Umri wa Watanzania kuishi waongezeka

Umri wa Watanzania kuishi waongezeka

Muktasari:

  • Uboreshaji wa huduma za afya, kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto wachanga, kuongezeka kwa kipato ni miongoni mwa mambo yaliyochangia umri wa kuishi Mtanzania kuongezeka

Dar es Salaam. Makadirio ya ukomo wa umri wa kuishi kwa Watanzania yameongezeka kutoka miaka 67 na miezi mitatu mwaka huu hadi kufikia ukomo wa miaka 74 ifikapo 2035, ikiwa ni ongezeko la miaka saba na miezi miwili ndani ya miaka 12 ijayo.

Ripoti ya Makadirio ya Taifa ya Idadi ya Watu nchini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha, kati ya mwaka 2013 hadi mwaka huu, wanaume waliongeza umri wa kuishi kwa miaka minne na miezi sita, huku wanawake wakiongeza miaka mitano na miezi minne, sawa na upungufu wa miezi minane kwa mwanamume.

Wanawake pia watakuwa na umri wa kuishi kuanzia sasa hadi ifikapo mwaka 2035, wakikadiriwa kuishi miaka sita juu zaidi ya ukomo wa kuishi kwa mwanamume.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti Repoa, Dk Donald Mmari alisema uboreshaji wa huduma za afya, kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto wachanga, kuongeza kipato cha watu ni maeneo ya viashiria vya Serikali ambavyo huchochea ongezeko la miaka katika makisio ya umri wa kuishi nchini.

Katika ripoti hiyo ya NBS, idadi ya vifo vya watoto wachanga ilikadiriwa kupungua kutoka vifo 42 hadi 43 kwa kila vizazi 1,000 mwaka 2013 hadi kufikia vifo 26 kwa kila vizazi 1,000 mwaka huu. Ifikapo mwaka 2035 inakadiriwa vifo hivyo kupungua hadi 13 kwa kila vizazi 1,000.

Wakati vifo hivyo vikipungua, takwimu pia zinaonyesha ukuaji katika wastani wa pato la kila Mtanzania kutoka Dola 867 kwa mwaka 2016 hadi kufikia dola 1,080 mwaka 2020, kiwango kilichowezesha kuingia uchumi wa kipato cha kati ngazi ya chini.

“Viashiria vikubwa ni kuimarika kwa afya na lishe bora, sasa hii ya kipato kuimarisha pia ina uhusiano kwa sababu ili awe na afya bora atalazimika kununua dawa na kula vizuri,” alisema Mchumi mwandamizi na mstaafu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samuel Wangwe.

Kwa mujibu wa hotuba ya hayati Rais John Magufuli inayohusu utendaji wa 2015/2020, kwa idadi ya wanaojifungulia vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2020, huku idadi ya rufaa za kwenda nje ya nchi zimepungua kwa asilimia 95.

Kutokana na ongezeko la makadirio ya ukomo wa umri wa kuishi, Dk Mmari anashauri kwamba mifuko ya hifadhi za jamii itazame hilo kwa kuongeza uwekezaji wa kuingiza wanachama wapya watakaokuwa na uwezo wa kulipa wanachama wastaafu wengi uzeeni.


Viongozi wa dini

Makadirio hayo yanaungwa mkono na mitazamo ya viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo ambao licha ya kuamini mipango yote ya ukomo wa umri wa kuishi iko chini ya Mungu, pia wanaamini katika misingi ya kanuni za kuishi mwanadamu ili kufikia malengo hayo.

“Sisi tunaamini umri wa kuishi binadamu ni matakwa ya Mwenyezi Mungu aliyempangia kuishi,” alisema Sheikh Khamis Mataka, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) alipozungumza na gazeti hili jana.

“Lakini pamoja na hivyo, bado tunaamini kuna kanuni na sababu za kuzingatia, kwa mfano usipokula vizuri afya yako itatetereka, ukifanya jambo fulani afya yako itaharibika au kuimarika, hata Uislamu tumekuwa tukifundisha namna ya kula vizuri, kutunza afya, kwa hiyo Watanzania wazingatie kanuni.

Askofu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) alisema kisayansi mtazamo huo uko sahihi, lakini upande wa imani anaamini Mungu ndiye ametoa zawadi hiyo ya kuongeza umri wa kuishi baada ya kuongeza idadi ya wanaomuabudu na kutii amri zake.

“Kuishi maisha marefu ni ishara nzuri kwa sababu maisha ni zawadi ya Mungu, ni jambo la kumshukuru Mungu sana ambaye ametuahidi mwenyewe katika amri zake kumi, kwamba ukiwaheshimu baba na mama utaishi miaka mingi hapa duniani, tuendelee kutii amri zake.”


Tahadhari kiafya, saikolojia

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichwale alitoa tahadhari akisema Watanzania wanatakiwa kulinda afya zao kwa kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ili kufikia makisio hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) hadi Aprili, 2021 magonjwa hayo yamekuwa yakiua watu milioni 41 kila mwaka duniani, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote. Katika kundi hilo, watu milioni 15 wana umri wa kati ya miaka 30 na 69.

Charles Mhando, mwanasaikolojia nchini anataja maeneo sita yaliyowezesha kuongeza umri na umuhimu wa kuzingatia kuongeza zaidi umri wa kuishi, ikiwamo umuhimu wa kulinda afya ya akili.

“Muda wa kuishi unaongezeka kwa sababu Watanzania wengi wanajitambua, kwa mfano zamani waliwaza sana kuhusu maisha yao, mtu akikosa 1,000 leo anajua maisha ndio basi tena, lakini sasa hivi unaambiwa ukikosa leo utaipata kesho, watu wamepunguza presha za maisha,” alisema.

Maeneo mengine ni kuongezeka kwa klabu za mazoezi katika mikoa mbalimbali nchini, kupata uhakika wa chakula ambacho ni msingi wa mawazo zaidi katika mahitaji ya msingi, huku wengi wakionekana kuzingatia mlo kamili wa chakula.

“Usomaji au ufuatiliaji wa maudhui ya kuumiza, habari mnazozalisha zina mchango mkubwa wa kuongeza muda wa kuishi au kupunguza, kama mtu atasoma mfululizo wa habari za matukio ya kuumiza, lazima ataathirika kisaikolojia,” alisema Mhando na kuongeza:

“Ndio maana tunashauri wenye msongo wa mawazo kuhakikisha muda mwingi wanafungua mitandao ya kijamii kuangalia kurasa za vichekesho, kutazama sinema zisizoumiza, kufanya mazoezi, kupata muda wa kulala.”


Tanzania na Dunia

Tovuti ya tathimini ya Idadi ya watu duniani(World Population review) mwaka 2022, inaonyesha Tanzania inatajwa kuwa na ukomo wa miaka 66 mwaka huu, ikiwa ni pungufu ya mwaka mmoja katika makadirio ya NBS,ikionyesha kuwa juu ya mataifa 38 ya Afrika yakiwamo mataifa 11 ya SADC.

Katika takwimu hizo Watanzania wana uhakika wa kuishi zaidi ikilinganishwa na majirani zake Malawi(65.1), Zambia(64.4), Uganda(64), Burundi(62.3), Zimbabwe(61.8), DRC Kongo(61) na Msumbiji(61.7). Hong Kongo inaongoza(87.1), Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa mwisho(54)