Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Johari: Upofu wa kwenye Filamu ulinitesa

Johari

Muktasari:

Huyo ni Blandina Chagula maarufu Johari, ambaye mbali ya kuigiza amejaliwa kipaji akimudu vyema kuuvaa uhusika katika uigizaji na kuonyesha tofauti kati ya huzuni na furaha.

Alianza kuigiza tangu enzi za kundi la sanaa za maigizo la Kaole, lakini hajawahi kushuka kiwango katika uigizaji.

Huyo ni Blandina Chagula maarufu Johari, ambaye mbali ya kuigiza amejaliwa kipaji akimudu vyema kuuvaa uhusika katika uigizaji na kuonyesha tofauti kati ya huzuni na furaha.

Katika mahojiano yake na Starehe, Johari anaeleza mambo mbalimbali asiyoweza kuyasahau katika uigizaji wake ikiwamo kulibadili soko la filamu kutoka enzi za kutazamwa bure kupitia runinga na sasa kuuzwa kwa wananchi.

Mkali huyo wa filamu anasema kuwa hataisahau tamthilia ya Johari, iliyobeba umaarufu na kumpa jina la usanii ‘Johari’.

Anasema anaikumbuka tamthilia hiyo kwa kuwa ndiyo iliyowapa wazo la kubadili mfumo wao wa utendaji kazi kutoka tamthilia walizokuwa wakiigiza na kuonyeshwa bure kwenye runinga na kuigeuza kuwa biashara, ambapo badala ya shabiki kuvizia vipindi vya televisheni ili aitazame vipande vipande, ataipata yote kwa kulipia akinunua Dvd.

“Ilikuwa ngumu sana, lakini kwa kuwa tulikuwa watu makini akiwamo marehemu Steven Kanumba, msimamo ulikuwa huo. Kwa shida mfumo huo ukakubalika na unafanya kazi vizuri hadi sasa na kuwapatia mafanikio wasanii wa filamu kwa kiasi fulani, “anasema.

Johari anaitaja filamu iliyompa shida wakati wa kuitayarisha kuwa ni ‘Yellow Banana’, ambapo aliigiza kama mlemavu asiyeona (kipofu), huku ukweli akiwa anaona.

Anasema kuwa wakati wa kupiga picha za filamu hiyo alipata wakati mgumu kwa kuwa kuna eneo, Vicent Kigosi (Ray), aliyeigiza kama mumewe alimpiga kibao huku akitakiwa kutoonyesha kama alikuwa anauona mkono uliokuwa ukija kumpiga, wakati ukweli ni kwamba aliuona.

Johari anafafanua kuwa jambo jingine analolikumbuka katika filamu hiyo ni pale alipoanguka kwenye ngazi, huku Ray (mumewe), akiwa amekaa na kimada kwenye kochi.

Anaeleza kuwa kipande hicho kilikuwa kikimliza hata akiwa peke yake kwani alianguka kweli hadi ngazi ya mwisho huku Ray akimudu vyema kumtazama bila kushtuka kwa kuwa alilewa kwenye penzi la kimada, baada ya yeye kuwa kipofu.

“Nilipata shida sana, kila anapotaka kunipiga nakwepa, hivyo ilinichukua muda sana kufanikiwa kupata picha isiyokuwa na chembe ya mshtuko. Lakini nilipoanguka kwenye ngazi na Ray kutulia bila kushtuka. Roho iliniuma kama kweli, hata nilipokuwa nikilia, nililia kwa hisia za kweli,” anasema Johari.

Anaeleza kuwa mbali na waigizaji kujituma kuna mambo yanayokatisha tamaa katika uigizaji.

Johari anafafanua kuwa kuandikwa vibaya na uzushi kwa mambo yanayodhalilisha ndiyo mambo yanayokwaza na kukatisha tamaa katika uigizaji.

Anawashauri wasanii kupendana na kuacha kushabikia mambo mabaya yanayowakuta wengine, badala yake waungane kwa pamoja kuwasaidia.

“Kwenye misiba, hali ni nzuri tupo pamoja, lakini kwenye majanga mengine yanayotupata, hatutakiwi kuchekana. Badala yake tupeane moyo na ushauri wa jinsi ya kutoka huko,”anasema Johari.

Anaweka wazi kuwa nyota wa filamu anahitajika kuwa na moyo mgumu kwa kuwa uzushi na mambo mbalimbali ya kusingiziwa huchangia kwa kiasi kikubwa kuwaondoa kwenye tasnia hiyo waigizaji wengi wakubwa.