Sababu umri wa Mtanzania kuishi kuongezeka hizi hapa

Dar es Salaam. Idadi ya miaka anayotarajia kuishi Mtanzania imeongezeka kutokana na kuboreshwa kwa mifumo ya huduma za afya na kampeni zinazoendelea za uhamasishaji wa maisha yenye afya bora.

Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu (HDR) ya mwaka 2023/24 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), inaonyesha umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 66.2 iliyoripotiwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia miaka 66.8 kwa mwaka 2023/2024.

Wachambuzi wanasema ongezeko hilo linaweza kuashiria matokeo chanya ya uboreshaji wa mifumo ya huduma za afya na kampeni zinazoendelea za uhamasishaji wa maisha yenye afya bora.

“Kwa sasa, idadi kubwa ya Watanzania wameanza kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao na kupokea matibabu ambayo yanachangia kurefusha umri wa kuishi.

“Ingawa bado hatujafanikiwa, bado tunaendelea kukabiliwa na magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza na ya milipuko tofauti ya nchi za Ulaya, lakini uelewa umeongezeka miongoni mwa watu siku hadi siku,” alisema mwanasayansi wa masuala ya tabia katika Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (Muhas), Profesa Deodatus Kakoko.

Alisema mambo mengine yanayochangia umri wa kuishi kuongezeka ni pamoja na uwepo wa taarifa za afya na ushauri unaotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusu huduma za matibabu na afya.

Profesa Kakoko alisema hata ulaji wa vyakula kwa Watanzania, pia umeimarika.

“Tabia hizi kwa pamoja zinachangia katika kuimarisha maisha marefu.” alisema na kuongeza kuwa hali ya maisha pia imebadilika kwa kiasi kikubwa, ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Kwa sasa kuna nyumba za kisasa ni tofauti na miaka ya nyuma, watu wamezidi kufahamu umuhimu wa usafi katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko.”

Kwa upande mwingine, mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka alisema uboreshaji wa huduma za afya umesaidia kwa kiasi kikubwa idadi kubwa ya watu kutambua afya zao mapema na kuanza matibabu.
Alisema hali hiyo imesaidia kuongeza umri wa kuishi kwa watu, tofauti na miaka ya nyuma.

Alisema awali huduma zilikuwa hazina uhakika na hata ufikiwaji wake ulikuwa wa mashaka, lakini kwa sasa kuna vituo vya afya na hospitali za kutosha.

“Siku hizi watu wanazingatia aina ya vyakula wanavyokula, na wengine wanafanya mazoezi ya mwili tumekuwa tunapuuzia ushauri wa Dk Janabi (Profesa Mohamed Janabi), lakini huo pia unasaidia sana kuongeza umri wa kuishi. Haya yote yanapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya milipuko na yale yasioambukiza,” alisema.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ni ya pili, baada ya Rwanda kwa wananchi wake kuwa na umri wa miaka 67.1 ya kuishi.

Burundi imeshika nafasi ya tatu, ikiwa na umri wa kuishi miaka 63.7 huku Uganda na Kenya zikishika nafasi ya nne na tano zikiwa na miaka 63.7 na miaka 62.1 katika mfuatano huo.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni miaka 59.7 huku Somalia, mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikifikia miaka 56.1.
Sudan Kusini imeshika mkia kwenye orodha hiyo, ikiwa na umri wa kuishi wa miaka 55.6.

Ripoti hiyo inaeleza kumekuwa na maendeleo yasiyo sawa yanayowaachia watu umasikini zaidi, ukosefu wa usawa na kuchochea mgawanyiko wa kisiasa katika kiwango cha kimataifa.

Inaeleza kluwa wakati nchi tajiri zinakabiliwa na viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu, nusu ya nchi maskini zaidi duniani zimesalia chini ya kiwango chao cha maendeleo,

na inaainisha kuwa pato la Taifa kwa wananchi, elimu na umri wa kuishi imekuwa sehemu isiyo na usawa.

Miongoni mwa nchi 35 zilizoendelea kwenye eneo ya maendeleo ya binadamu zaidi ya nusu (nchi 18), bado hazijarejea katika viwango vyao vya maendeleo ya binadamu tangu mwaka 2019.

“Kuongezeka kwa pengo la maendeleo ya binadamu, ŕipoti inaonyesha kuwa mwelekeo wa miongo miwili wa kupunguza kwa kasi kukosekana kwa usawa kati ya mataifa tajiri na maskini sasa uko kinyume. Ni lazima tuongeze uwezo wetu wa kushughulikia changamoto zilizopo na kuhakikisha matarajio ya watu yanatimizwa,” alisema Mkuu wa Mpango wa Maendeleo (UNDP), Achim Steiner katika ripoti hiyo.