Wizi mitandaoni bado tatizo

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi akijibu maswali ya wabunge leo Jumatatu Mei 12,2025 bungeni jijini Doodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Kwa mujibu wa takwimu za TCRA za robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25, idadi ya laini za simu nchini Tanzania zimefikia milioni 90.4 na utumiaji wa intaneti umefikia milioni 49.3, Bunge limeelezwa.
Dodoma. Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, amesema ukuaji wa teknolojia umekuja na fursa na changamoto zake, ikiwamo wizi wa mitandaoni ukihusisha Simbanking.
Mahundi amebainisha hayo leo Mei 12, 2025 bungeni Dodoma akieleza kwamba watumiaji wa huduma za mawasiliano wamekuwa wakifanyiwa hadaa na kujikuta wametapeliwa fedha zao mtandaoni.
Kwa mujibu wa takwimu za TCRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) za robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25, idadi ya laini za simu nchini Tanzania zimefikia milioni 90.4 na utumiaji wa intaneti umefikia milioni 49.3, Bunge limeelezwa.
Mahundi alikuwa akijibu swali la Fakharia Shomari Khamisi ambaye ameuliza; ni lini Serikali itakomesha wizi wa mtandao kupitia Simbanking na ni wahalifu wangapi wamekamatwa na hatua gani zimechukuliwa?
Mbunge huyo ameuliza ni lini Serikali itaweka hadharani adhabu na orodha ya wanaofanya uhalifu huo.
Naibu Waziri amesema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imeendelea kukua kwa kasi hapa nchini na duniani kwa ujumla na kusababisha kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Miongoni mwa maeneo yaliyofaidika ni pamoja na huduma za fedha.
“Katika kukabiliana na changamoto hizi, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa mawasiliano nchini imeendelea kuelimisha umma kuhusiana na masuala mbalimbali ya usalama mtandao kwa kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo ya SITAPELIKI, NIRAHISI SANA,” amesema Mahundi.
Kwa mujibu wa Mahundi, ili kupambana na mambo hayo ni kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu namna bora na salama ya kutumia mitandao ikiwemo utunzaji wa nywila, kuwa na nywila imara.
Amesema kwa upande mwingine Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kujiimarisha katika aina hizi mbaya za uhalifu na tayari hatua, mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa wahalifu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko amesema kuna kilio kikubwa cha Watanzania katika wizi wa mitandao unaosababishwa na usajili holela wa laini za simu.