu?
Zingatia maendeleo mengine muhimu. Wataalamu wawili wa Kiswahili, Profesa Saidi Ahmed Mohammed (mtunzi wa kitabu maarufu Asali Chungu, 1976)na Prof Mohammed A. Mohammed, walichapisha Kamusi ya Visawe, mwaka 2002. Imechapwa tena. Kisawe ni neno linalofanana na jingine. Kiingereza ni “Synonym.”
Kamusi ya visawe hukusaidia unapotaka kusema neno lile lile bila kulirudia . Kwa mfano, mathalan, bimithili, tuseme, nk. Banja, pasua, vunja, bangua, nk. Ruhusa, idhini, ridhaa, itikio, kubalia, achia, nk.
Kamusi hii haikuwepo katika Kiswahili.
Kwa lugha nyingine kubwa, licha ya kamusi, ukiingia tu Google kutafuta visawe vyake utavipata. Kiswahili hakuna.
Mbali ya Kamusi ya Visawe , kamusi mpya za TUKI za Kiingereza na Kiswahili zimetolewa upya karibuni na kurasa nyingi na maneno zaidi. Ya Kiingereza kuja Kiswahili mathalan, imeongezeka kurasa 900 hadi 1000. Maana yake nini? Msamiati wa Kiswahili unaongezeka. Kazi nazo zazidi kuwa nzuri.
Maendeleo hayo, yanakuja.
Kinachoharibu si wataalamu wa lugha: magwiji wanaotunga riwaya, au kufundisha vyuo na kamusi. La hasha.
Tunaoharibu ni wanasiasa, wanahabari, waalimu mashuleni na watunzi wa nyimbo wanaoendelea kutukuza Kiswanglish na kuparaganya herufi L na R, kama rafiki yangu Masudi Pashamoto Msele.
Tatizo hili lilikuwa dogo zamani kutokana na watu wa mikoani kutojua sawasawa lugha. Linazidi kukua. Watanzania wengi wanaoandika mitandaoni na mablogi hawatofautishi “ bahili” na “bahiri”, “ mhalifu” na “mharifu”, “mpira” na “mpila.” Zamani watoto wadogo walioota mapengo ndiyo walioharibu. Siku hizi tunashindwa kupambanua. Sikiliza wimbo mpya wa Diamond -Salome. Mara ngapi karudia neno “Sarome”?
Wasikilize watangazaji wa redio FM wanavyochanganya na kuboronga nahau kwa kusema “Nyimbo hii” badala ya “wimbo huu”- au “nyimbo hizi”-wanashindwa kutaksirisha wingi wa neno “wimbo” kuwa “nyimbo.”
Toba!
Sasa ikiwa wanahabari, wasanii, wanasiasa na waalimu mashuleni tunawafundisha watoto kusema “Luninga” kinyume cha “Runinga,” nani ataokoa jahazi la kesho? Nani atasahihisha wanaokua na kuiga kusema “Sarome” kwa kuwa mtu maarufu kaimba vile? Je wahusika tunasoma na kujifunza Kiswahili sawasawa? Au tunajimamasa na kubabaisha tu ?
-Bpepe: [email protected]
-Tovuti: www.freddymacha.com