Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simu za kisasa Zinawaathiri wengi kisaikolojia hata kusahau majukumu

Muktasari:

Hii inatokana na wengi kutumia simu za kisasa maarufu kama smartphone ambazo zina uwezo mkubwa wa mawasiliano ya intaneti.

Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa sasa ndiyo habari ya mjini. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaotumia mitandao ya kijamii sehemu mbalimbali duniani.
Hii inatokana na wengi kutumia simu za kisasa maarufu kama smartphone ambazo zina uwezo mkubwa wa mawasiliano ya intaneti.
Inakadiliwa kuwa kwa sasa mtu mmoja kati ya watu wanne duniani kote, anatumia mojawapo ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao hii, ni vijana wenye umri chini ya miaka 30. Na wengi hutumia simu za mkononi zenye mtandao wa intaneti na wengine hutumia kompyuta kutembelea mitandao hiyo. Pamoja na faida kadhaa za matumizi ya mitandao hiyo, baadhi ya watafiti wa maswala ya afya ya jamii wanabainisha kuwa matumizi ya mitandao hii yana athari kwa afya ya kisaikolojia na ubora wa maisha kwa watumiaji.

Jambo la kuvutia ni kwamba watafiti wamegundua kuwa watu wengi wanaotumia mitandao ya kijamii hawana utulivu wa kihisia na wengi wanakabiliwa na wasiwasi.

Katika utafiti ulioongozwa na Dar Meshi wa Chuo Kikuu cha Freie cha Ujerumani, inaonekana kuwa watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanapata uraibu fulani. Uraibu huo ni wa kutaka kuendelea kuwasiliana na hata kuona fahari kuzidi kuongeza idadi ya wale anaowasiliana nao. Wengi wao huhangaika ili kuinua kiwango chao cha kujisikia vizuri kihisia.

Mwaka 2012, shirika linalojihusisha na maswala ya hali ya wasiwasi nchini Uingereza (Anxiety UK) lilifanya utafiti kuhusu athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na kubaini kuwa asilimia 53 ya washiriki wa utafiti huo walikuwa wamebadilika kitabia kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Na asilimia 51 ya watu wote waliokiri kuwa walibadilika kitabia. Mabadiliko yao yalikuwa yameegemea kuwa hasi kuliko chanya.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 66 ya washiriki wa utafiti walikosa usingizi na utulivu wa kihisia kila walipomaliza kutumia mitandao ya kijamii.

Asilimia 55 walisema kuwa walihisi wasiwasi na kukosa furaha pale waliposhindwa kupata mtandao ili kuunganishwa na mitandao ya kijamii wanayoipenda.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Dk Linda Blair, mtaalamu wa saikolojia anasema kuwa watu wengi hupata athari za kisaikolojia kwa sababu wanashindwa kudhibiti matakwa yao,” anasema akisisitiza: afikiri jambo kubwa ni watu kuanza kutawaliwa na teknolojia, badala ya wao kuitawala,” anasema Dk Blair.

Katika utafiti mmoja ilibainika kuwa watu wengi kwa sasa hawana uwezo wa kukaa mbali na simu za mkononi, luninga na kompyuta.

Inapotokea kusahau simu au kushindwa kuingia katika mitandao ya kijamii, wengi hukabiliwa na matatizo ya kukosa utulivu wa kiakili na kuonyesha dalili sawa na zile anazoonyesha mtu anayekosa sigara.

Ili kufuatilia jambo hili, wanasayansi walifanya jaribio kwa wanafunzi wa vyuo vikuu 12 kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwataka wasitumie kabisa simu za mkononi, kompyuta, runinga na radio kwa saa 24 lakini wengi walionyesha dalili za kuweweseka kwa tamaa ya kutaka waingie kwenye mitandao ili wawasiliane.

Katika utafiti ulioongozwa na Profesa James A. Roberts wa Chuo kikuu cha Baylor, Marekani, ilibainika kuwa wanafunzi wa kike hutumia wastani wa saa 10 kwa siku kuperuzi mitandao kupitia simu za mikononi ikilinganishwa na wanaume ambao hutumia wastani wa saa nane.

Watafiti pia walibaini kuwa wanafunzi wengi hutumia wastani wa dakika 94.6 kwa kutuma na kusoma ujumbe mfupi wa maneno au picha, dakika 48.5 kutuma barua pepe na wastani wa dakika 38.6 kila siku kutembelea mitandao ya kijamii.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa matumizi ya kiwango hiki cha mitandao ya kijamii na matumizi ya simu kwa wanafunzi, yanaambatana na uwezekano mkubwa wa kufanya vibaya katika masomo.

Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la kisayansi la Journal of Behavioral Addictions toleo la 3(4) la mwaka 2014.

“Tafiti za siku za usoni ni muhimu zikajikita katika kuchunguza kwa nini simu za mkononi zinavuka msitari wa kuwa kifaa cha kusaidia watu na kuwa kifaa kinachoathiri kwa ubaya hali ya ustawi wetu na wa watu wengine,” anasema Profesa James A. Roberts.

Dk Larry D. Rosen, ambaye pia ni Profesa wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha California (CSU) anabainisha kuwa vijana wanaotumia kwa kiwango kikubwa mitandao ya kijamii, wanaonyesha dalili za afya mbaya ya akili ikiwa ni pamoja na kuwa na mwelekeo wa ukali na kupenda kujitenga.

Anasema licha ya kutaka kutumia muda mwingi wakiwa peke yao, wengi huwa na wasiwasi, msongo wa mawazo na matatizo mbalimbali ya kisaikolojia.

Utafiti mwingine unaenda mbali zaidi kwa kuhusisha matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya.

Utafiti huo unadai kuwa vijana wanapoona picha za watu wanaowasiliana nao wakiwa wanatumia dawa za kulevya nao hushawishika kuiga tabia hizo.

Asilimia 40 ya vijana walioshiriki utafiti huo walikiri kushawishiwa na mitandao ya kijamii na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya ya maisha ya vijana 2011 Marekani.

Mtaalamu wa Magonjwa ya Binadamu, Dk Shita Samwel anasema, teknolojia huwa inamrahisishia binadamu kupata taarifa, kuburudika na kuelimika.

Hasara za kiafya ni pale anapokitumia kifaa hadi kupata uraibu. Hii ni hali ya akili kujenga mazoezi kupita kiasi na kumfanya mtu kuwehuka na kuacha mambo mengine akitaka kutumia muda wote.

Dk Samwel anasema Hasara za uraibu wa mitandao ni pamoja na kupata unene uliopitiliza wa mwili na kuwa katika hatari ya magonjwa ya moyo na kisukari, mara nyingi wenye hawajishughulishi na mazoezi na kazi nyingine.

Tatizo jingine ni uoni hafifu na ulemavu wa macho wa kudumu. Ni tatizo ambalo lipo kutokana na vioo vya simu na kompyuta kuwa na mwanga ambao huiathiri lenzi ya jicho.

Anasema watu hawa pia hupatwa na tatizo la kukosa hamu ya chakula kutokana na muda wote akili yao huwa katika kile anachokifanya. Tendo la kupata hamu ya kula linahitaji fikra na hisia za mfumo wa fahamu ili kuuandaa mwili kupokea aina ya mlo ulioandaliwa.

“Kuna tatizo pia la upungufu wa maji mwilini inayochangiwa na kujishughulisha zaidi na jambo moja, uchovu na kichwa kuumwa,” anasema Dk Samwel.

Baadhi ya wenye uraibu wa mitandao, anasema hupata matatizo ya kisaokologia ikiwamo ile hali ya kumaliza hisia zake za kimapenzi kupitia mawasiano.

Wengine huamua kutazama picha za video za ngono au kuchati na wapenzi wa mitandaoni.

Anabainisha pia uraibu ni chanzo cha mifarakano ya wenza wengi kutokana na mwenza mwenye hali hii kutomjali na kupungua kwa hisia za mapenzi kwani akili yake imetawaliwa na yaliyomo mitandaoni.

Faida ya mitandao

Ingawa wataalamu wengi wanaangalia upande wa athari hasi zaidi, baadhi ya watafiti wanaamini kuwa mitandao ya kijamii inaweza pia kuwa na athari chanya.

Mitandao ya kijamii inaweza kutumika kama njia muhimu ya kutambua watu wenye afya njema kiakili na wenye matatizo ya afya ya akili.

Baadhi wanaamini kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii inasaidia watu kuwa na afya nzuri kisaikolojia kutokana na kuwaunganisha na marafiki wengi ambao huwawezesha kufanya vitu vya kufurahisha.

Utafiti ulioongozwa na James Fowler wa Chuo Kikuu cha California San Diego (UCSD), unaonyesha kuwa mitandao ya kijamii ni njia bora ya kueneza furaha. Utafiti huo ulibaini kuwa mtumiaji mmoja wa mtandao wa kijamii anapoweka habari za kufurahisha, huhamasisha wengine pia kuweka habari za kufurahisha katika kurasa zao.

“Utafiti wetu unaonyesha kuwa watu hawachagui tu watu wa kushirikiana nao, bali pia huwasaidia marafiki zao kubadili jinsi wanavyojisikia kihisia.

“Tuna ushahidi wa kutosha kuwa hali ya kihisia inaweza kusambaa kwa njia ya mtandao na kwamba hisia chanya husambaa haraka kuliko hisia hasi,” anasema Fowler.

Matumizi ya mitandao ya kijamii pia inaweza kuwa na athari chanya kwa watu waliotengwa na jamii zao kwani huwapa fursa ya kuwasiliana na watu mbalimbali duniani bila kipingamizi.

Hali hiyo inaweza kuwasaidia baadhi ya watu kuboresha afya ya kihisia na kutibu matatizo ya msongo wa mawazo, wasiwasi na sononeko.



Athari za mitandao
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na daktari bingwa wa magonjwa ya akili Ethan Kross wa Chuo Kikuu cha Michigani unabainisha kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kumfanya mtu akose furaha.
“Kwa juujuu unaweza kuona kuwa mitandao kama vile Facebook inawatimizia watu hitaji muhimu la mawasiliano ya kijamii, lakini badala ya kuimarisha ustawi wa kiafya, mitandao hii husababisha jambo lililo kinyume chake,” anasema Dk Kross.