Wizara Mambo ya Ndani kuajiri 7,666, yaja na vipaumbele vitano

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa akiungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma leo Mei 26, 2025.
Muktasari:
- Katika bajeti hiyo iliyopitishwa na Bunge, zimetengwa fedha ili kutoa ajira kwa watumishi 7,666 katika vikosi mbalimbali vilivyo chini ya wizara hiyo huku ikilenga kuboresha na kujiimarisha kwenye utendaji kazi
Dodoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeomba Sh2.06 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 zitakazotekeleza vipaumbele vitano ikiwa ni ongezeko la Sh1.71 trilioni sawa na asilimia 120.
Katika bajeti hiyo iliyopitishwa na Bunge, zimetengwa fedha ili kutoa ajira kwa watumishi 7,666 katika vikosi mbalimbali vilivyo chini ya wizara hiyo huku ikilenga kuboresha na kujiimarisha kwenye utendaji kazi.
Mgawanyo wa ajira hizo umeelezwa kuwa, watumishi 56 watakwenda Makao Makuu ya Wizara, Jeshi la Polisi litaajiri watumishi 5,237, Magereza (766) huku Zimamoto na Uokoaji wataajiriwa 1,000.
Pia, makadirio hayo yanaonesha kwa upande wa Uhamiaji imetengewa nafasi 457 wakati Mamlaka ya Vitambulisho (Nida) ikitengewa nafasi 150.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni leo Jumatatu Mei 26, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema kati ya fedha hizo, Sh701.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi mengine huku Sh950.31 bilioni ni kwa ajili ya mishahara na Sh415.1 bilioni ni za miradi ya maendeleo.
“Katika fedha za maendeleo Sh388.6, ni fedha za ndani na Sh26.5 ni fedha za nje,” amesema.
Waziri Bashungwa amevitaja vipaumbele katika bajeti hiyo ni kuendelea kudumisha usalama wa raia na mali zao.
Amesema wizara itatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Tume ya Haki Jinai, kuboresha na kujenga miundombinu ya ofisi na makazi ya maofisa, wakaguzi na askari.
“Vipaumbele vingine ni kuimarisha na kuboresha huduma za uhamiaji mtandao na kuanza zoezi la usajili na utambuzi wa watu chini ya umri wa miaka 18,” amesema.
Kwenye bajeti bajeti hiyo, pia zimetengwa Sh34.88 bilioni zitakazowezesha mafunzo kwa watumishi 30,879.
Amesema kati ya hao, watumishi 138 ni wa Makao Makuu ya Wizara na 22,500 ni wa Jeshi la Polisi huku watumishi 3,241 ni wa Jeshi la Magereza na 2,347 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, 2,611 wa Idara ya Uhamiaji na wengine 42 wa Nida watapewa mafunzo.
“Mheshimiwa Naibu Spika, Jumla ya Sh2.04 bilioni zimetengwa kwa mwaka 2025/26 ili kuwezesha upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, vituo na makazi kwa maofisa, wakaguzi na askari, ambapo kati ya fedha hizo Sh532.45 milioni ni za Jeshi la Polisi,” amesema Bashungwa.
Waziri huyo amesema Sh795.76 milioni zimepangiwa Jeshi la Magereza, Sh600 milioni ni za Zimamoto na Uokoaji na Sh120 milioni za Idara ya Uhamiaji.
Waziri ametaja pia mkakati wa kupambana na uhalifu wa kifedha na kuondoa changamoto hiyo kwa wananchi.
Amesema wizara imetenga Sh2.3 bilioni kwa ajili ya kugharamia upatikanaji wa taarifa za upelelezi za uhalifu wa kifedha, ikiwamo kuwajengea uwezo watendaji waliopo Kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu wa Kifedha (FCU) na kuimarisha ushirikiano na wadau, katika matumizi ya vifaa vya kisasa.
Kwenye mkakati huo, Waziri Bashungwa amesema wizara imetenga Sh30 bilioni kwa ajili ya mafunzo kwa watendaji ikiwamo kutoa elimu ya jinsi kushughulikia ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa wanawake na watoto.
Amesema pia kwa mwaka wa fedha 2025/26, wizara itaratibu na kufuatilia wafungwa 5,500 wanaolengwa kuwekwa chini ya Sheria ya Huduma za Jamii, Sura ya 291 na Sheria ya Kifungo cha Nje.

Kuhusu udhibiti wa wahamiaji haramu, amesema Serikali imeelekeza Sh69.08 bilioni zitengwe na wizara kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mifumo ya Uhamiaji Mtandao kwa kuisimika katika maeneo ambayo hayana.
Maoni ya Kamati
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa amesema wizara hiyo inapaswa kuweka utaratibu mzuri na unaotekelezeka kwa kuanza maandalizi ya awali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema kamati pia imeitaka Serikali iendelee kuboresha hali ya vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa majeshi yaliyoko chini ya wizara hiyo ili kuboresha utendaji kazi wao katika kukabiliana na uhalifu pamoja na majanga yanayoweza kutokea nchini.
“Serikali iendelee na mkakati wa kuboresha vifaa na vitendea kazi kwa majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kwani kufanya hivyo kutaongeza ufanisi wa kazi na kusaidia kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli,” amesema Kawawa.
Aidha, licha ya jitihada zilizofanyika katika kipindi cha miaka minne iliyopita ya kuongeza ajira kwa majeshi hayo, Kawawa amesema Serikali inapaswa kuendelea kuajiri zaidi kwa lengo la kuongeza askari watakaoimarisha utendaji kazi sambamba na kuwahudumia wananchi.
“Lakini hili liende sambamba na ongezeko la mahitaji kutokana na ukuaji wa makazi na shughuli za kiuchumi,” amesema mwenyekiti huyo.
Amesema kamati pia imetoa ushauri kuhusu maendeleo ya teknolojia, ikibainisha kukua kwa teknolojia kunachangia kuibuka kwa aina mpya za uhalifu.
Mwenyekiti huyo, amesema kamati imeitaka Serikali iimarishe matumizi ya zana na vifaa vya kidigitali katika kazi za majeshi, huku wakipendekeza kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Kadhalika, kamati imeitaka Serikali kukamilisha mchakato wa kuanza kutumia mfumo wa Jamii Namba, ikieleza kuwa kufanya hivyo kutamwezesha mwananchi kuwa na namba moja ya utambulisho itakayoweza kutumika katika kila eneo.