Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo kuhamasisha wanaume kupima saratani ya matiti

Muktasari:

  • ACT Wazalendo inaungana na wanawake wote duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, Machi 8, 2025 ikifanya kongamano jijini Dar es Salaam litakaloongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dorothy Semu.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amejitolea kuwa balozi wa kuhamasisha wanaume kupima saratani ya matiti.

Mbali na hilo, ameomba Serikali kuhakikisha katika kila zahanati, kituo cha afya kuna huduma ya uangalizi wa awali wa kupima viashiria vya saratani ya matiti na ya mlango wa shingo ya kizazi.

“Tukihamasisha tu watu wapime bila huduma hizi kupatikana ngazi za chini ni kazi bure, zinapaswa kuwepo kuanzia kwenye zahanati na vituo vya afya,” amesema Shaibu.

Shaibu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika wiki ya maadhimisho ya ngome ya wanawake wa chama hicho leo Machi 6, 2025 kuelekea kwenye Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 8, 2025, amesema wanaume wanahitaji elimu kuhusu saratani ya matiti.

“Wengi huwa tunafahamu wanawake pekee ndiyo wanapata saratani ya matiti, lakini kupitia maadhimisho haya nimepata elimu kwamba hata wanaume wanapata saratani ya matiti.

“Asilimia moja ya wanaopata saratani ya matiti ni wanaume, hivyo kuna haja ya wanaume kulifahamu hili, leo najitolea kuwa balozi kwa kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na kuwahamasisha wanaume wengine pia kufanya,” amesema.

Katika maadhimisho hayo, Shaibu alitembelea pia baadhi ya mabanda, ikiwamo la damu salama na la wanawake wajasiriamali.

Amesema amepata nafasi ya kuwasikiliza wanawake wajasiriamali ambao kilio chao ni kilekile cha masoko na mitaji.

“Hili la mitaji, Serikali inatakiwa ilichunguze kwenye utoaji wa ile mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri na pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

“Watu wa damu salama, pia, wamenieleza kuhusu uhitaji wa damu, kuna mahitaji kwa watu wanaopata ajali, kina mama zetu wanaojifungua na watu wengine, ACT Wazalendo tunalifanya hili kwa vitendo kuhamasisha watu kuchangia damu,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake Taifa, Janeth Rithe amesema wanaiadhimisha siku ya wanawake kipekee kwa kufanya vitu tofauti ikiwemo kutoa elimu na kuhamasisha kupima saratani ya matiti na mlango wa kizazi.

“Tumewahamasisha wanawake kupimwa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti, pia tumehamasisha uchangiaji damu na wanawake wajasiriamali wamepata fursa ya kuonyesha bidhaa zao na kuziuza.

“Vilevile, tumetoa elimu ya ujasiriamali ambayo leo imefanywa na mtaalamu mkufunzi wa ujasiriamali, baada ya hapa tutakwenda kutoa elimu hii chini kuanzia ngazi ya kata kwa lengo la kuwapa fursa wanawake, kujifunza na kujikwamua kiuchumi,” amesema akisisitiza kwamba ACT Wazalendo inafanya vitu vya kushikika na sio kutoa matamko.