Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini baadhi ya wanawake hukoma hedhi kabla ya umri

Muktasari:

Ingawa kuna wanaowahi au kuchelewa kidogo, kwa kawaida wasichana huanza kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza wanapofikia umri kati ya miaka 12 na 16. Hali hii muhimu katika maisha na makuzi ya msichana; hujulikana kama ‘kuvunja ungo’. Msichana anapovunja ungo, anatazamiwa kuendelea kupata damu ya hedhi kila mwezi hadi anapofikia kipindi cha kukoma hedhi.

Tumepokea maswali mengi juu ya suala la kukoma hedhi ghafla, leo tutajibu swali hili.

Ingawa kuna wanaowahi au kuchelewa kidogo, kwa kawaida wasichana huanza kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza wanapofikia umri kati ya miaka 12 na 16. Hali hii muhimu katika maisha na makuzi ya msichana; hujulikana kama ‘kuvunja ungo’. Msichana anapovunja ungo, anatazamiwa kuendelea kupata damu ya hedhi kila mwezi hadi anapofikia kipindi cha kukoma hedhi.

Katika sehemu mbalimbali duniani, wanawake wengi hufikia kipindi cha kukoma hedhi wakiwa na umri kati ya miaka 45 na 55, lakini wapo wachache wanaofikia kipindi hicho wakiwa na miaka 60 au zaidi.

Utafiti uliofanywa na Rosemary Mrina mwaka 2009 mkoani Singida, ulibainisha kuwa wanawake wengi hapa nchini hufikia kipindi cha komahedhi wakiwa na wastani wa miaka 47.

Komahedhi ni hali ya kawaida ya utendaji wa mwili wa mwanamke inayotokea mwanamke anapopoteza uwezo wa kuzaa kutokana na kuwa na umri mkubwa.

Dalili ya kwanza inayoonyesha kuwa mwanamke amefikia kipindi cha komahedhi, ni kutokuona damu ya hedhi kila mwezi kwa zaidi ya miezi 12 mfululizo. Mwanamke anapofikia hali hii hawezi kupata damu ya hedhi.

Katika hali ya kawaida siyo rahisi msichana mwenye afya njema kukoma hedhi katika kipindi cha ujana. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, baadhi ya wasichana huingia mapema katika kipindi cha komahedhi wakiwa na umri kati ya miaka 13 na 19 na wanawake wengine huingia katika kipindi hicho wakiwa na umri chini ya miaka 40.

 

Matatizo ya kukosa hedhi

Katika ulimwengu wa leo ambao unasisitiza wasichana kupata elimu ya darasani hadi kufikia chuo kikuu, kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wasichana na wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta elimu, kujikuta wanakoma kupata hedhi katika kipindi cha kuhangaikia elimu. Hali hii ya komahedhi ya mapema, huwanyima baadhi ya wasichana na wanawake fursa ya kupata watoto na kufurahia maisha ya ndoa zao. Halikadhalika wasichana na wanawake wengi wanaopata hali hii, wanakabiliwa na athari hasi za kisaikolojia na wakati mwingine huangukia katika imani za kishirikina kwa kuhisi kuwa wamelogwa.

Mbali na dalili ya kutokuona damu ya mwezi, msichana pia anaweza kutokwa jasho mara kwa mara wakati wa usiku, kukosa usingizi na kukojoa mara kwa mara.

Pia, kupungua kwa hamu ya tendo la kujamiiana, kupungua kwa majimaji yanayolainisha uke wakati wa tendo la ndoa, ukavu wa ngozi na kukasirika bila sababu za msingi. Mambo hayo huongeza hali ya msongo na kumnyima msichana furaha na raha.

Watafiti wengi wa maswala ya afya ya uzazi wanabainisha kuwa kutokana na sababu mbalimbali, kati ya asilimia moja hadi nane ya wanawake walioko katika umri wa kuzaa hukabiliwa na tatizo hili la komahedhi ya mapema.

Huko nchini Marekani, takwimu zinaonesha kuwa asilimia nne ya wanawake hupata hali hii. Pia utafiti uliofanywa na Taasisi ya Mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi (ISEC) iliyoko Bangalore,India nao unabainisha kuwa, wastani wa asilimia nane ya wanawake wenye umri kati ya miaka 35 na 39 wanapata komahedhi ya mapema kuliko walivyotarajia.

Tatizo hili linaweza kusababishwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, tiba ya upasuaji wa kuondoa mfuko wa kizazi, tezi za mayai, matibabu kwa kutumia mionzi, dawa za kutibu saratani, athari ya baadhi ya kemikali au urithi wa vinasaba vyenye mwelekeo wa tatizo hili.

 

Kinachosababisha komahedhi

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 10 na 20 ya wasichana na wanawake wote wanaopata tatizo hili, ni wale ambao katika familia zao kuna historia ya kutokea kwa komahedhi ya mapema. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha California San Francisco (UCSF) cha Marekani na kuchapishwa mwaka 2013 katika Jarida la Cancer, ulibainisha kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya urithi wa vinasaba vya aina ya BRCA na kutokea kwa komahedhi ya mapema.

“Matokeo ya utafiti wetu yanaonyesha kuwa mabadiliko yanayotokea katika vinasaba hivi, yana uhusiano na kutokea kwa mapema kwa hali ya komahedhi, hali ambayo inaweza kusababisha ongezeko la hali ya ugumba,” anasema Dk Mitchell Rosen, Profesa wa Sayansi ya Uzazi na Magonjwa ya Wanawake, Chuo Kikuu cha California San Francisco.

Mambo mengine yanayochangia kutokea kwa komahedhi ya mapema ni pamoja na tezi za mayai kushindwa kufanya kazi ya kutengeneza mayai na kuzalisha vichocheo vinavyodumisha hali ya jinsi ya kike, lishe duni, matumizi holela ya dawa kama vile Tamoxifen, uvutaji mkubwa wa sigara, magonjwa ya tezi la shingo pamoja na kisukari. Vyanzo vingine ni uambukizo wa virusi vya mafindofindo, ugonjwa wa Kifua kikuu pamoja na msongo wa mawazo wa muda mrefu. Wasichana wanaofanya mazoezi mazito ya kukimbia pia wanaweza kupata hali hii.

Kuhusu vyanzo vya tatizo hili, Dk Marjorie Dixon, bingwa wa tiba za uwezeshaji wanawake wagumba kupata watoto katika Kituo cha Sayansi za Afya cha Sunnybrook kilichopo jijini Toronto nchini Kanada, anasema: mara nyingi sababu hazieleweki ila baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa ni kutokana na kupungua kwa vichocheo vya jinsi mwilini hasa estogeni.

 

Wenye tatizo wafanye nini?

Msichana anayepata koma hedhi ya mapema, anashauriwa kuonana na mtaalamu wa magonjwa ya wanawake haraka ili kufanyiwa tiba pamoja na uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kuchunguzwa afya yake kuhusu uwezekano wa kuwa na tatizo la kisukari au maradhi ya tezishingo.

Ili kupunguza athari mbaya za hali hii inashauriwa kuboresha hali ya lishe kwa kutumia vyakula vyenye vitamini na madini kwa wingi. Matumizi ya maharage ya soya au mazao yake pia yanasaidia kwa vile yana dawalishe aina ya phytoestrogens kwa wingi ambayo inasaidia katika kudumisha afya ya jinsi kwa wanawake wa rika zote.

Mazoezi mepesi kila siku pia yanasaidia kupunguza athari mbaya za tatizo hili kwa wasichana na wanawake kwa ujumla.

 

Maoni au maswali tuma [email protected] au 0713247889