Moshi. Inawezekana. Hilo ndilo neno sahihi linaloweza kutumika kuelezea namna wanawake wanavyoweza kufanya mambo makubwa endapo watapewa nafasi katika vyombo vya maamuzi kama ilivyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ambaye alichukua uongozi wa juu wa nchi Machi 19, 2021 kurithi mikoba ya Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, ni kielelezo cha wanawake wengi ndani na nje ya nchi, walioonyesha kiwango cha juu cha uchapa kazi.
Wakati dunia leo ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kwa Tanzania Rais Samia anatazamwa kama mwanamke wa mfano na kutoa hamasa kwa wanawake wengine kupigania haki ya kuingia katika vyombo vya juu vya maamuzi, sawa na ilivyo kwa wanaume.
Chachu ya nafasi za uongozi kuwa 50/50 ilianzia katika azimio la Beijing nchini China mwaka 1995 ndilo lililofungua zama mpya ya kusaka usawa wa kijinsia na ni kupitia kongamano hilo, sheria katika nchi nyingi duniani zilifanyiwa marekebisho.
Huwezi kuzungumzia mafanikio kwenye harakati za ukombozi wa wanawake na watoto wa kile nchini bila kumtaja, Mama Gertrude Mongella, aliyeongoza harakati wa Beijing na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika.
Mwaka 1993-95, Mongella alikuwa katibu mkuu wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake na kuhudhuria mkutano wake wa nne uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.
Kwa maneno mengine, Mama Mongella ndiye aliyewaongoza wanawake wenzake wa Tanzania kwenye mkutano huo, uliojadili masuala ya msingi ikiwemo kupinga na kupambana na ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, Februari 2022, mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF), Anna Kulaya alisema lengo hilo la Beijing litafanikiwa endapo wanawake watapata nafasi nyingi zaidi za uongozi kwenye vyombo vya uamuzi.
Suala hilo kwa sasa si miujiza tena, linawezekana kwa kuwa ipo nyota inayowaangazia (Rais Samia) kuelekea kwenye mafanikio.
Samia ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za makamu wa Rais na baadaye Rais, pia anasifika kwa namna alivyoendesha Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014 akiwa makamu mwenyekiti chini ya Samuel Sitta.
Nafasi nyingine alizowahi kushika ndani ya Serikali ni pamoja na Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira (2010-2015) na Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (2005-2010).
Mbali na Rais Samia, kwa Tanzania wapo wanawake wengine wanaoshikilia na waliowahi kushikilia nyadhifa za juu ndani na nje na kuwa kielelezo cha mwanamke katika uongozi na popote unapotaja kielelezo cha mwanamke huwezi kuacha kuwataja.
Katika Bara la Afrika, Rais Samia anaingia katika orodha ya viongozi wanawake ambao ni Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde, Ameeneh Gurib-Fakim aliyewahi kuwa Rais wa Mauritius (2015-2018) na Joyce Banda, Rais wa Malawi (2012-2014)
Wengine ni Dk Ackson Tulia ambaye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioukwaa uspika 2022 na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 jijini Luanda nchini Angola.
Dk Tulia aliwashinda wapinzani wake Adji Diarra Mergane Kanouté kutoka Senegal, Catherine Gotani Hara kutoka Malawi na Marwa Abdibashir Hagi kutoka Somalia, wote wakiweka historia ya kuwa wabunge wanawake kutoka Afrika.
Tulia Ackson anakuwa mwanamke wa tatu kuongoza IPU baada ya Najma Heptulla wa India (1999–2002) na Gabriela Cuevas wa Mexico (2017–2020), lakni anakuwa wa kwanza kutoka Afrika kushika nafasi hiyo.
Kabla ya nyadhifa hizo, nyota ya Dk Tulia ilianzia akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na mbunge wa Mbeya Mjini.
Mama Mongella akizungumza na gazeti hili jana juu ya siku ya leo alisema, “mimi nafurahi…mimi niliona siku nyingi kuwa inawezekana mwanamke akashika nafasi yoyote na ndiyo maana nikafanya vurugu zote duniani kuonesha kuwa tunaweza.”
Alisema “kuna mifano mingi tu ya wanawake wanaofanya vizuri, sikuwa na mashaka nayo tangu nizaliwe, nilimwona mama yangu anavyopambana.”
Hata hivyo, Mama Mongella alisema wanawake waliopo ngazi za chini (wasiokuwa viongozi) , “wapo imara zaidi na sijapata kuona, wanajua majukumu yao, wanajua kusimamia familia zao, wanaweza katika ujasirimali.”
“Walioko chini ni imara zaidi kuliko hata wa juu. Kati ya wanawake ninaowasifu ni wanawake wa chini, sisi wa juu tunafaidi, huko chini wako shamba na juani, utamchezea huyo mama, kwa hiyo wa chini ni imara zaidi,” alisema Mama Mongella.
Wanawake wengine wanaotajwa kama kielelezo cha wanawake katika uongozi ni waliomo kwenye vyombo vya ulinzi akina Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda anayeshikilia wadhifa wa Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi, moja ya chombo kikubwa nchini.
Mwingine ambaye anatajwa kuwa kielelezo ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania (CGI) Dk Anna Makakala, Ofisa Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, na kiongozi mpya wa chama cha siasa cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu.
Wadhifa wa Kaganda aliyeteuliwa Oktoba 24, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan, ni nafasi juu kuwahi kushikwa na mwanamke ndani ya Jeshi la Polisi, sawa na Makakala ambaye ni Kamishna wa Jeshi la Uhamiaji, wadhifa mwingine wa juu kuwahi kushikwa na mwanamke.
Dk Makakala amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa takriban miaka minane sasa tangu alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli Februari 10, 2017.
Yupo pia Dk Stargomena Tax aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Waziri wa kwanza mwanamke wa Ulinzi.
Hao ni baadhi tu ya wanawake waliopo kwenye nyadhifa za juu kwa sasa, lakini wapo pia waliowahi kushika nafasi nzito kimataifa kama Dk Asha-Rose Migiro aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na Profesa Anna Tibaijuka aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) na baadaye msaidizi wa katibu mkuu (under secretary) na wengine wengi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna ni mwanamke mwingine anayesimama kama kielelezo cha wanawake waliofanikiwa katika utendaji.
Kinachomfanya awe mfano wa kuigwa ni hatua yake ya kuwa mmoja wa wanawake waliowahi kuongoza taasisi za kifedha na benki anayoiongoza ikifanya vyema chini ya utawala wake.
Ruth aliteuliwa kuiongoza benki hiyo Agosti 18, 2020 wakati bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo ikiwa chini ya Dk Edwin Mhede.
Katika kipindi ambacho nafasi za wanawake zinamulikwa kwa tochi kwenye nafasi za juu za vyama vya siasa, Dorothy Semu amechaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama (KC) cha ACT-Wazalendo.
Hii ndiyo nafasi ya juu katika chama hicho akiwa wa pili baada ya Zitto Kabwe kung’atuka.
Ndani ya chama, Dorothy amekuwa katibu mkuu (2017 – 2020), makamu mwenyekiti Bara (2020 – 2024) na aliwahi kukaimu nafasi ya mwenyekiti kwa mwaka mmoja baada ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.
Tanzania pia ina utajiri wa kuwa na rubani mwanamke , Kapteni Neema Swai, akiwa ni yeye pekee aliyefikia cheo cha rubani kiongozi ambaye hadi Juni 2023 alikuwa amerusha ndege kwa zaidi ya saa 8,700.
Huyu ndiye alirusha ndege kubwa ya mizigo aina ya Boeing 767-300F kutoka Seattle, Marekani hadi Dar es Salaam, Tanzania, umbali wa maili 9,432.
Mwanamke huyo (34), alisema wanawake wana uwezo kama wanaume katika kufanya kazi, hivyo aliihamasisha jamii kuwasomesha watoto wa kike na kuwajengea uwezo kwa kuwasaidia kufika wanapotaka, kama yeye alivyosaidiwa na wazazi wake.
Miongoni mwa wanawake mashujaa nchini huwezi kuacha kumtaja Mariam Mwakabungu (26) mwenye simulizi tofauti, ya siku hii adhimu.
Mariam alijipatia umaarufu Julai mwaka jana, baada ya kuokoa maisha ya vichanga kadhaa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, Dar es Salaam. Hivi sasa ana ajira rasmi katika chumba cha watoto wachanga hospitalini hapo.
Julai 18, Mwananchi liliripoti habari kuhusu Mariam, ambaye kwa wakati huo alijitolea kukumbatia watoto njiti aliowakuta wametekelezwa na mama zao hospitalini hapo, alipokwenda kumtembelea rafiki yake aliyejifungua mtoto kabla ya wakati.
Mariam anaikumbuka Machi mwaka jana, yenye tofauti kubwa na mwaka huu, akisema moyo wa huruma, kujitoa na kufanya kitu cha tofauti kama mwanamke imemweka alipo sasa.
“Nakumbuka Machi mwaka jana nilikuwa nyumbani tu, wakati huo niliendelea na biashara ndogondogo za kukopesha kinamama chupi, sidiria na madera. Biashara niliyoifanya miaka mingi, lakini Machi mwaka huu nasherehekea tofauti kama mwanamke jasiri.
“Namshukuru Mungu mwaka huu amenifikisha salama na ninafanya hii huduma ya kukumbatia watoto si wale waliotelekezwa pekee, sasa hivi nawasaidia watoto wa kinamama ambao wamefariki au wanaoumwa ambao hawawezi kuhudumia watoto wenyewe pale Amana.”
Mariam anasema simulizi yake itumike kuhamasisha wanawake wenzake popote wanapoishi na kwenye mazingira yanayowazunguka, wanapokuta kitu ambacho wanaweza kujitolea wafanye hivyo kuleta mabadiliko kwenye jamii.
Anasema wanawake wameumbwa na moyo wa ujasiri na wanaweza.
“Mungu ametupa moyo wa ujasiri sana na wa huruma, kwa hiyo tukijitahidi kufanya hivyo pia Mungu anazidi kutusaidia,” anasema.
Samia kuwakumbuka wengine
Wakati wanawake hao wanatajwa kwa mafanikio hayo, wengine wengi leo wanatambuliwa na kupewa tuzo kama waajiri wenye sera imara au programu maalumu zinazolenga kuwainua wanawake kufikia malengo yao kwenye kampuni mbalimbali pamoja na waajiri wenye wanawake wengi kweny nafasi za juu za uongozi, maarufu kama The Citizen Rising Woman.
Katika kutambua mchango wao, Rais Samia leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi hafla ya utoaji tuzo za msimu wa nne wa zinazofanyika katika ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam.
Rais Samia pia anatarajiwa kushiriki mahojiano ya ana kwa ana kuhusu mchango wa Serikali katika kuwezesha wanawake kwenye uongozi wa nyanja mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Victor Mushi, utoaji wa tuzo hizo zilizoanza kuratibiwa na Kampuni ya MCL mwaka 2021, utaambatana na matukio mbalimbali yatakayohanikiza maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani.
Tangu kuanza kwa mradi wa The Citizen Rising Woman, mpaka sasa gazeti la The Citizen limeshachapisha makala za wanawake viongozi 217 kutoka sekta mbalimbali na msimu huu unaoisha una jumla ya makala za wanawake 240.
Hafla hiyo itakayoambatana na utoaji wa mada mbalimbali, itahusisha mada nne zitakazotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Grobal Compact Nertwork Tanzania, Marsha Macatta, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serengeti, Dk Obinna Anyalebechi, Mwanzilishi mwenza wa Empower, Miranda Naiman na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji, Dk Anna Makakala.
Mchokoza mada atakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi.