Hivi ndivyo anavyopaswa kulala mjamzito

Dar es Salaam. Mwanamke anapopata ujauzito hupitia mabadiliko mbalimbali ya mwili na afya yake.

Inaelezwa mara zote mabadiliko hayo husababishwa na mtoto aliyetumboni, lakini pia, kuongezeka kwa homoni mwilini mwake.

Wataalamu wanasema mabadiliko hayo huyafanya maisha ya mjamzito kubadilika kuanzia kwenye mavazi, chakula, uwezo wa kutekeleza majukumu ya kila siku sambamba na namna ya kulala.

Kutokana na mabadiliko hayo, ndipo wataalamu wa afya huwashauri wajawazito mambo kadhaa waanze kuyazingatia ili mtoto aliyeko tumboni aweze kukua vizuri, lakini na mama aendelee kuwa na afya bora.
Mambo hayo ni pamoja na kuzingatia mlo kamili, unywaji wa maji ya kutosha, matumizi ya dawa za folic asidi pamoja na vitamin, kufanya mazoezi mepesi na mengineyo.

Lakini pia katika wakati huo kuna mambo mbalimbali ambayo mjamzito hushauriwa kuyaepuka, ikiwemo ulevi, uvutaji wa sigara, uvaaji wa nguo za kubana pamoja na kujiepusha kulalia mgongo, haswa katika kipindi ambacho ujauzito umefika miezi minne na kuendelea.

Inaelezwa kuwa mjamzito kuwa na mazoea ya kulalia mgongo, hasa mimba inapokuwa katika umri wa zaidi ya miezi mitatu, humuweka mtoto na mama katika hatari ya kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa nchini Ghana na Chuo Kikuu cha Michigan, wajawazito wanaopendelea kulalia mgongo wako kwenye hatari ya watoto kufariki kabla au wakati wa kuzaliwa mara tano zaidi.

Utafiti huu uliofanyika nchini Ghana, unaunga mkono utafiti wa hivi karibuni uliofanyika nchini Australia unaojulikana kama Sydney Stillbirth Study, uliosema wanawake wanaolala chali wakati wa ujauzito wako kwenye hatari mara sita zaidi ya kuzaa watoto wafu. Utafiti huu wa Australia ulifanyika kwa miaka mitano.


Wajawazito

Hilda Msami, ambaye kwa sasa ni mjamzito, mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, anasema kila anapojaribu kulalia mgongo huwa anahisi kuishiwa nguvu na kushindwa kupumua vizuri.

“Hivyo nikijaribu kulalia mgongo siwezi kulala, hata kwa dakika tatu,” amesema.

Magdalena Uswege, mkazi wa Kinondoni anasema huwa analalia mgongo pale anapohisi maumivu mgongoni, huweka mito kadhaa nyuma ya mgongo ili kutafuta nafuu.

“Nikilalalia mgongo bila ya kuweka mito nahisi kukosa pumzi, hivyo kushindwa kupumua vizuri,” anasema.

Naye Neema Kiswaga anasema ujauzito wake unapokuwa mkubwa huwa anaacha kulalia mgongo, hii inatokana na elimu anayopewa katika kituo cha afya anapokwenda kliniki kwenye mahudhurio ya kila mwezi.


Madaktari wafafanua

Akizungumza na Mwananchi, Daktari wa masuala ya uzazi, Cyril Massawe anasema mjamzito hapaswi kulala chali, hasa mimba inapokuwa na umri mkubwa kwa sababu kadiri mtoto anavyokua tumboni, uzito wake huongezeka na hata mfuko wa uzazi hutanuka kuelekea usawa wa kitovu.

Massawe anasema kutokana na kuongezeka kwa uzito, mjamzito akilalia mgongo husababisha mgandamizo mkubwa kwenye mishipa ya damu iliyopo katika mgongo.

Anasema mishipa hiyo hutoa damu kwenye moyo na kusambaza sehemu mbalimbali za mwili na mshipa mwingine hutoa damu sehemu za chini za mwili na kuirudisha kwenye moyo.

“Mjamzito anapolala chali mfuko wa uzazi hukandamiza hiyo mishipa ya damu, hivyo kupunguza uwezo wa kusafirisha damu katika maeneo mbalimbali ya mwili, ikiwemo kwenye mfuko wa uzazi,” anasema.

Pia anabainisha athari zinazoweza kutokea kwa mjamzito kutokana na damu kushindwa kusafirishwa vizuri kuwa ni pamoja na kuhisi kizunguzungu mara kwa mara, mapigo ya moyo kwenda mbio pamoja na kushuka zaidi kwa shinikizo la damu, hali inayomuweka mtoto na mama katika hatari.

Kwa upande wake Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daudi Gambo anasema kulalia mgongo pia kuna athari kubwa kwa mtoto aliye tumboni.

Anasema tabia hiyo huathiri usafirishaji wa damu katika mwili wa mjamzito kunakosababishwa na kukandamizwa kwa mishipa ya damu.
Anasema hali hiyo inaweza kumsababishia kushindwa kupata oksijeni ya kutosha.

Pia, anasema mtoto aliyeko tumboni hushindwa kupata virutubisho vya kutosha kutokana na damu kushindwa kufika ipasavyo katika plasenta, hivyo kumuweka mtoto katika hatari.

“Hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwa mama na mtoto aliye tumboni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa,” anasema.

Aliongeza kuwa mama kama anataka kuegemea mgongo kwa muda mfupi, anashauriwa kuweka mito ili ajiinue, hiyo itapunguza mgandamizo ambao ungekuwepo kama angelala kwa mgongo.


Namna sahihi ya kulala kwa mjamzito

Dk Gambo anasema mjamzito anatakiwa kulala kwa ubavu ili kuruhusu mwili kuendelea na shughuli zake kama ilivyo kawaida.
Anasema tafiti mbalimbali zinashauri mjamzito kulalia zaidi upande wa kushoto, kwa sababu damu husafirishwa kwa urahisi zaidi kutoka kwenye moyo wa mama na kwenda kwenye kondo la mtoto na kumpa virutubisho vingi zaidi.

“Mama anapolala ni vizuri akaweka mto katikati ya miguu, inasaidia kulala kwa uhuru na damu kusafirishwa vizuri na kutopata maumivu ya mgongo,” anasema.