Wanaume 305 wafunga uzazi, madaktari waeleza faida

Muktasari:
- Kufunga uzazi kwa wanaume maarufu ‘vasectomy’ ni njia ya uzazi wa mpango ambayo hufanywa kwa njia ya upasuaji kwa kukata au kufunga mirija inayosafirisha mbegu za uzazi za mwanaume, ili kuzuia mwanamke asipate mimba.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema jumla ya wanaume 305 kote nchini, wamejitokeza kufunga uzazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo yamesemwa Juni 2, 2025 na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, ililiomba kuiidhinishia Sh1.61 trilioni katika mwaka mwaka 2025/26 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbe 10.
Amesema ikilinganishwa na miaka iliyopita, idadi ya wanaume wanaojitokeza inaanza kuongezeka, hali inayochangiwa na elimu wanayoipata kutoka kwa wataalamu wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs).
“Wizara imeendelea kuhamasisha wanaume kutumia njia za uzazi wa mpango, ikiwemo ya kufunga uzazi (vasectomy), ambapo kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, wanaume 305 walitumia njia hiyo,” amesema Mhagama.
Wakati wanaume wengi wanaposikia kuhusu kufunga uzazi huwa wagumu kukubaliana na hatua hiyo, mwanaume aliyefanikiwa kufunga uzazi, amesema hatua hiyo imemwongezea muda wa kushiriki tendo huku ikiimarisha nguvu zake za kiume.
Mwanaume huyo, John Sai (49) mkazi wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, amesema alifikia hatua hiyo baada ya mke wake, Leah Kilasa kuchoka matumizi ya njia za uzazi wa mpango.
John anakuwa miongoni mwa asilimia ndogo ya wanaume wa Kiafrika waliofunga uzazi, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2013.
Faida za ‘vasectomy’
Kufunga uzazi kwa wanaume, ni njia ya uzazi wa mpango ambayo hufanywa kwa njia ya upasuaji kukata au kufunga mirija inayosafirisha mbegu za uzazi za mwanaume, ili kuzuia urutubishaji wa yai la mwanamke.
Upasuaji mara nyingi hufanywa kwa muda wa dakika takriban 15, mgonjwa huwa macho lakini huwa hapati maumivu yeyote na njia hiyo huzuia mimba kwa asilimia 95.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Remigius Rugakingira amesema njia ya kufunga uzazi kwa wanaume haiathiri nguvu za kiume, uwezo katika tendo wala kulifurahia tendo la ndoa. Mwanaume ataweza hayo yote isipokuwa hataweza kumpa mwanamke ujauzito.
“Ni wanaume wachache sana wanaofunga uzazi. Kufunga uzazi kwa wanaume unasaidia kupanga mipango ya baadaye kwa familia na taifa kwa ujumla,” amesema Dk Remigius.
Kuna faida kubwa za mwanaume au mwanamke kufunga kizazi kwani? Njia mbalimbali ambazo wanawake wamekuwa wakizitumia kupanga uzazi ikiwemo vidonge, sindano, vijiti na kitanzi zimekuwa zikadaiwa kuwa na matokeo hasi kwa baadhi yao.
Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya kinamama, Issa Rashid amesema njia hiyo ni nzuri na kwamba kwa sasa kuna teknolojia mpya za kufunga kwa matundu kwa wanaume na wanawake.
“Kufunga kizazi ni afya kwa wote wawili, kwani inawapa nafasi ya kufanya maamuzi na kutokuwa na hofu ya kushika mimba iwapo hawana uhitaji kwa wakati huo na pia inawapa muda wa kuwaangalia na kuwalea vizuri watoto walionao,” amesema.