Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri wa ardhi akabidhi hati 1,195 Mwanza, asisitiza umiliki kisheria

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo akizungumza na wakazi wa Kata ya Nyambiti wilayani Kwimba alipokuwa akikabidhi hati za kimila zaidi ya 527. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Dk Akwilapo amesema umilikishaji rasmi wa ardhi ndiyo suluhisho la kudumu la migogoro inayowakabili wananchi wengi vijijini.

Kwimba. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo amekabidhi jumla ya hati za kimila 1,195 katika vijiji vya Solwe Kata ya Nyambiti wilayani Kwimba na Lubuga, Kata ya Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza, akiwataka wananchi kumiliki ardhi kisheria ili kuondokana na migogoro pamoja na kuzuia kunyanyaswa na kuporwa haki zao.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa hati hizo Julai 6, 2026, Dk Akwilapo amesema umilikishaji rasmi wa ardhi ndiyo suluhisho la kudumu la migogoro inayowakabili wananchi wengi vijijini.

Amesema baadhi ya wananchi wanashindwa kupimiwa ardhi kutokana na kukosa namba ya kitambulisho cha Taifa (Nida), akisisitiza umuhimu wake katika kupata huduma mbalimbali za kiserikali.

"Unaweza ukaona huna uhitaji sasa, lakini mwanao akitaka kupata pasipoti ataulizwa baba yako ni Mtanzania? Akisema hana namba ya Nida, inaanza changamoto nyingine," amesema.

Aidha, ameonya viongozi wanaouza ardhi kinyume cha sheria akisisitiza kuwa ardhi ya kijiji si mali ya mtu binafsi bali inasimamiwa kwa niaba ya wanakijiji wote.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo akiwakabithi hati za kimila mke na mume  wakazi wa Kata ya Mabuki Wilayani Misungwi. Picha na Saada Amir

Amesema Serikali itaendelea na upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi huku asilimia 10 ya mapato ya kodi ya ardhi ikirejeshwa kusaidia shughuli hizo ili kupunguza migogoro.

Naye Kamishna wa Ardhi wa wizara hiyo, Nathaniel Nhonge amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wananchi.

"Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunawafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao na kuwapa elimu ya matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro," amesema.

Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, Wilson Luge amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kwa wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.

Amesema katika Mkoa wa Mwanza kuna vijiji 545, huku Wilaya ya Kwimba ikiwa na vijiji 119, lakini vijiji vyenye mipango ya matumizi ya ardhi ni 20 pekee, ambapo 15 tayari vimefikiwa.

Ameongeza kuwa jumla ya hati za kimila 10,300 ziko tayari kugawiwa kwa wananchi wa wilayani humo kwa awamu mbalimbali.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija amesema wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na migogoro mingi ya ardhi, hasa inayohusisha ndugu kwa ndugu na wajukuu wanaodai mali za urithi.

Amesema katika uzoefu wake wa miaka mitatu wilayani humo, migogoro mingi aliyokutana nayo ni ya kifamilia, ambapo baadhi ya watu hurudi vijijini wakidai kufuatilia makaburi ya ndugu zao lakini lengo likiwa kudai ardhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng'wilabuzu Ludigija akizungumzia namna wajukuu wanavyosababisha migogoro ya ardhi wakati wa ugawaji wa hati za kimila Kata ya Nyambiti. Picha na Saada Amir

"Lakini katika migogoro hii, kuna baadhi ya wananchi waliwahi kuishi katika maeneo haya zamani, labda miaka ya 60 au 70. Wanaporudi huanza kwa kisingizio cha kufuatilia makaburi ya ndugu zao, lakini lengo huwa ni kuibua migogoro ya ardhi," amesema.

Ameongeza kuwa migogoro mingine hutokana na mila ambapo mtoto wa mwisho hubaki nyumbani kuwahudumia wazazi na baadaye kurithi mali iliyobaki, lakini baada ya wazazi kufariki wajukuu hurudi kudai kugawana mali hiyo.

"Mimi nawaambia, kama mnataka kugawana hatuwazuii, lakini kusanyeni mali zote za familia ndipo mgawane kwa haki," amesema.

Amesisitiza kuwa suluhisho la migogoro hiyo ni wananchi kupima na kumiliki ardhi zao kisheria ili kuwa na nyaraka halali.

Kwa upande wake, Diwani wa Wala na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Elias Kapunda amesema wananchi wengi bado wanakosa elimu ya umiliki wa ardhi, hali inayochangia migogoro.

"Unakuta mtu anayenyang’anywa ardhi ni mzee, anashindwa kusafiri hadi Mwanza kufuatilia haki yake, hivyo tunaomba wasaidiwe kwa kupimiwa na kumilikishwa hati," amesema.

Wakazi wa Kata ya Nyambiti wilayani Kwimba wakifurahia wakati wa ugawaji wa hati za kimila walizokabidhiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo. Picha na Saada Amir

Wilayani Misungwi, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji, Grace Massawe amesema kupitia wadau mbalimbali wamefanikiwa kupima mashamba ya wananchi na kuandaa hati miliki za kimila 8,017.

Amesema katika hafla hiyo, jumla ya hati 668 zimetolewa kwa wananchi wa Kijiji cha Lubuga, Kata ya Mabuki, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupunguza migogoro ya ardhi na kuimarisha umiliki halali vijijini.