Zimebaki siku 18 mgawo wa umeme uwe historia

Muktasari:
- Mgawo wa umeme ulianza Septemba 2023 huku sababu ikielezwa kwamba upungufu wa maji kwenye vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo. Hadi sasa maeneo mbalimbali ya nchi yanakabiliwa na kukatika kwa umeme, hata hivyo Serikali imeahidi kwamba mgawo utakwisha Machi 2024.
Dar es Salaam. Zimebaki siku 18 mgawo wa umeme iwe historia! Ndivyo unaweza kusema baada ya kauli ya matumaini ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kuwa ifikapo katikati ya Machi 2024 hakutakuwa na kadhia hiyo tena nchini.
Dk Biteko amebainisha hayo leo Februari 25, 2024 alipotembelea mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) sambamba na kuwasha mtambo namba tisa, akieleza kufikia katikati ya Machi, mwaka huu nchi itakuwa na ziada ya megawati 70 za umeme.
Kauli hiyo ya Dk Diteko imekuja baada ya kuwashwa kwa mtambo namba tisa kwenye bwawa hilo ambao umeingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa ambazo zinatajwa kupunguza makali ya mgawo wa umeme nchini.
Amesema Machi 2024, mtambo namba nane utakamilika na kuzalisha megawati nyingine 235 ambazo zitafanya kuwa na umeme wa ziada ya megawati 70 na kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea.
“Katika mitambo hii miwili, namba tisa na nane tutakuwa na megawati 470, ukichukua upungufu tuliona wa megawati 200 mpaka 400 maana yake ni kwamba tutakuwa na ziada ya megawati 70,” amesema Dk Biteko.
Mtambo namba nane unatarajiwa kuwashwa Machi na hafla ya uzinduzi wa mitambo yote miwili (namba tisa na nane) itafanyika mwezi huo ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi pia amealikwa.
Wakati Dk Biteko akieleza hayo, mkandarasi wa mradi huo, Meadows, Mohamed Zaky amefichua namna alivyokuwa akipewa msukumo na Serikali ili ukamilike mapema ujenzi huo nje ya muda waliokubaliana.
“Tulipaswa kukamilisha Juni (2024), lakini mradi huu umekamili hivi sasa kutokana na msukumo tuliokuwa tukiupata kwa Dk Biteko, simu zilikuwa ni nyingi mara kwa mara wakitusisitiza kuumaliza mapema na tumefanikiwa,” amesema mkandarasi huyo.
Dk Biteko katika ziara ya kutembelea bwawa hilo, amesema walichokuwa wanakihitaji ni Watanzania ni kupata umeme ili kuondokana na mgawo.
“Huo ndio ulikuwa mkakati wa Rais Samia, tunamshukuru mkandarasi tulipomwambia kukamilisha mradi huu mapema, alifanya kazi usiku na mchana na leo hii tumeingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa,” amesema.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema megawati 235 zilizoingizwa kwenye gridi ya Taifa baada ya mtambo namba tisa kuwashwa zimepunguza makali ya mgawo na kwenye baadhi ya mikoa umekwisha kabisa.
“Huko majumbani, kuna maeneo hakuna mgawo tena, mwezi ujao tutaingiza umeme wa mtambo namba nane, kisha namba saba utafuata ambao nao uko kwenye hatua nzuri, tutazungumza na mkandarasi kujua namba saba itakuwa ni lini, lakini hadi kufikia Desemba mitambo yote tisa itakuwa imewashwa,” amesema.
Katibu Mkuu huyo pia amebainisha kuendelea kuwatumia kwenye miradi mingine mbalimbali vijana wazawa 10,000 waliofanya kazi kwenye bwawa la Nyerere.
Amesema katika ujenzi wa bwawa hilo, asilimia kubwa waliwatumia wazawa ambao wamewapa vyeti maalumu na wataendelea kuwatumia katika miradi mbalimbali inayoendelea nchini.
“Tulifanya kazi na Veta, wakawatathmini na kuwapa vyetu maalumu vya utambuzi vijana hawa wazawa ambao mbali na hapa tutaendelea kuwatumia kwenye miradi mingine,” amesema katibu mkuu huyo.
Akizungumzia ongezeko la maji, ambalo awali ilielezwa kupungua kuwa ndiyo chanzo cha kupungua kwa umeme nchini, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema yapo ya kutosha kwenye mabwawa yakufua umeme ya Kihansi na Kidatu huku la Julius Nyerere likibakiza mita 4 kujaa.
Amesema, bwawa la Nyerere linalohitaji lita za ujazo bilioni 32.7 hivi sasa, maji yaliyoingia yamefika lita za ujazo bilioni 28.
Mgawo wa umeme nchini Tanzania ulianza Septemba, 2023 kutokana na upungufu kwa uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo vya maji.
Septemba 25, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), GIssima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini.
Miezi sita aliyopewa na Rais Samia kuhakikisha mgawo wa umeme nchini inakwisha Machi 25, 2024.
Septemba 28, 2023, Nyamo-Hanga amesema changamoto ya umeme inayoendelea nchini hadi kufikia Machi mwaka huu itakuwa imekwisha.
Februari 6, 2024, Bunge liliazimia Serikali ihakikishe mradi wa JNHPP unakamilika haraka na kuanza uzalishaji kuanzia Februari 2024 kama ilivyoahidi.