Asimulia huduma ya dharura ilivyookoa maisha ya mwanaye aliyechinjwa

Muktasari:
- Wakati dunia ikiadhimisha siku ya magonjwa ya dharura, vifo milioni 37.8 hutokea kila mwaka kutokana na kukosa huduma za dharura kwa wenye magonjwa ya ajali, kiharusi na magonjwa ya mshtuko wa moyo.
Dar es Salaam. “Nilikata tamaa. Mwili wa mtoto wangu ulipoteza mawasiliano ya upumuaji kati ya mdomo, pua na koo kushuka chini kwenye kiwiliwili, baada ya kukatwa koromeo lake.”
Dakika chache zinaweza kuamua maisha ya mtu, uhai au kifo. Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya simulizi hiyo ya Mkazi wa Goba Kinzudi jijini Dar es Salaam, Shani Charles aliyeshuhudia huduma aliyopewa mtoto wake Malik, aliyekatwa koromeo na kupona.
Malik (7) ni miongoni mwa wagonjwa 250 wanaofikishwa katika Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kila siku, wakiwa wamepata majanga mbalimbali ikiwemo ajali, mshtuko wa moyo, kiharusi, magonjwa ya figo, kuangukiwa na ghorofa na mengineyo.

Mtoto wa Shani alipokewa katika kitengo cha dharura Julai 15, 2024 baada ya kukatwa koromeo na kitu chenye ncha kali na mtumishi wao wa ndani, hali iliyomfanya asote hospitalini hapo kwa siku 107 akitibiwa koo.
Akizungumza leo Jumanne, Mei 27, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya magonjwa ya dharura duniani, Shani amesema alipokea taarifa kuwa mtoto wake amekatwa na kisu shingoni, hali iliyompa mshtuko na kwenda nyumbani haraka.
“Nilifika na kukuta eneo la tukio limetapakaa damu, nilimchukua mtoto na kupanda bodaboda haraka mpaka kituo cha afya, kufika wakanipeleka Muhimbili.
“Tulifikia huduma za dharura ilikuwa usiku sana, walipambana mpaka saa 9 usiku kuhakikisha mwanangu anakaa sawa, nakumbuka Dk Juma na Dk Said walitusaidia sana,” amesema Shani.
Ameeleza kuwa mtoto alikuwa akihema hewa inatoka kupitia kwenye koo, akipumua inakuja kwenye koo na kadri alivyokuwa anapumua hewa ilikuwa inatoka ikiwa imeambatana na damu.
“Hofu yangu damu ilikuwa haikati. Walimpa huduma nzuri na mpaka anatoka chumba cha upasuaji na kupelekwa wodini ICU tulipata matumaini damu ilikata, tulipewa huduma bila kujali tuna pesa au hatuna,” amesema Shani.
Akisimulia zaidi amesema walikata tamaa kwani hakukuwa na mawasiliano kati ya mdomo, pua na koo kushuka chini kwenye kiwiliwili.
“Tunamshukuru Profesa Janabi (Mohamed) alikuwa anahakikisha kila siku ametuona. Mwanangu sasa ni mzima, anacheza, ufahamu uko vizuri nashkuru sauti yake iko vizuri anaongea na kupiga kelele kama hakuna chochote kilichowahi kutokea,” amesimulia Shani.

Kwa upande wa Malick ametoa shukrani zake, “Nawashkuru madaktari na wauguzi kwa kunisaidia na kuokoa maisha yangu, asanteni sana kwa kujitoa na kunisaidia.”
Utafiti uliofanyika Hospitali ya Muhimbili unaonyesha uwepo wa kitengo cha dharura hospitalini hapo ilisaidia kuokoa maisha kwa wagonjwa kwa asilimia 40.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili - Mloganzila, Dk Julieth Magandi amesema matokeo chanya kwa wagonjwa waliotibiwa katika kitengo cha dharura Muhimbili, utafiti ulionyesha kwamba kitengo kimeweza kupunguza vio vya magonjwa yaliyotokana na dharura kwa asilimia 40.
“Baada ya kuona Muhimbili imefanikiwa katika hili, Serikali ikaona ichukue Muhimbli kama mfano na kujenga kujenga majengo ya dharura ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa katika hospitali za mikoa yote na wilaya zilizopo nchini,” amesema Dk Magandi.
Mkuu wa Idara ya Dharura Muhimbili, Dk Juma Mfinanga amesema idara hiyo kwa siku inapokea wagonjwa 200 mpaka 250 na wote wanahitaji kupewa huduma za haraka.
“Kutokana na uwezo mzuri wa mafunzo tuliyopewa wote hawa tunawamudu, lengo kubwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anayehitaji huduma za dharura lazima apewe, afya ndiyo kipaumbele chetu,” amesema.
Dk Mfinanga ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya dharura, amesema walianza huduma hiyo mwaka 2010 ikiwa idara moja pekee nchini na mpaka sasa wana miaka 15, kukiwa na mafanikio ya kutumika kama kituo cha kusomesha wataalamu wengi na kuwezesha ujenzi wa vituo zaidi ya 100 nchi nzima.
“Kazi yetu kubwa Muhimbili tukishirikiana na Muhas tunafundisha njia sahihi kutoa huduma za dharura pia tunafundisha wale wanaokuja hospitalini wanatakiwa waanzie nyumbani kumpa mgonjwa huduma.”
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonyesha zikiunganishwa huduma bora ya kabla ya kufika kituoni na hospitalini, hupunguza uwezekano wa kifo kwa mgonjwa kwa asilimia 50.
Vifo milioni 37.8 hutokea kutokana na kukosa dharura ikiwemo ajali, kiharusi na magonjwa ya mshtuko wa moyo.