Prime
ANTI BETTY: Nimwambie shemeji watoto anaolea sio wake?

Anti habari. Naomba usiniwashie moto nisaidie nifanyeje kutoa au kuishi na siri hii maana naona imeanza kunishinda.
Nina rafiki yangu wa tangu shule ya awali, tulipoteana baadaye nikaja kukutana naye baada ya mume wangu na wake kuwa wanafanya kazi ofisi moja. Kwa kuwa tulikuwa marafiki kuanzia hapo tukawa karibu zaidi.
Sasa hivi ana watoto watatu, mdogo kamzaa miezi 10 iliyopita ila wote siyo wa huyu shemeji yangu aliyemuoa.
Ninajua na baba wa watoto hao ninamjua pia kwani tulisoma naye chuo, kinachoniuma ni namna anavyowahudumia kwa mapenzi na gharama bila kujua siyo watoto wake.
Kibaya zaidi ikitokea amesafiri baba wa hawa watoto huja kuwaona hapo hapo nyumbani.
Ninaumia sana, natamani nimueleze huyu shemeji yangu huu uchafu wa huyu shoga yangu.
Nipe mbinu nifanyeje?
Ninaelewa kuwa unafuatilia mambo ya watu, lakini ni vizuri kujua kuwa kuna mipaka ambayo tunapaswa kuzingatia kuhusu maisha ya wengine.
Kila mmoja wetu anapita katika changamoto zake binafsi na kuna mengi yasiyosemwa. Inawezekana rafiki yako na mumewe wanalijua unalolijua wewe ila wana makubaliano kutokana na changamoto hizi na zile.
Kumbuka na usisahau, nakusisitizia kufanya maamuzi katika maisha ya wengine, hususan ya mahusiano kama ya rafiki yako na mume yanaweza kuleta madhara makubwa sana.
Kila familia ina historia yake, na masuala kama haya mara nyingi yanahitaji uelewa na uvumilivu. Badala ya kujipa jukumu lisilokuhusu la kufikisha taarifa hizi mbaya kabisa kwenye familia ya mwenzako, mpe muda rafiki yako pengine anatafuta wakati muafaka wa kuliwasilisha hilo.
Kila mtu ana haki ya kuamua ni lini na jinsi gani anataka kushirikisha wengine taarifa kuhusu maisha yake.
Pia kuna sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ambapo zinaweza kukutia matatani ukiamua kuzungumza habari za watu wengine.
Kuzungumzia watu wengine bila idhini yao ni uvunjifu wa faragha. Hii inaweza kusababisha migawanyiko na maelewano mabaya baina ya marafiki.
Mtu anapokuwa na watoto na familia, ni muhimu kutambua kwamba maisha yao ni ya muhimu na yanahitaji kuheshimiwa. Tafadhali jaribu kuepuka kuingilia na badala yake, tumia wakati wako kuwasaidia watu zaidi kwa njia inayowajenga, bila ya kuwafanya wajisikie wakosefu kwa kukosa maadili kama huyo rafiki yako.
Sifurahii alichokifanya, lakini mimi na wewe hatujui kwa nini amefanya hivyo kwa sababu hujasema. Muhimu kama alikushirikisha kuhusu hao watoto mshauri asiendelee kuruhusu huyo baba wa hao watoto kuja hapo nyumbani kwani ipo siku ataleta taabu kubwa.
Mshauri katika njia rafiki ili asije kukuona unaingilia maisha yake.
Pia hebu tafuta shughuli ufanye kuliko kufuatilia maisha ya watu, unajua katika hilo sakata unalotaka kulianzisha watakaoathirika ni hao watoto na siyo huyo mama.
Wao wanajua huyo ni baba yao na anawalea na kuwatunza kwa mapenzi kama ulivyosema, huoni kama ukiweka bayana kuwa si watoto wake watalazimika kwenda mahali pengine wasipopazoea na wanaweza wasipate huduma kama hapo.
Likikujia hilo wazo, fikiria kuhusu watoto na utakavyoitwa mahakamani kutoa ushahidi wa baya lolote litakalojitokeza.