Je, saratani ya matiti huwa ni ya kurithi
Muktasari:
- Ndiyo! kama ilivyo kwa aina nyingine za saratani, ya titi pia huwa ni ya kurithi kutokana na vinasaba vya ugonjwa wa aina hii ya saratani kurithishwa kwenye vizazi vya familia husika. Hata hivyo, wanawake
Daktari naomba kujua, saratani ya titi huwa ni ya kurithi?
Janeth, Moshi
Ndiyo! kama ilivyo kwa aina nyingine za saratani, ya titi pia huwa ni ya kurithi kutokana na vinasaba vya ugonjwa wa aina hii ya saratani kurithishwa kwenye vizazi vya familia husika. Hata hivyo, wanawake wengi wanaopata ugonjwa wa saratani ya matiti wanatokana na vihatarishi vingine tofauti na sababu za kurithi. Hivyo ukweli ni kwamba kwa kuwa mmoja wa wanafamilia aliwahi kuugua ugonjwa huu haimaanishi kuwa kila mmoja katika familia atapata ugonjwa huu. Nashauri wanawake waendelee kujiepusha na vihatarishi vya ugonjwa wa saratani ya titi kama vile ulevi, kuepukana na uzito wa mwili uliopitiliza na uvutaji wa sigara.
Naidhibiti vipi sukari inayopanda?
Mimi nina tatizo la sukari inayopanda. Nifanye nini ili niweze kuidhibiti?
Francis Francis
Pole sana Francis, tatizo lako limetokana na kiwango cha sukari kuzidi kwenye damu. Ili kudhibiti sukari isiendelee kupanda kwenye damu unashauriwa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara, kutumia dawa za kudhibiti kupanda kwa sukari kama ulivyoelekezwa na daktari, kula vyakula vinavyosaidia kupanda kwa sukari kwa wingi kama vile matunda yenye nyuzi lishe, vyakula vyenye carbohydrate kwa wingi . Unashauriwa pia kujenga ukaribu na wataalamu wa lishe kwa ajili ya ushauri wa nini unapaswa ule kila siku, kupima sukari yako mara kwa mara ili kuangalia mwenendo wa sukari yako.
Zipi dalili za ugonjwa wa figo na ini?
Ningependa kufahamu dalili za ugonjwa wa figo na ini.
Amani Justine
Dalili kuu zinazoashiria kuwa unashambuliwa na ugonjwa wa figo ni pamoja na uchovu uliokithiri, kuhisi baridi kwenye mazingira ambayo siyo ya baridi, kupata shida ya upumuaji, kukosa nguvu za mwili, muwasho wa mwili, kujaa maji kwenye baadhi ya sehemu za mwili na hasa miguuni na viganjani, kuvimba kwenye baadhi ya sehemu za mwili hasa usoni na tumbo. Dalili nyingine ni kuhisi ladha tofauti ya chakula, kuvurugika kwa tumbo, kichefuchefu na kutapika, mabadiliko yanayojitokeza kwenye mienendo ya mkojo kama vile kutoa kiasi kidogo cha mkojo na mkojo kubadilika rangi iliyochanganyika na damu.
Sababu za kiungulia ni zipi?
Mimi nina tatizo la kiungulia nikila kitu chochote lazima nisumbuliwe na kiungulia.
Elias Burwaye
Pole sana tatizo la kiungulia linasababishwa na baadhi ya matatizo ya kiafya yanayojitokeza kwenye mfumo wa chakula na hasa uwepo wa kiasi kikubwa cha gesi tumboni. Gesi ikijaa hutengeneza mkandamizo hadi kwenye njia ya chakula, kuna visababishi ambavyo ni pamoja na unywaji wa pombe, kahawa mara kwa mara na vinywaji vilivyochakatwa ambavyo vina gesi kwa wingi, matumizi ya dawa mara kwa mara na hasa ya antibiotiki. Pia, ulaji wa matunda yenye ladha chachu na yenye asidi kama vile maembe mabichi na machungwa. Kiungulia pia kinaweza kusababishwa na maradhi ya vidonda vya tumbo na hasa kiungulia kikiwa kinatokea mara kwa mara, hivyo nakushauri waone wataalamu wa afya kwa ajili ya vipimo vya kuangalia vidonda vya tumbo.
Sipati hedhi na sina mimba
Dokta nina mwezi wa pili sijaziona siku zangu nimepima mimba hakuna lakini tumbo lina maumivu na maziwa yanauma.
Aziza Msomali
Aziza tatizo la kukosa hedhi limekuwa likiwapata wanawake wengi. Sababu kuu na ya asili ya kukosa hedhi kuwa mjamzito, au kufikia umri ambao mwanamke hawezi tena kushika mimba na kuzaa. Tofauti na sababu hizi mbili, ni dhahiri kuwa kukosa hedhi ni tatizo la kiafya linalohitaji msaada wa kimatibabu. Baadhi ya sababu ni pamoja na matumizi ya aina mbalimbali za uzazi wa mpango, baadhi ya matumizi ya madawa ya magonjwa mengine kama vile ya sonona, saratani, na hata dawa za shinikizo la damu lakini pia matatizo yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni pia yanaweza kusababisha. Kukosa hedhi kwa zaidi ya miezi miwili linaweza kuashiria matatizo mengine ya kiafya kama vile uwepo wa uvimbe kwenye mfumo wa uzazi hasa kwenye ovari au hata kwenye mfuko wa uzazi. Nakushauri nenda hospitali waone wahudumu wa afya kwa vipimo.