Watafiti wagundua dawa asilia kuotesha nywele wenye vipara

Muktasari:
- Hii ni habari njema sana kwa watu wenye vipara au nywele zisizoota na pia wale wenye nywele zinazokatika hovyo, utafiti wa kisayansi umeonesha mmea huu una uwezo wa kipekee katika kuchochea ukuaji wa nywele na kuzuia kipara.
Arusha. Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) wamegundua dawa ya asilia yenye uwezo wa kuzuia nywele kukatika lakini pia kuotesha nywele kwa watu wenye vipara.
Pia wamefanikiwa kugundua dawa ya kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi yanayotokana na uzee.
Katika ugunduzi wa kwanza wa dawa ya kuotesha nywele kwa watu wenye vipara, imetokana na magome ya mti ulioko Wilaya ya Ngorongoro unaojulikana kama Mporojo na kwa Kiingereza unaitwa 'wormwood' kwa kitaalamu 'Albizia anthelmintica'.
Ugunduzi huu umetokana na utafiti wa kina wa miaka 12 tangu mwaka 2013 wa mimea ya tiba za asili ambayo iko katika hatari ya kutoweka ili kuihifadhi katika bustani za mimea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Aprili 22, 2025, Mkurugenzi wa Utafiti wa Tawiri, Dk Julius Keyyu amesema utafiti huo wa kusaka mimea yenye uwezo wa tiba za asili ulihusisha jamii za Kimasai, Hadzabe, Datoga na Iraqw na umefanikisha kupata matokeo mazuri.
"Hii ni habari njema sana kwa watu wenye vipara au nywele zisizoota na pia wale wenye nywele zinazokatika hovyo, utafiti wa kisayansi umeonesha mmea huu una uwezo wa kipekee katika kuchochea ukuaji wa nywele na kuzuia kipara," amesema.
Amesema kuwa ugunduzi huo iliyotokana na mmea huo ulioko Wilaya ya Ngorongoro imesajiliwa kwa jina la “Composition for Hair Growth Stimulation or Hair Loss Prevention Using an Extract of Albizia anthelmintica.”

Mkurugenzi wa Utafiti kutoka TAWIRI, Dk Julius Keyyu (wa pili kulia) na watafiti wengine kutoka TAWIRI wakionyesha sampuli za mimea iliyofanikisha ugunduzi wa dawa hizo.
Amesema kuwa mizizi ya mmea huo pia yamefanyiwa utafiti na umegundulika kutibu minyoo, malaria na maumivu ya miguu.
"Teknolojia ya ugunduzi huu tayari imekabidhiwa kwa kampuni ya Kimataifa ya Winwik Enterprise Ltd ya Korea Kusini kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za kuoshea nywele, dawa na mafuta.
Kutokana na manufaa makubwa yaliyooneshwa na mti huo wa mporojo, Tawiri imeanza utafiti wa namna bora ya kuhifadhi na kuzalisha kwa njia ya kilimo ili kuepuka kutoweka kwa mmea huo kutokana na uvunaji usiodhibitiwa wa magome porini.
Katika hatua hiyo pia Tawiri wamefanikiwa kugundua dawa ya kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi ya uzee inayotokana na mmea wa Mugufe au kitaalamu 'Maerua edulis)' unaojulikana kwa Kidatoga kama Ekwida.
"Gunduzi hii imesajiliwa kwa jina la “Composition for Skin-Lightening and Improving Wrinkles Using Extract of Maerua edulis.”
Dk Keyyu amesema teknolojia hiyo bado haijakabidhiwa kwa kampuni yoyote na inatangazwa kwa wadau wa sekta ya vipodozi kwa ajili ya uwekezaji.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Rogastian Msafiri amesema lengo la utafiti huo lilikuwa kufanya ugunduzi wa dawa na vipodozi yanayotokana na bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili kwa jamii za Kanda ya kaskazini.
"Lengo letu kubwa ilikuwa ni kubaini mimea inayotumika kwa tiba asili ambayo iko katika hatari ya kutoweka ili kuihifadhi katika bustani za mimea au ‘botanical garden isitoweke bali izidi kuwa msaada kwa jamii zetu na Taifa kwa ujumla".
Amesema mafanikio ya utafiti huo umefanywa na watafiti kutoka Tawiri, wakishirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Bioanuwai ya Korea Kusini (NIBR) na Taasisi ya Tiba Asili Tanzania (ITM)