Wenye ulemavu 250 wapata ujuzi wa kompyuta

Muktasari:

  • Zaidi ya watu 200 wenye ulemavu wa macho wamepata ujuzi wa kompyuta.

Dar es Salaam. Takriban watu 250 wenye ulemavu wa macho wamepata ujuzi wa awali wa kompyuta na Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kipindi cha miaka 10.

Ujuzi huo wameupata katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kinachoutoa bila malipo kwa wenye ulemavu huo.

Leo, Machi 22, 2023 wahitimu wanane wa taaluma hiyo wamekabidhiwa vyeti, ikiwa ni mara ya kwanza kutolewa tangu elimu hiyo ilipoanzishwa chuoni hapo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vyeti hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo, Teknolojia za kujifunza na Huduma za Mikoa, Profesa Alex Makulilo amesema hatua hiyo ni baada ya changamoto zilizokuwa zinawakabili wahitimu.

Amesema tangu kuanzishwa kwa elimu hiyo, wahitimu hawakuwa wanapewa vyeti badala yake waliishia kuwa na ujuzi pekee.

"Kwa sasa tumeona sasa tuwapatie vyeti vitakavyowasaidia kuvionyesha kama uthibitisho kwamba wana ujuzi walioupata OUT," amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia za Kujifunzia na Menejimenti, Dk Catherine Mkude amesema awali wahitimu hao walipata mkwamo kwenye maombi ya kazi kwa kukosa vyeti hivyo.

Amesema baada ya chuo hicho kulibaini hilo kimeamua kuanza kutoa vyeti watakavyovitumia kama ithibati ya kitaaluma.

Hata hivyo, amesema kwa miundombinu iliyopo chuo hicho kina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 20 kwa wakati mmoja.

"Mwanafunzi anasoma kwa mwezi mmoja hadi mitatu anakuwa amehitimu, tumeweka Musa huo kwa kuwa wenzetu wenye ulemavu wanaopaswa kufundishwa taratibu," amesema.

Ameeleza kwa kuwa Tanzania imejikita katika maendeleo ya kidigitali, chuo hicho kimewiwa kuanzisha programu hiyo kuwawezesha wenye ulemavu kunufaika na mabadiliko ya digitali.

Amesema mapato ya ndani,  ndiyo yanayotumika kugharimia mafunzo hayo kwa wanafunzi, kadhalika ufadhili wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Benadetha Msigwa ni mmoja wa wahitimu hao, amesema kabla ya vyeti ilikuwa vigumu kuomba kazi kwa kuwa hawakuwa na viambatanisho.

"Unaona tangazo la ajira unakuta kimeandikwa wenye ujuzi wa kompyuta watapewa kipaumbele, ujuzi tunao lakini huna kiambatanisho nani atakuamini, lakini sasa mambo mazuri," amesema.