Taifa linahitaji mtazamo mpya wa elimu ya ufundi


Muktasari:

Zamani elimu hii haikuwa kipaumbele. Ilionekana i mkondo kwa watu wasioweza kusoma katika mfumo wa masomo ya kawaida.

Dar es Salaam.Kwa muda mrefu, elimu ya ufundi nchini Tanzania imeonekana kama njia ya pili ya kupata maarifa na ujuzi.

Watu waliopitia mfumo huu walionekana ni wale ambao hawakuwa wamefanya vizuri kiasi cha kutosha na kuwa na sifa ya kusoma elimu ya sekondari ambalo ni daraja la kati nchini kuelekea elimu ya juu.

Hali hii iliweka vikwazo vingi kwa wale waliotaka kujiendeleza kielimu kupitia mfumo wa elimu ya ufundi, ambapo njia ya kuanzia na kumalizia haikuwa wazi.

Kwa mfano, ilikuwa vigumu kwa mtu aliyemaliza elimu ya ufundi kuendelea na masomo ya shahada, kwa vile hakukuwa na programu za kutosha za aina hiyo. Waliojaribu kuhamia mikondo mingine ya elimu walikabiliwa na vikwazo vingi, na kufanya ionekane kuwa haiwezekani kusoma shahada kupitia mkondo wa elimu ya ufundi.

Hata katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu, kulitengwa nafasi chache kwa wale waliopitia elimu ya ufundi, lakini wengi walioingia, walikuwa ‘watu wazima’ waliochelewa kusoma' hata kama umri wao ulikuwa sawa na wenzao.

Kama haaitoshi, kulikuwa na kozi chache ambazo waliruhusiwa kuzisoma watu wa kada hii.

Madhara ya hali hii

Matokeo ya vikwazo hivi vilifanya jamii kudharau elimu ya ufundi na wengi kuikwepa, hasa kwa kuzingatia kuwa mkondo huo waliona usingewafikisha mbai kielimu zaidi ya kupata ajira.

Elimu ya ufundi ikajikuta katika nafasi ya kudhalilishwa na kuonekana kama ni kwa wale waliofeli kuingia katika elimu ya sekondari na vyuo vya elimu ya kawaida.

Kwa kutambua upungufu huu, Serikali iliamua kubadilisha sera na sheria ili kuwezesha ufundi kuonekana kama ni "elimu" yenye hadhi sawa na elimu ya sekondari.

Hivyo, sheria zilitungwa na lilikokuwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), likaanzishwa kusimamia elimu hiyo.

 Hali halisi vyuo vya ufundi

Wakati Serikali inaweka zaidi msukumo kwenye elimu ya shule za msingi na sekondari, hali ni tete kwenye vyuo vya ufundi.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaelezwa kujikita zaidi kwenye vyuo vya ufundi stadi (VETA), huku vyuo vya FTC vikiwa vimeachwa nyuma.

Vyuo vya FTC hapo awali vilifundisha ushoni, ufundi magari, na maendeleo ya jamii, lakini hali ya sasa haikisi sayansi na teknolojia. Vyuo hivi vimekosa vifaa vya kisasa na miundombinu yake ni chakavu.

Vyuo kama kile vilivyopo wilayani Monduli, Uyole na vingine vingi vimeachwa kwa muda mrefu bila mikakati ya kuviboresha.

Kwa mujibu wa mpango mpya wa Serikali, hata vyuo vya ualimu vitakuwa havitoi tena astashahada bali stashahada pekee, ambapo wanafunzi watalazimika kusalia vyuoni miaka mitatu badala ya miwili ya awali.

Hali katika vyuo vya FTC imezorota kutokana na ufinyu wa bajeti na kutopewa kipaumbele.

Wanafunzi hulipa ada ya Sh600,000 kwa mwaka, lakini fedha hizi hazitumiki kikamilifu kugharamia bajeti ya ndani ya taasisi husika.

 Serikali imeweka utaratibu ambapo ada za wanafunzi zinaingia moja kwa moja kwenye wizara husika, hali inayosababisha uongozi wa vyuo kuomba ruzuku za kuendesha vyuo hivyo.

Wamiliki wa baadhi ya vyuo wanatamani serikali iwape mamlaka kamili ya kukusanya na kutumia michango kuendeleza taasisi zao.

Wanasema kwamba maombi mengi hayafanyiwi kazi au kutolewa kwa wakati, hali inayozorotesha ufanisi katika utendaji na ufundishaji.

Licha ya tuhuma za ufisadi zilizokuwepo wakati wa utaratibu wa wakuu wa vyuo kukusanya fedha za Elimu ya Kujitegemea (EK), vyuo vilikuwa na miradi ya kujitegemea na kuhudumia jamii inayozunguka vyuo hivyo.

Wahitimu waliweza kuonesha tija katika soko la ajira kutokana na falsafa ya Mwalimu Nyerere ya elimu ya kujitegemea, ambayo iliwafanya wanafunzi kushiriki katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Hata hivyo, kizazi cha sasa hakina shauku ya kushiriki katika shughuli za kilimo kwa kutumia teknolojia za zamani.

Wanahitaji mafunzo ya kisasa kama vile ufundi magari, kompyuta, udereva na huduma za hoteli.

Hii ina maana kuwa ni muhimu kwa Serikali na wadau wa elimu kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa ili kuwapa wanafunzi ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.

Ni wakati wa kuimarisha elimu ya ufundi

Kwa ujumla, Serikali inapaswa kuimarisha mipango ya kuboresha elimu ya ufundi kwa kutoa rasilimali za kutosha na kuhakikisha kuwa vyuo vya FTC vinapata vifaa na miundombinu inayofaa. Hii itawezesha wanafunzi kupata elimu bora na kuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, na hatimaye kuboresha uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Ni muhimu pia kwa wadau wa elimu kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya kimataifa katika kuleta mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya elimu ya ufundi. Ushirikiano huu unaweza kusaidia kuleta teknolojia mpya na kuongeza uwekezaji katika vyuo vya ufundi, na hivyo kuboresha ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Vilevile, Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinavyotolewa na vyuo vya ufundi vinatambulika kikamilifu katika soko la ajira.

Hii itawawezesha wahitimu wa vyuo hivi kupata ajira bora na kujiendeleza kitaaluma. Pia, mfumo wa elimu unapaswa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na kuhusisha mafunzo ya vitendo zaidi ili kuwaandaa wahitimu kwa mazingira halisi ya kazi.

Katika mazingira ya sasa ya uchumi wa kidijitali, ni muhimu pia kuwekeza katika mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama)

 Vyuo vya ufundi vinapaswa kuanzisha programu za mafunzo ya Tehama na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ujuzi wa kisasa unaohitajika katika soko la ajira.

Hata hivyo, Serikali pia inapaswa kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wa vyuo vya ufundi ili kuongeza ari ya kujifunza na kufundisha.

Motisha hizi zinaweza kujumuisha kutoa mikopo ya elimu, kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu, na kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri.

Elimu ya ufundi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.


 Jitihada za mfano

Katika jitihada za kuimarisha sekta ya ajira nchini, Serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali imezindua miradi ya kuboresha elimu ya ufundi.

Mfano wa hivi karibuni ni mradi wa Skills for Development Tanzania (SET) awamu ya pili wenye thamani ya Sh24 bilioni. Mradi huu unalenga kuimarisha nafasi za ajira kwa vijana na walimu katika vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Mradi huu, ulioanza mwaka 2022 na kutarajiwa kumalizika mwaka 2026, unatekelezwa na serikali ya Uswisi kupitia shirika lake la kiserikali la Swisscontact.

Paul Medeye, mtaalamu wa mafunzo ya vijana wa Swisscontact, anasema mradi huu unahusisha tathmini ya mahitaji ya ujuzi, maendeleo endelevu ya kitaaluma, na mafunzo ya vijana.


 Mradi huu umelenga kuboresha maendeleo ya ujuzi wa ufundi kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, wakiwemo kina mama vijana katika mikoa ya Morogoro, Iringa, na Mbeya.

Kwa mujibu wa Medeye, waliamua kuendeleza mradi huu hadi awamu ya pili baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza ya SET I, ambayo iliwafaidisha zaidi ya vijana 10,000 kwa kuwapatia mafunzo endelevu ya kilimo, ufugaji wa kuku, na masuala mengine yanayohusiana.

Naibu Waziri Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, anasema mradi huu unasaidia Serikali kuboresha maendeleo ya ujuzi ili kuunda fursa za ajira kwa vijana, ambao ni takriban asilimia 70 ya idadi ya watu wa Tanzania.


Tujifunze kutoka nchi hizi

Nchi zilizoendelea kama Ujerumani, Uswisi, Finland, na Uingereza zimewekeza sana katika elimu hii na zimepata mafanikio makubwa. Kwa mfano, Ujerumani ina mfumo wa mafunzo ya ufundi (Dual System) ambapo wanafunzi wanapata mafunzo darasani na kwa vitendo kwenye kampuni. Hii imeimarisha uchumi wao.

Uswisi na Finland, wanafunzi wanapata mafunzo bora yanayowapa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Uingereza imeanzisha programu za mafunzo ya ufundi zinazoshirikiana na kampuni, na kuongeza nafasi za ajira kwa vijana.

Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi hizi kwa kuhakikisha vyuo vya ufundi vina vifaa vya kisasa, walimu waliohitimu vizuri, na mazingira bora ya kujifunzia.

Pia, ni muhimu kuanzisha programu za ushirikiano kati ya vyuo vya ufundi na sekta binafsi ili kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

Kwa kufanya hivyo, Tanzania itapunguza ukosefu wa ajira, kuongeza ujuzi wa wafanyakazi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ni wakati sasa kwa Serikali, wadau wa elimu, na jamii kuwekeza kikamilifu katika elimu ya ufundi ili vijana wapate ujuzi unaohitajika na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.


Mtalaa wa elimu ya amali

Licha ya kuonekana elimu ya ufundi kusuasua kwa miaka nenda rudi, kwa sasa ni kama Serikali imetambua ilipojikwaa.

Alianza Rais Samia Suluhu Hasan aliyechokoza mjadala wa kitaifa kwa kuagiza kufanyike mapinduzi ya mfumo wa elimu ili elimu inayotolewa ilenge kwenye ujuzi zaidi kwa minajili ya kuwasaidia wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu.

Watendaji wake kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wakaingia kazi na kufanya maboresho ya mtalaa wa elimu ya msingi na sekondari. Uboreshaji huo ukazaa mtalaa mpya wa elimu ya amali ambayo ina uhusiano mkubwa na elimu ya ufundi.

 Oktoba 10 mwaka 2023, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aligusia kwa nini Serikali imeanzisha elimu ya amali nchini.

Alisema lengo la Serikali ni kutaka kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambapo watakapomaliza wawe na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.

“Kwenye elimu hii ya amali tutakuwa na michezo, kilimo pamoja na ufundi ambapo mtoto atakapomaliza kusoma atapata na cheti chake alichosomea hivyo nawaomba kama kuna mtu ana uwezo wa kutoa elimu hii awasiliane na Serikali na sisi tutaboresha mazingira yake,” alisema .

Picha kwa hisani ya newtimes