Simulizi ya Millicent: Kutoka ujauzito hadi UDSM

Millicent Mavika
Muktasari:
- Baada ya milima na mabonde ya kusaka elimu, Millicent Mavika sasa ni mwajiriwa wa Brac Maendeleo kwenye mradi wa AIM, akiwa msaidizi wa mradi.
Dar es Salaam. Millicent Mavika, akiwa na umri wa miaka 17 bado akihitaji kulelewa na kupata elimu, alijikuta akiitwa mama, wakati ndio kwanza alikuwa kidato cha pili.
“Wakati nataka kurejea shuleni baada ya kujifungua, jamii inayonizunguka haikuniamini kwa sababu iliniona kama mtu niliyepoteza uelekeo. Si wao pekee, hata mimi kuna wakati nilijiona nimeshapotea, lakini nilijipa moyo,” anasema.
Millicent, mzaliwa wa Tanga kwa sasa ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika mazungumzo na Mwananchi hivi karibuni, mhitimu huyo anasema kichwani bado amebeba kumbukumbu ya milima na mabonde aliyopita katika safari ya kusaka elimu.
Anasema safari yake ya elimu ilianza kwa bashasha mwaka 2003 alipojiunga darasa la kwanza, pasipo kujua akifika kidato cha pili angekwaa kisiki kutokana na hali duni kiuchumi ndani ya familia yake.
“Bahati mbaya nilipofika kidato cha pili nilishindwa kuendelea na masomo baada ya mzazi wangu kushindwa kulipa ada na michango mingine ya shule. Nilibaki nikisubiri labda naweza kupata bahati ya kurudi shuleni,” anasema.
Akiwa bado nyumbani mwaka 2013 alipata ujauzito, jambo lililosababisha kutoelewana kati yake na wazazi.
“Nilipopata mimba hali ilikuwa mbaya, ndugu na wazazi hawakunielewa kwani kwa umri nilikuwa bado mdogo, kulitokea kutokuelewana na mama lakini baadaye akarudi kunisaidia, maana yeye ni mzazi,” anasimulia.
Wakati huo akiwa na miaka 17, anasema alijiona kama mtu aliyepoteza uelekeo lakini anachoshukuru ni kuwa baba wa mtoto wake hakukimbia majukumu, alikuwa naye bega kwa bega hadi alipojifungua.
Licha ya mama na mzazi mwenziwe kumsaidia, bado kiu yake ilikuwa kuendelea na masomo akitafuta kila namna ili kurejea shuleni.
Anasimulia wakati wengine wakimuona kama aliyepotea njia, yupo mtu aliyemtazama tofauti akiamini anastahili kupewa nafasi nyingine.
Millicent anasema kaka yake, Simon Mavika alimtafutia nafasi ya kurudi shule kwa sababu aliamini kitendo cha mdogo wake kupata ujauzito kilikuwa cha bahati mbaya.
“Millicent ni binti niliyekuwa nafahamu uwezo wake darasani, alipopata mimba nilijua changamoto alizopitia ndizo zilisababisha apate mimba lakini bado ana kitu cha ziada, alipopata nafasi nilimwambia hii ni nafasi nyingine Mungu amekupa ukiitumia vizuri utafanikiwa. Nashukuru naye alinilewa na kufika hapo alipo,” Simon.
Anasema licha ya changamoto nyingi ambazo Millicent amepitia, bado alisimama imara na kufika pale alipo sasa, ambako familia inajivunia.
Nafasi ya kurudi shule ilikuwa chini ya taasisi ya Brac Maendeleo, ambayo ilikuwa na madarasa maalumu kwa wasichana walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kupata ujauzito.
“Niliposema narudi shuleni, jamii inayonizunguka haikuamini kwa sababu iliniona kama ni mtu niliyepoteza uelekeo.Si wao tu, hata mimi kuna wakati nilikuwa nikijiangalia najiona kabisa nimeshapotea kwenye ramani, lakini nilijipa moyo,” anasema Millicent.
Anasema hilo lilionekana hata kwa familia yake kwani kipindi cha mwanzo walikuwa wakimchukulia kama mtu anayepoteza muda.
Baada ya kupata nafasi ya kurudi darasani kupitia madarasa waliyokuwa wamendaliwa akiwa na wenzake, anasema aliruhusiwa kwenda na mtoto, jambo lililompa urahisi wa kumuangalia mwanaye huku akijifunza.
Anaeleza jambo hilo lilimpa moyo kwani katika darasa hilo, pia baadhi ya watu walimpa ushirikiano kipindi chote cha masomo.
Millicent alisoma elimu ya sekondari kupitia mfumo wa QT, mwaka 2016 alikuwa hatua ya kwanza na mwaka 2017 akiwa hatua ya pili.
Mfumo wa elimu ya QT (Qualifying Test) ni mpango maalumu wa elimu unaowapa fursa watu waliokosa au kuacha masomo katika mfumo rasmi wa elimu, kuendelea na elimu ya sekondari.
Unawawezesha wanafunzi waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali kufanya mtihani wa QT, ambao unawaruhusu kusajiliwa kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne (CSEE) kama watahiniwa wa kujitegemea.
Kidato cha tano
Matokeo yalipotoka alichaguliwa kujiunga kidato cha tano mwaka 2018 katika shule iliyokuwa karibu na nyumbani kwao.
Hatua hii ilimfanya kuanza kumuacha mtoto kwa mama yake mdogo, ili aweze kuhudhuria masomo.
“Kutokana na hali duni ya maisha niliendelea kuwezeshwa, nililipiwa ada ya miaka yote miwili na kununuliwa vifaa ya shule ikiwemo vitabu. Hata baada ya kumaliza sekondari ya upili (kidato cha tano na sita) na kupata alama za kuniwezesha kwenda chuo, nilisaidiwa namna ambayo naweza kupata mkopo,” anasema.
Alipofika chuoni na kuchagua fani ya Sayansi ya Siasa anasema maisha yalikuwa kawaida lakini mchakamchaka wa fani aliyosoma anaukumbuka.
“Fani niliyokuwa nasoma ilinibidi kujua mambo mengi, hasa yanayoendelea kwa wakati huo katika jamii yetu. Lakini maisha mengine hasa ya kiuchumi hayakuwa mabaya sana kwa sababu nilifanikiwa kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), nililipiwa ada kwa miaka yote mitatu na pia kupata pesa ya kujikimu,” anasema na kuongeza:
“Kilichonivutia kusoma fani hii ni kwa sababu inahusiana na maisha halisi, watu na jamii kwa ujumla, niliami kwa kuichagua nitagusa jamii katika nyanja zote hata kwenye siasa pia.”
Anasema safari yake imezaa matunda na sasa ni mwajiriwa wa Brac Maendeleo kwenye mradi wa AIM, kama msaidizi wa mradi, na mtoto wake atatimiza miaka 11 Aprili mwaka huu.
“Wito wangu kwa kinadada wengine ni kumtanguliza Mungu katika kila jambo, wasikate tamaa hata kama wanapitia changamoto wanazodhani hawawezi kuondokana nazo. Pia waweke juhudi katika kila jambo wanalotamani walitimize katika maisha yao,” anasema.
Kwa upande wa Serikali, kiu ya Millicent ni kuona watoto wa kike wanaangaliwa hasa wale wanaopitia changamoto za kimazingira na kiumri.
Pia kutengeneza fursa nyingi za ajira ili waweze kujitengenezea kipato chao wenyewe.
Mwongoro rasmi
Millicent ni miongoni mwa waliorudi shuleni kabla ya kutolewa mwongozo rasmi wa kuruhusu wasichana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo mimba kurudi shuleni kupitia mfumo rasmi wa elimu.
Kabla ya mwongozo huo, Novemba 24, 2021 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiwa bungeni jijini Dodoma alitoa tamko kuhusu Serikali kuruhusu wanafunzi wote walioacha shule hata kwa sababu ya ujauzito kuwa wataweza kurudi shule katika mfumo rasmi.
Tamko hilo lilifuatiwa na Waraka wa Elimu namba 2 ambao unatumika kuwarejesha wasichana hao shuleni.
Tangu wakati huo hadi sasa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania (TEWW) kupitia Mradi wa Kuongeza Ubora wa Elimu ya Sekondari (Sequip-AEP) umefanikiwa kuwarejesha shule wanafunzi wa kike 10,239 waliokuwa wamekatisha masomo nchi nzima.
Taarifa hiyo ilitolewa na aliyekuwa naibu mkuu wa taasisi hiyo anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri, Profesa Philipo Sanga alipozungumza kwenye warsha ya watendaji wa taasisi hiyo Januari 28, 2024.
Profesa Sanga alisema wasichana waliorejeshwa shule mbali na sababu ya kupata ujauzito, zipo sababu nyingine zilizowafanya wakatishe masomo ikiwamo umaskini uliokithiri, kupata magonjwa yaliyowafanya washindwe kwenda shule kwa muda mrefu na utoro.
Alisema mradi huo umetazama changamoto hizo na kuhakikisha kuwa hazikwamishi tena ndoto za wanafunzi hao wa kike.
"Wakati mradi huu unaanza mwaka 2022, taasisi yetu iliweka malengo ya kupokea na kusajili wanafunzi wa kike waliokatisha masomo wapatao 12,000 katika kipindi cha miaka mitano ya mradi tayari tumeshapokea na kusajili wanafunzi 10,800 na wanaendelea na masomo," alisema Profesa Sanga ambaye sasa ni Mkurugenzi wa TEWW.
Hata hivyo, alisema baada ya kuona mwamko mkubwa wa wanafunzi wa kike kujitokeza kujisajili, mwaka huu wa nne wa mradi, Serikali imeona umuhimu wa kuwarejesha shule watoto wa kiume ambao nao walikatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya utoro.
Alisema kazi hiyo ya kuwarejesha wanafunzi imeanza na inaendelea vizuri na mpaka sasa wanafunzi wa kiume 888 wameshasajiliwa, lengo ni kusajili wanafunzi 1,000 nchini.