Serikali kuwakutanisha wataalamu kufanya tafiti dawa za asili
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akipata maelezo ndani ya maabara ya Taasisi ya Mafunzo ya Afya Ifakara, mjini Bagamoyo
Muktasari:
- Serikali imeanza maandalizi ya kuwakutanisha wataalamu wa afya, tiba asilia, sheria na utafiti ili kuweka mkakati wa kufanyia tafiti za kisayansi dawa za asili, hatua inayolenga kuthibitisha usalama, ubora na ufanisi wake.
Bagamoyo. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametangaza mpango wa Serikali kuwakutanisha wataalamu wa afya, wataalamu wa tiba asilia, wanasheria na watafiti kwa lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa kufanya tafiti za kisayansi kuhusu dawa za asili zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali nchini.
Mpango huo unalenga kuthibitisha usalama, ubora na ufanisi wa dawa hizo kwa kuzingatia viwango vya kisayansi, hatua inayotarajiwa kuongeza imani ya jamii katika matumizi ya tiba asilia na kuwezesha dawa zitakazothibitika kutumika kwa usalama.
Wakati juhudi hizo za Serikali zikiendelea, ikumbukwe tayari Wizara ya Afya ilishatoa utaratibu wa dawa za asili kutumika katika hospitali 14 za umma ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Morogoro, Dodoma, Sekou-Toure Mwanza, Arusha Mount Meru, Tanga Bombo, na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo jana Jumatano, Julai 8, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha maarifa ya tiba asilia yaliyopo miongoni mwa wataalamu wa ndani yanatumika katika utafiti na maendeleo ya sekta ya afya.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na watafiti wa Taasisi ya Mafunzo ya Afya Ifakara, mjini Bagamoyo mkoani Pwani
"Tutakuwa na kikao kazi kitakachowakutanisha wataalamu kutoka hospitali, vyuo vikuu, Wizara ya Afya, wataalamu wa tiba asilia, wanasheria na watafiti ili kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kutumia maarifa yaliyopo kufanyia tafiti dawa za asili," amesema.
Amesema tafiti hizo zitahakikisha dawa zinazodaiwa kutibu magonjwa mbalimbali zinapimwa kisayansi ili kubaini ufanisi wake, kiwango sahihi cha matumizi pamoja na madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, ushiriki wa wanasheria katika mchakato huo utasaidia kulinda haki na ubunifu wa wataalamu wa tiba asilia watakaowasilisha maarifa yao, ikiwemo masuala ya umiliki wa ubunifu na hatimiliki.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameipongeza Taasisi ya Afya Ifakara kwa uwezo wake wa kufanya majaribio ya kitabibu (clinical trials) ya dawa zinazotengenezwa ndani na nje ya nchi, akisema uwezo huo unawajengea wataalamu wa Tanzania uzoefu unaohitajika katika tafiti za kimataifa.
Amesema Serikali sasa inataka kuona tafiti nyingi zaidi zikielekezwa kwenye dawa za asili zinazopatikana nchini kabla ya kuanza majaribio kwa binadamu.
"Tunataka yale tunayoyaamini yana uwezo wa kutibu yafanyiwe utafiti wa awali. Kabla ya dawa kujaribiwa kwa binadamu, lazima zipitie majaribio ya maabara ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake," amesema.
Ameeleza baada ya kukamilika kwa hatua hizo za awali na dawa kuthibitika kuwa salama, ndipo inaweza kuendelea katika hatua nyingine za majaribio ya kitabibu kwa mujibu wa taratibu za kisayansi.
Profesa Mkenda amesema dawa zitakazothibitika kisayansi zitatoa fursa ya kupata hatimiliki na kuzalishwa kwa viwango vinavyokubalika, huku akisisitiza kuwa lengo kuu la Serikali si mapato pekee bali kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.
Pia amesisitiza umuhimu wa Taasisi ya Afya Ifakara kuendelea kushirikiana na vyuo vikuu vya ndani na vya kimataifa ili kuimarisha uwezo wa Tanzania kufanya tafiti za kiwango cha kimataifa na kuzalisha maarifa pamoja na bidhaa zitakazonufaisha wananchi.
Julai 1, 2026, Profesa Mkenda alifungua mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambapo aliwataka watafiti kutumia mbinu za kisayansi kuthibitisha ufanisi wa tiba asilia ili kuimarisha mfumo wa afya na kuchangia safari ya kufikia Bima ya Afya kwa Wote (UHC).
Mkurugenzi wa Sayansi katika Taasisi ya Mafunzo ya Afya Ifakara, Dk. Ally Olotu akifanya wasilisho la namna taasisi hiyo inavyofanya kazi mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliyetembelea taasisi hiyo kwa ziara ya kikazi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sayansi wa Taasisi ya Afya Ifakara, Dk Ally Olotu, amesema taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kufanya tafiti za dawa za asili zinazogunduliwa nchini.
Amesema kwa muda mrefu taasisi hiyo imekuwa ikifanya tafiti za dawa zinazotengenezwa nje ya nchi, lakini sasa imefika wakati wa kuelekeza nguvu katika tafiti za dawa zinazotokana na rasilimali za Tanzania.
"Tutashirikiana na Serikali kuhakikisha dawa za asili zinazopatikana nchini zinafanyiwa tafiti za kisayansi ili kubaini usalama na ufanisi wake. Hili ni eneo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya na sayansi nchini," amesema.