Wataalamu wa afya waonya matumizi tiba mbadala kutibu macho

Muktasari:
- Kambi ya macho imeanza jana Aprili 18, 2025 , chini ya madaktari bingwa 68 na wataalamu wa afya iliyoratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust kwa kushirikiana na The Bilal Muslim Mission Tanzania.
Mbeya. Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila amesema hayo jana Aprili 18, 2025, baada ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini Dk Tulia Ackson, kuzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa wa macho.
Kambi hiyo ya siku nne imeratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust kwa kushirikiana na The Bilal Muslim Mission of Tanzania, inayohusha matibabu ya uchunguzi wa macho,upasuaji na utoaji wa miwani.
Dk, Mwasubila amesema asilimia kubwa wananchi wakiona dalili za awali ukimbilia kupata tiba mbadala jambo ambalo linaathiri mifumo ya mishipa ya fahamu na kupelekea kupata upofu wa kudumu na uoni hafifu.
"Kuna changamoto wapo wananchi wanashindwa kufika Hosptali kutokana na gharama kubwa, lakini wapo wenye fedha, lakini uingiza imani potofu na kukimbilia kwenye tiba mbadala pasipo kujua athari kiafya," amesema.
Dk Mwasubila ametaja makundi mengine ambayo yako kwenye hatari ya kupata upofu ni yaliyo athirika na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu.
Wakati huohuo, ameitaka jamii kubadili mifumo ya maisha na matumizi ya vyakula kwa lengo la kudhibiti magonjwa yasiyo ambukizwa ambayo yamekuwa ni hatari na kupoteza maisha ya watu.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya,Dk Yesaya Mwasubila akizungumza na wananchi waliojitoleza kwenye kambi la madaktari bingwa wa macho. Picha na Hawa Mathias
Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ameitaka jamii kutumia fursa hiyo na kwamba wamepokea madaktari bigwa na wataalam 68 kutoka hosptali mbalimbali nchini.
"Hii ni awamu nyingine, wamekuja mwaka juzi walifanya uchunguzi wa matatizo ya macho kwa zaidi ya wananchi 5,000, kati ya hao 260 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho," amesema.
Mratibu wa kambi hiyo ya macho, Ain Sharrif amesema ujio wao ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita na ombi la Spika wa Bunge Dk, Tulia Ackson ikiwa ni awamu ya pili katika Jiji la Mbeya.
Amesema mambo yanayofanywa na DkTulia ni kutekeleza maandiko ya vitabu vya dini kwa kutoa sadaka kwa kujali afya za wananchi wa Mkoa wa Mbeya.
Mkazi wa Mtaa wa Mabatini, Telezia Kisunga amesema ujio wa madaktari bingwa imekuwa mkombozi kwani idadi kubwa wanakwepa kwenda kupata huduma katika hosptali za serikali kutokana na gharama kubwa za matibabu.
Kuhusu suala la matumuzi ya tiba mbadala, amesema ni kweli wengi wanaona ni vyema kukimbilia huko kutokana na ukosefu wa kipato cha kukidhi gharama za matibabu.
Mkazi wa Forest, Peter Fredy amesema kwa kipindi kirefu anasumbuliwa na tatizo la macho lakini amekwama kufika kwa wataalamu wa afya kutokana na ukata.