JICHO LA DAKTARI: Jinsi ya kukabili tatizo la michirizi ya ngozi mwilini

Michirizi ikiwa inaonekana kwenye eneo la tumbo. Huweza pia kutokea kwenye maeneo mbalimbali ya mwili kama vile karibu na makwapa, mapaja, kiuno, mikononi na miguuni.
Muktasari:
- Ni muhimu kufanya mazoezi ya mwili ili kupunguza unene na kiasi cha mafuta ili yasirundikane kwenye ngozi.
- Ni muhimu pia kupunguza uzito wa mwili taratibu.
- Wataalamu wa afya wanaweza kufanya upasuaji ili kuondosha michirizi kwenye ngozi hasa pale inaposababisha matatizo makubwa ya kisaikolojia.
Michirizi ya ngozi ni moja ya matatizo yanayowapata watu wengi hasa wasichana na wanawake. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wengi wanasumbuliwa na tatizo hili. Kati ya asilimia 50 na 80 ya wanawake pamoja na asilimia 40 ya wanaume husumbuliwa na tatizo hili.
Michirizi hii inaweza kujitokeza katika sehemu mbalimbali za mwili ambazo ngozi yake ina mafuta mengi kama vile sehemu ya chini ya tumbo, mapajani, mikononi, kwenye matiti, kwapani na kwenye makalio. Kwa wanaume michirizi hii inaweza kutokea mabegani na mgongoni.
Chanzo cha tatizo
Ngozi ya binadamu ina matabaka matatu yaani tabaka la juu, tabaka la kati na tabaka la chini. Michirizi ya ngozi huanzia katika tabaka la kati ambalo kimsingi ndilo linaloipatia ngozi uimara na uwezo wa kuvutika. Sehemu hii ya ngozi inapovutika kupita kiasi ndani ya kipindi kifupi na ikaendelea kuwa katika hali hiyo, ngozi huvimba na kusababisha kuchanika kwa nyuzi za ngozi ziitwazo collagen. Hali hii pia husababisha upungufu wa elastin na fibronectin, vitu ambavyo huifanya ngozi kuwa imara na kuvutika kwa urahisi.
Uvimbe na mchaniko wa tabaka la kati la ngozi unapopona, huacha makovu yanayoonekana kama michirizi ya kudumu kwenye ngozi. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Dk Frank Wang, profesa mshiriki na daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi katika Chuo Kikuu cha Michigan katika ripoti ya utafiti wake iliyochapishwa Novemba 2015 katika jarida liitwalo British Journal of Dermatology.
Hali hii kwa wanawake hujitokeza zaidi wakati wa ujauzito kiasi kwamba asilimia 90 ya wanawake wajawazito hupata tatizo hili kwa ukubwa unaotofautiana. Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa wasichana wanaobeba ujauzito katika umri mdogo wanakabiliwa na tatizo hili zaidi ya wengine. Takribani asilimia 70 ya wasichana hupata tatizo hili wakati wa barehe na takribani asilimia 40 ya wavulana nao hupata tatizo hilo katika kipindi hiki cha makuzi. Chanzo chake katika kipindi hiki ni ongezeko la kiasi kikubwa cha homoni za mwili.
Wanaume wanaofanya mazoezi ya kutunisha misuli pia wanaweza kukabiliwa na hali hii kutokana na mabadiliko ya muda mfupi ya umbo la miili na misuli yao. Watu wanene au wanaopoteza uzito wao ndani ya kipindi kifupi, nao pia wanaweza kupata tatizo hili.
Baadhi ya watafiti wanahusisha hali hii na urithi wa vinasaba vya kijenetiki. Wanaamini kuwa kama mmoja wa wazazi ana tatizo hili basi kuna uwezekano mkubwa watu wa uzao wake kupata tatizo hili pia.
Jambo jingine ambalo linaweza kusababisha hali hii ni matumizi ya vipodozi vyenye viambato vya dawa aina ya cortisone kama vile clobetazole au matumizi ya dawa hizo za hospitalini kwa muda mrefu. Cortisone hufanya ngozi kuwa laini na kupoteza uwezo wake wa kuhimili hali ya ngozi kuvutika. Hali hii pia inaweza kutokea katika baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa unaosababisha unene wa kupindukia(Cushing syndrome).
Jambo jingine linalochangia kutokea kwa tatizo la michirizi ya ngozi ni lishe duni hasa ulaji wa vyakula vyenye upungufu wa madini ya Zinc. Madini haya husaidia mwili kuzalisha kiasi cha kutosha cha chollagen, ambayo ni muhimu kwa ajili ya ngozi kuwa na uwezo wa kuvutika bila kupata athari mbaya. Ukosefu au upungufu wa Zinc husababisha ngozi kupata michirizi au milia kwa urahisi.
Madhara yake
Ingawa mara nyingi michirizi ya ngozi haina madhara makubwa ya kiafya, baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa tatizo hili la ngozi linaweza kusababisha athari za kisaikolojia kwa baadhi ya watu wenye tatizo hili. Hii ni kutokana na ukweli kuwa michirizi hii inaharibu mwonekano na mvuto wa mtu hasa katika sehemu zisizofunikwa na mavazi au pale mtu anapovua nguo.
Katika utafiti mmoja ilibainika kuwa, karibu nusu ya wanawake hasa vijana wenye michirizi ya ngozi wanasononeshwa na makovu ya kudumu ya michirizi hii. Wengi walibainisha kuwa makovu haya yanaathiri vibaya uchaguzi wa mavazi yao na jinsi wanavyoamua kuvaa. Asilimia 20 walidai kuwa wamekuwa wakijaribu kuwaficha wapenzi au wenzi wao wa ndoa kuhusu tatizo hilo.
Baadhi ya wachunguzi wa maswala ya afya ya uzazi pia wanadai kuwa, wanawake wenye michirizi ya ngozi hasa wakati wa ujauzito wanaweza kukabiliwa na tatizo la kushindwa kudhibiti mkojo mara baada ya kujifungua kutokana na udhaifu wa misuli ya pango la nyonga. Michirizi hii pia inaweza kusababisha muwasho, hisia za ngozi kuwaka moto na ukavu wa ngozi kwa baadhi ya watu.
Utafiti mmoja uliochapishwa mwaka 2012 na Dk Jacquelyn Dosal wa Chuo kikuu cha Miami, Marekani ulibainisha kuwa michirizi ya ngozi inaweza kuchanika na kusababisha vidonda kwa wagonjwa wenye tatizo la saratani.
Jinsi ya kukabiliana nalo
Njia ya kwanza ya kukabiliana na tatizo hili ni kuzingatia kanuni bora za lishe pamoja na kunywa maji ya kutosha kila siku. Ni vizuri kula chakula chenye madini ya kutosha ya zinc na aina mbalimbali za vitamini ili kuimarisha afya ya ngozi.
Njia nyingine inayosaidia kukabiliana na tatizo hili ni kuchua misuli mara kwa mara ili kuongeza kiasi cha damu. Utafiti uliofanyika nchini Uturuki mwaka 2012 unaonyesha kuwa wanawake wanaochua misuli kwa angalau dakika 15 kwa kutumia mafuta ya mlozi wanapunguza uwezekano wa kupata michirizi ya ngozi.
Utafiti mwingine uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba, Tehran huko Iran nao ulionesha kuwa kuchua misuli kwa mafuta ya mizeituni wakati wa ujauzito, hupunguza uwezekano wa kupata michirizi ya ngozi.
Maoni au maswali tuma [email protected] au 0713247889