Prime
Hantavirus ugonjwa unaotazamwa kwa tahadhari duniani
Muktasari:
- Hantavirus ni kundi la virusi vinavyosambazwa zaidi na panya na aina nyingine za jamii ya panya pori.
Katika siku za karibuni, dunia imeanza tena kugeukia habari za ugonjwa wa hantavirus baada ya kuzuka kwa maambukizi kwenye meli ya watalii iliyokuwa ikielekea Hispania.
Shirika la Afya Duniani ( WHO) limethibitisha kuwa watu kadhaa waliambukizwa huku baadhi yao wakipoteza maisha, jambo lililoibua hofu mpya kwa wasafiri na sekta ya afya duniani.
Lakini hantavirus ni ugonjwa gani hasa, unatoka wapi na kwa nini wataalamu wanaendelea kuutazama kwa jicho la tahadhari?
Kwa kifupi, hantavirus ni kundi la virusi vinavyosambazwa zaidi na panya na aina nyingine za jamii ya panya pori. Virusi hivi vinaweza kusababisha magonjwa makubwa yanayoathiri mapafu, figo na mfumo wa damu wa binadamu.
WHO inaeleza kuwa maambukizi mengi hutokea pale mtu anapovuta hewa yenye chembechembe kutoka kwenye mkojo, mate au kinyesi cha panya walioambukizwa.
Ugonjwa huu si mpya duniani. Historia inaonyesha kuwa hantavirus ilianza kutambulika kwa kiwango kikubwa wakati wa Vita vya Korea miaka ya 1950, ambapo wanajeshi wengi waliugua homa kali iliyokuwa ikiathiri figo. Baadaye, mwaka 1978, watafiti walifanikiwa kugundua virusi hivyo karibu na Mto Hantan nchini Korea Kusini ndipo jina “Hantavirus” likapatikana.
Ugonjwa unaokuja kimyakimya
Kinachoufanya hantavirus kuwa hatari ni namna dalili zake zinavyoanza kama mafua ya kawaida.
Mgonjwa anaweza kupata homa, maumivu ya misuli, kichwa kuuma, uchovu na wakati mwingine kutapika. Lakini ndani ya muda mfupi hali inaweza kubadilika na kuathiri mapafu au figo kwa kasi kubwa.
Katika bara la Amerika, virusi hivi husababisha ugonjwa unaojulikana kama Hantavirus Cardiopulmonary Syndrome, ambao huathiri mapafu na moyo.
WHO inasema ugonjwa huo unaweza kuua hadi nusu ya wagonjwa wanaoupata. Ulaya na Asia, wagonjwa wengi hupata aina inayoshambulia figo na mishipa ya damu.
Kwa mujibu wa WHO, duniani kote inakadiriwa kuwa watu kati ya elfu 10 hadi zaidi ya laki moja huambukizwa hantavirus kila mwaka, huku wagonjwa wengi wakiwa Asia na Ulaya.
Marekani imeripoti chini ya wagonjwa 1,000 tangu miaka ya 1990, lakini Amerika Kusini imekuwa na wagonjwa kila mwaka.
Wataalamu wa afya wanasema mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa makazi karibu na maeneo yenye panya pamoja na safari za kimataifa vinaongeza uwezekano wa maambukizi.
Meli ya watalii yazua taharuki
Hivi karibuni, WHO ilitoa taarifa kuhusu mlipuko wa hantavirus uliotokea kwenye meli ya watalii iliyokuwa ikisafiri kuelekea visiwa vya Canary nchini Hispania.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa zaidi ya watu saba walihusishwa na maambukizi hayo huku watu watatu wakifariki dunia.
Ripoti mbalimbali zilisema wagonjwa hao walionyesha dalili za homa kali, matatizo ya kupumua na mshtuko wa mwili kabla ya baadhi yao kupoteza maisha.
Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha maambukizi hayo, ingawa wataalamu wanaamini panya waliokuwa kwenye mazingira ya safari hiyo wanaweza kuwa chanzo.
Kilichozua mjadala mkubwa ni taarifa kuwa aina ya 'Andes hantavirus' inayohusishwa na mlipuko huo, inaweza kusambaa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine, jambo ambalo si la kawaida kwa hantavirus nyingi.
WHO imesisitiza kuwa maambukizi ya aina hiyo hutokea kwa nadra sana na huhitaji ukaribu mkubwa kati ya watu.
Mtaalamu mmoja wa magonjwa ya kuambukiza alinukuliwa na dhirika la habari la Reuters akisema, “Hii si Covid mpya, lakini ni tukio linalohitaji umakini mkubwa kwa sababu mazingira ya meli yanaweza kurahisisha maambukizi.”
WHO pia imesema hatari kwa umma wa dunia kwa sasa bado ipo chini, lakini shirika hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa.
"Tunaamini huu utakuwa mlipuko mdogo ikiwa hatua za afya ya umma zitatekelezwa na mshikamano utaonyeshwa kati ya nchi zote,” anasema mkurugenzi wa WHO anayehusika na tahadhari na mwitikio wa dharura, Abdi Rahman Mahamud kama alivyonukuliwa na shirika la habari la DW.
Je, kuna dawa au chanjo?
Hadi sasa hakuna chanjo rasmi wala dawa maalumu ya kutibu hantavirus. WHO inaeleza kuwa matibabu yanayopatikana ni ya kusaidia mwili kupambana na madhara ya ugonjwa huo, ikiwemo kusaidia mgonjwa kupumua vizuri na kufuatilia kazi za moyo na figo.
Madaktari wanasema wagonjwa wanaowahi hospitali mapema wana nafasi kubwa zaidi ya kupona kuliko wanaochelewa kupata matibabu.
Kutokana na kukosekana kwa chanjo, njia kuu ya kujikinga ni kudhibiti mazingira yanayoweza kuwa na panya. WHO inapendekeza watu kufunga mianya kwenye nyumba, kuhifadhi chakula vizuri na kuhakikisha maeneo yenye kinyesi au mkojo wa panya yanasafishwa kwa uangalifu mkubwa.
Badala ya kufagia sehemu yenye kinyesi cha panya kwa ufagio mkavu, wataalamu wanashauri kutumia dawa ya kuua vijidudu au maji kwanza ili kuzuia chembechembe kuruka hewani.
Wafanyakazi wa mashambani, migodini, maghala na maeneo ya misitu wanatajwa kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi.
Tahadhari bado ni muhimu
Ingawa hantavirus si ugonjwa unaosambaa kwa kasi kama mafua au Uviko-19, wataalamu wa afya wanaonya kuwa dunia haipaswi kupuuza magonjwa yanayotoka kwa wanyama.
WHO inasema uzoefu wa miaka ya karibuni umeonyesha kuwa magonjwa mengi mapya huanzia kwa wanyama kabla ya kuingia kwa binadamu.
Ndiyo maana shirika hilo linaendelea kusisitiza mfumo wa “One Health” unaounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Kwa sasa, jambo kubwa linaloshauriwa ni wananchi kuwa makini na usafi wa mazingira na kuepuka kugusa au kuvuta hewa kwenye maeneo yenye panya bila tahadhari.
Kwa wengi, hantavirus inaweza kuonekana kama ugonjwa wa mbali usio na madhara makubwa. Lakini historia ya milipuko ya magonjwa duniani inaonyesha kuwa tahadhari ya mapema ndiyo kinga bora zaidi kuliko kusubiri janga litokee.
Makala haya kwa hisani ya mitandao