Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa awaita wadau kuchangia vitabu

Muktasari:

  • Takwimu zinaonesha uwiano wa vitabu na wanafunzi ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu katika masomo yasiyokuwa ya sayansi, huku kwenye masomo ya sayansi uwiano ukiwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka sekta binafsi nchini kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023  na mitaala iliyoboreshwa,  kwa kuhakikisha kuna upatikanaji wa kutosha wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Amesema tayari Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu kwa kujenga madarasa nchi nzima kwa shule za msingi na sekondari kinachobaki sasa ni utoshelevu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vitabu.

Majaliwa ameyasema hayo leo Machi 7, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yaliyobebwa na kauli mbiu ‘Kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja’.

Amesema ushiriki wa wadau katika elimu hususan kuwezesha upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi nchini, utasaidia kukabiliana na upungufu uliopo na kuiwezesha nchi kufikia lengo la kila mwanafunzi kuwa na kitabu cha kila somo.

“Hii kauli mbiu inasisitiza haki ya kila mwanafunzi kupata kitabu, inasaidia kupunguza pengo la elimu kwa mtoto anayetoka familia yenye uwezo na isiyo na uwezo kwa sababu wote watapata vitabu. Kufanikisha hili ni lazima sekta binafsi na wadau washirikiane na Serikali ili kuongeza wigo wa uchapaji vitabu,”amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Aneth Komba amesema matembezi haya pamoja na maadhimisho ya miaka 50 yamejikita katika kukusanya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, sekta binafsi, mashirika ya dini na watu binafsi.

Amesema Sh297.29 bilioni ndicho kinachotafutwa ili kuwezesha uzalishaji wa vitabu kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita.

“Katika kiasi hiki cha fedha Sh6.7 bilioni kwa kuanzia zitatumika kununua kompyuta mpakato 15,934 kwa ajili ya kupakia vitabu vya kiada na ziada katika nakala laini pamoja na maudhui mengine ya kielektroniki kwa wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita katika mikoa 10 Tanzania Bara na Zanzibar kwa uwiano wa kompyuta moja kwa mwanafunzi mmoja (1:1).

“Kuhusu uwiano wa kitabu na mwanafunzi kwa sasa hali ilivyo ni kuwa vitabu vingi tunavyochapa na kusambaza ni kwa uwiano wa 1:3. Hata hivyo vitabu vyote vya masomo ya sayansi katika baadhi ya maeneo tayari vinasambazwa kwa uwiano wa 1:1 na vitabu vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu vinasambazwa kwa uwiano wa 3:1,”amesema Dk Aneth.

Katika matembezi hayo Sh1.1 bilioni zilikusanywa ikiwa ni michango ya wadau katika kufanikisha kampeni ya kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja.

Akizungumza na Mwananchi,  Mwajabu Msonde ambaye ni mmoja wa washiriki wa matembezi hayo amesema kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuchangia kwenye elimu.

“Ni muhimu tukajenga huu utamaduni, kama tunavyochangia sherehe tuone haja ya kuchangia elimu tusiishie kuwa walalamikaji. Kila siku tunasikia kuna uhaba wa vitabu tujiulize tunafanya nini angalau kupunguza uhaba huo,  kwa hiyo naona sawa tuchangie watoto wapate vitabu,”amesema Mwajabu.

Kwa upande wake mdau wa elimu, Ochola Wayoga amesema licha ya kampeni hiyo kuwa na nia njema ni vyema ikatafutwa suluhisho la kudumu la kuhakikisha kuna uwiano mzuri wa vitabu na wanafunzi.

“Wadau wanaweza kuchangia vikanunuliwa hivyo vitabu kwa sasa, lakini nafikiri ni muhimu ukawekwa mpango endelevu katika eneo hili la vitabu kwa sababu kila mwaka wanaingia wanafunzi wapya kwenye mfumo wa elimu.

“Katika hilo la matumizi ya teknolojia nalo si baya ila ni lazima tuwe makini kuhakikisha lengo linafikiwa, wenzetu wa Kenya walijaribu hili lakini likashindikana sisemi kwamba kwetu litashindwa ila ni vyema tukajipanga vizuri,” amesema Wayoga.