Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuongeza uwekezaji, ATE yaitaka Serikali kupunguza tozo ya ujuzi

Chama cha Waajiri Tanzania chini ya Uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wake,Dk Aggrey Mlimuka kinapenda kuona mazingira ya uwekezaji yanakuwa salama nchini.Picha ya mtandao

Muktasari:

  • ATE inaona hoja ya kufanya hivyo licha ya tozo hiyo ya asilimia 4.5 kwenye mshahara ghafi wa kila mfanyakazi kupunguzwa, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kutoka asilimia sita za miaka ya nyuma.
  • Kwa miaka kadhaa, ATE imekuwa ikipigania kupunguzwa kwa ushuru wa ujuzi ambao mwaka 2014/15 ulikuwa asilimia sita kabla ya kupunguzwa hadi asilimia tano mwaka 2015/16 na asilimia 4.5 iliyotangazwa na Waziri wa Fedha Dk Philip Mpango, Juni mwaka jana.

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kinaitaka Serikali kupunguza Tozo ya Ujuzi na Maendeleo (SDL) inayolipwa na kampuni kutoka asilimia 4.5 mpaka mbili ili kupunguza gharama za ufanyaji biashara nchini.

ATE inaona hoja ya kufanya hivyo licha ya tozo hiyo ya asilimia 4.5 kwenye mshahara ghafi wa kila mfanyakazi kupunguzwa, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kutoka asilimia sita za miaka ya nyuma.

Kwa miaka kadhaa, ATE imekuwa ikipigania kupunguzwa kwa ushuru wa ujuzi ambao mwaka 2014/15 ulikuwa asilimia sita kabla ya kupunguzwa hadi asilimia tano mwaka 2015/16 na asilimia 4.5 iliyotangazwa na Waziri wa Fedha Dk Philip Mpango, Juni mwaka jana.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka anasema ushawishi unaendelea kwa kuishirikisha Serikali ili Bunge liridhie kufanikisha kushushwa kwa tozo hiyo mpaka asilimia mbili.

“Kama ambavyo tunasema, ni furaha yetu kuona tozo ya ujuzi ikiwa asilimia mbili ili kuwapunguzia mzigo waajiri ambao tayari wanalipa kodi nyingi. Pia, itakuwa ni moja ya vivutio vya uwekezaji na kuifanya Tanzania iongeze ushindani,” anasema.

Dk Mlimuka anasema kiwango cha sasa cha asilimia 4.5 siyo tu ni kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, bali kipo juu zaidi duniani.

Mbali na kiwango kuwa kikubwa, anasema ATE hawajaridhika na mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ambao unaifanya sehemu kubwa kuchangia bodi inayotoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, badala ya kusaidia ujuzi kama ilivyokusudiwa.

Kwa kawaida, theluthi moja ya mapato yatokanayo na tozo hii inabidi iende Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) na theluthi mbili zinazobaki kwa ajili ya Bodi Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB).

“Hatudhani kama hili ni jambo la haki kwa sababu hii ni kodi ya stadi na itumike kwa ajili hiyo, siyo kugharamia elimu ya juu ambayo tayari waajiri tumeshalipia. Msimamo wetu ni kwamba fedha zote ziende kuimarisha ujuzi,” anaeleza.

Kupunguzwa kwa tozo ya ujuzi kunatarajiwa kuwapunguzia wafanyabiashara hasa waajiri mzigo na kuwapa mwanya wa kuajiri watu wengi zaidi.

ATE inaamini kiwango cha chini cha tozo hiyo kitawafanya waajiri wengi wamudu kukilipa hivyo kuondoa uwezekano wa ukwepaji.

“Kwa mazingira ya sasa, unapoajiri wafanyakazi zaidi, mzigo wa kodi nao unaongezeka. Wakati mwingine inakatisha tamaa kuajiri,” anasema.

Licha ya tozo hiyo, waajiri nchini wanachangia asilimia 10 ya mishahara ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii bila kusahau wajibu wao kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ingawa wana bima walizowakatia.

“Mfuko ulioanzishwa wa kufidia wafanyakazi wanaoumia sehemu za kazi ni utaratibu mzuri, kwamba mfanyakazi akiumia afidiwe. Sasa kama lengo ni kumfidia mfanyakazi, mwajiri ana utaratibu huo kupitia bima.

Hatuoni kama hii ni haki kwa mwajiri huyo ambaye analipia bima wafanyakazi wake wanaoumia sehemu za kazi vilevile akalazimika kulipia asilimia moja ya mishahara ya wafanyakazi wake kama bima kwa wanaoumia. Kwahiyo unaona inalipwa mara mbili. Ni vizuri kama ingetumika hii kwa wale ambao hawana utaratibu wa bima,” anasema mkurugenzi huyo.

Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi inataka mwajiri wa sekta binafsi kuchangia asilimia moja ya malipo ya mishahara ya mwaka, wakati mwajiri wa sekta ya umma anatakiwa kuchangia asilimia 0.5.

ATE ni chombo kinachowawakilisha waajiri katika kuboresha maslahi yao na mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili kuwa na tija kwa pande zote; Serikali, wafanyakazi na waajiri wenyewe. Chombo hiki kinaundwa na kampuni, viwanda na vyama vingine vya waajiri.

Pia, Dk Mlimuka analalamikia sheria za kazi nchini na kusema baadhi ya vipengele siyo rafiki katika kutekeleza majukumu yao ya biashara. Anatolea mfano wa kumwachisha mtu kazi, kuwa kitendo hicho kimefanywa kuwa kigumu zaidi kuliko kuajiri.

Wakati mfanyakazi wa umma anaweza kusimamishwa kazi kisha akalipwa nusu mshahara, sheria za Tanzania zinataka mwajiri wa sekta binafsi kulipa mshahara wote iwapo atamsimamisha kazi mfanyakazi wake.

Dk Mlimuka anasema iwapo mwajiri akitaka kuongeza muda wa kazi, sheria inamtaka kuomba kibali kutoka kwa waziri husika, hali ambayo anashauri ingeachiwa vyama vya wafanyakazi.