Fahamu lugha za mapenzi kwenye uhusiano

Ni vyema kila aliyeko kwenye uhusiano, mapenzi au ndoa kufahamu ziko namna za kuwasiliana na kufahamiana baina ya wapenzi ambazo endapo mmoja anakosea kwa kujua au kutokujua anakuwa analeta misuguano yenye athari sana kwenye penzi husika.
Kila mmoja hana budi kuifahamu lugha mwenzake anayoitumia kuonyesha penzi au kumaanisha penzi ili basi uweze kuyafanya mambo kwa mrengo ule ule wa mpenzi wako na yeye vilevile akufahamu na kufanya mambo kupitia lugha yako.
Hapa kila mmoja anakuwa anaugusa moyo wa mwenzake na kuiongeza furaha katika uhusiano.
Maneno ya kupongeza
Unaweza ukawa unafanya mambo mengi mema kwa mpenzi wako lakini anaangalia na kunyamaza akifahamu ndani yake kwamba ni wajibu wako kufanya vile.
Wako watu wenye kiu sana na maneno ya kupongezwa ya kushukuriwa au kuhamasisha. Kwa mfano, mwenzako amekusaidia kuanua nguo zako nje, akimaliza au unapogundua nguo zimetolewa na lilikuwa jukumu lako kuzitoa, usione ugumu wa kumwambia mpenzi asante kwa kunisaidia kuanua nguo.
Anaweza akaamua kumlisha mtoto, wewe ukiwa unafanya mambo mengine, usichukulie kirahisi tu kwamba na yeye si mzazi lazima amlishe mtoto pia, hapana, mwambie mpenzi nakushukuru umenisaidia kumlisha mtoto na mimi nikaweza kufanya hiki na kile.
Akipendeza mwambie umependeza, nguo hiyo inakutoa vema sana, akifanya kitu hata kama ni kidogo mpongeze na kumwambia unatambua mchango wake mzuri. Wako wenye kiu kubwa na maneno haya na kwao wasipoyasikia ni kama vile hawajapendwa kabisa na unaposema neno hili kwake unanyanyua kitu kikubwa sana ndani yake.
Ni vyema ukafahamu kama mpenzi wako ni mwenye lugha ya mapenzi basi usimnyime chakula cha nafsi yake. Mpongeze, mshukuru na kumwambia maneno yenye hamasa yatakayomshibisha.
Matendo ya kuhudumia
Nadhani unakumbuka ule usemi unaosemwa mara nyingi kwamba, “matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno,” wengine wanasema maneno matupu hayavunji mfupa. Misemo hii yote inatuma ujumbe mmoja kwamba maneno matupu yakiongewa tu pasipo matendo basi hakuna tija.
Wapo ambao matendo ndio kitu pekee cha wao kuonyesha penzi na hata wao kulitafsiri penzi kutoka kwa mtu mwingine pia.
Hapa namaanisha, kwa yeye kukuonyesha anakupenda atakuwa tayari kukufanyia kitu au kukusaidia kitu na ili ajue unampenda na yeye anatamani kuona wewe ukimfanyia kitu au vitu, anataka kuona matendo, sio maneno tu.
Yamkini una juhudi sana za kumwambia mpenzi wako kuwa unampenda sana na unafurahi kuwa naye maishani, haya ni maneno mazuri na makubwa sana, lakini kama yeye ni mmoja ya watu wenye lugha ya matendo ya kuhudumia itakuwia ngumu kumuonyesha unampenda kwa sababu kwake yeye upendo au mapenzi hayaonyeshwi kwa maneno, bali kwa kumsaidia kitu au vitu.
Yeye anatarajia akiosha vyombo umsaidie kufuta, akiandaa chakula umsaidie kuandaa meza, akimalizia kuvaa umsaidie kumwandaa mtoto ili muwahi, na vitu vingine kama hivi.
Cha ajabu ni kwamba kwa mmoja kutokuona mapenzi yakionyeshwa kwa lugha yake basi anahitimisha hapendwi.
Sasa angalia jinsi watu wawili wanaoishi nyumba moja kama mtu na mkewe, kila mmoja akifahamu fika anampenda mwenzake lakini mmoja anaona kabisa kuwa hapendwi.
Lakini kama wakisaidiwa kuzifahamu lugha zao za penzi, basi kila mmoja atamfahamu mwenzake na kuongea kwa lugha yake.
Kutoa na kupokea zawadi (gifts)
Katika jamii mbalimbali kwa miaka mingi sana kutoa zawadi kwa mtu au watu kumekuwa kukitazamwa kama ishara ya kuonyesha upendo.
Na mtu mwenye tabia ya kutoa zawadi mara kwa mara basi anaonekana kwenye jamii husika kwamba ni mtu mwenye upendo sana.
Itaendelea